Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuwa mchangiaji wa kwanza katika Wizara hii muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeskiliza vizuri hotuba zote tatu, lakini kipekee napenda sana niwapongeze Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na Makatibu wao Wakuu pamoja na watendaji wote wa Wizara hii, kwa kazi kubwa ambayo wameifanya. Ipo kazi kubwa ya kuboresha miundombinu ya shule zetu zile kongwe ambayo imefanyika, kila mwenye macho anaona, kazi kubwa imefanyika, tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia taasisi ambazo wanazisimamia zipo taasisi ambazo zinafanya kazi nzuri, tunawashukuru sana. Na miongoni mwa taasisi hizo ni Bodi ya Mikopo; bodi hii tunaona kabisa kwamba sasa hivi inafanya kazi nzuri sana, tumeona kabisa wanafunzi sasa wanajielekeza kwenye masomo peke yake, hakuna mambo yale ya kugomea au ya kutafuta fomu za mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunawaomba pamoja na pongezi hizo lakini wazidi kuboresha kama ambavyo tumeendelea kushauri miaka yote, kwamba kwa kuwa hii ni Bodi ya Mikopo na ni mikopo, kama hata Mheshimiwa Rais amezungumza mara nyingi, basi ni vizuri hii mikopo isiwe na ubaguzi kwa maana ya mwanafunzi yeyote aweze kuwa na stahiki ya kuweza kupata mikopo kwa vigezo vile tu vya kitaaluma lakini visiwepo kwamba huyu sijui baba yake ni nani, huyu baba yake ni nani. Hii itakuwa ni nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze TCU; wamekuwa wanasimamia eneo hili vizuri, tumeona maboresho ya vyuo mbalimbali vikielekezwa kuboresha maeneo yao mbalimbali. Lakini niwashauri kwamba wasiwe sana wanafanya kazi kama matarishi, kama migambo, ni vizuri kwa kuwa hapa wanasimamia elimu wakae na wale wadau, haswa vyuo hivi ambavyo viko chini ya taasisi za dini, wazungumze nao, wawaelekeze na wawaelekeze mwelekeo wa Serikali unakotaka twende, lakini kuvifungia tu ama kuvinyang’anya baadhi ya kozi na kadhalika sio jambo zuri. Kwa hiyo, ni vizuri sana wakae na wadau hawa vizuri, hawa ni wadau wa maendeleo ambao wanasaidia katika Sekta hii ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Sera ya Elimu; juzi hapa niliuliza swali katika eneo hili linalogusa Sera ya Elimu, lakini majibu ambayo nimeyapata bado kwa kuwa ilikuwa kwenye swali nahitaji nipate ufafanuzi zaidi. Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 imeweka bayana kwamba elimu ya msingi itaishia Darasa la Sita na Naibu Waziri wakati analijibu akasema sera sio msahafu, lakini sasa japokuwa sio msahafu lakini hata mitaala inayotengenezwa inaishia Darasa la Sita. Maana yake ni kwamba wanafunzi wa Darasa la Saba ni kama wanakwenda kuota jua tu kwa mwaka mzima, wanapoteza muda. Kwa hiyo tunapenda tupate majibu yanayoeleweka; ni lini hii sera itatekelezwa kwa mujibu wa sera yenyewe ilivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, kwenye Sera ya Elimu vitabu bado ni tatizo. Hivi ninavyozungumza hapa Darasa la Tano mpaka sasa hivi bado vitabu vya huu mtaala mpya havijakwenda. Kwa hiyo, Serikali ituambie, hawa wanafunzi wa Darasa la Tano watasoma kwa vitabu gani? Maana wanaendelea sasa hivi tuko kwenye mwezi wa nne sasa, wanasoma vitabu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema juzi, kwamba sera sio msahafu inawezekana tukafika mpaka Darasa la Saba; sera hii mpya imefafanua kabisa kwamba mitaala ya elimu itaishia Darasa la Sita, hao Darasa la Saba watakuwa wanasoma mtaala upi maana hakuna kitu ambacho kimeandaliwa kwa ajili ya Darasa la Saba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo kwenye hiyo Sera ya Elimu pia tupate majibu ni mitaala ya shule za mchepuo wa Kiingereza. Mpaka sasa hivi kuanzia Darasa la kwanza mpaka la tatu bado hawana vitabu, inabidi wachukue vitabu hivihivi vya Kiswahili wafanye direct translation ambacho sio kitu kizuri. Kwa hiyo, tunapenda kuona kwamba kuna vitabu vya mchepuo wa Kiingereza ambavyo vimeandaliwa kwa ajili ya watoto hao wanaosoma mchepuo huo. Na Waheshimiwa Wabunge, kwa taarifa yenu hapa tunazungumza watoto wengi ambao ni watoto wetu sisi Wabunge na watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika suala la elimu nizungumzie suala zima la watoto hawa wanaosoma shule hizi za private, watoto wetu. Ukisoma Katiba, Ibara ya 13(4) – wewe ni mwanasheria mbobezi – inasema ni marufuku kwa mtu yeyote kubaguliwa na mtu au mamlaka yoyote inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria yoyote au katika utekelezji wa kazi au shughuli yoyote ya mamlaka ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hapa kuna ubaguzi wa wazi tunawafanyia watoto wanaosoma katika shule za private. Kwa sababu sasa hivi tuna elimu bila malipo kwa watoto ambao wanasoma shule za Serikali, lakini huku kwenye private wazazi tumekubali tunalipa ada, lakini kwa kuwa kuna ruzuku ambayo Serikali inatoa kusaidia watoto hawa wa shule za Serikali kwenye mitihani, basi hii iende pia kwenye shule za private kwa sababu na hawa ni watoto wa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa bahati mbaya sana – Mheshimiwa Waziri ulitazame hili kwa kina – katika utoaji wa elimu kuna wadau wakuu kama watatu; kuna Serikali yenyewe na wewe kama Wizara na TAMISEMI lakini na hawa private secor, hizi private schools nyingi ni shule za dini na kwenye shule za dini mara nyingi wanatoa elimu hii kwa watoto wale wegine ni yatima kabisa ambao hawana uwezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa watoto hawa hawana uwezo, mashirika ya dini yanasaidia kuchukua gharama zile za ada, Serikali ichukue jukumu tu hizi gharama ndogo ya kwenye ada za mitihani tuwasaidie ili waweze kuwa na usawa. Lakini hii haitakuwa haki kabisa kwamba hawa wanapata haki hawa wengine hawapati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu hii Taasisi ya Elimu Tanzania; nimesoma hapa katika hotuba ya Wizara, ukurasa wa 147 kipengele kidogo cha (4) anasema “Kuendelea na uandishi wa vitabu vya kiada kwa Darasa la Sita, Saba, Kidato cha Kwanza mpaka cha Sita na moduli kwa ajili ya Elimu ya Ualimu pamoja na kuandaa maudhui ya kielektroniki”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa changamoto iliyoko hapa ni kwamba mpaka sasa hivi mamlaka hii pia sisi tunadhani kwamba imeshindwa kwenye hili eneo la uchapishaji wa vitabu. Na hili eneo huko nyuma lilikuwa linafanywa na private sector, tumepitisha Sheria hapa ya PPP. Sasa nasikitika kuona kwamba mamlaka hii kwa maoni yangu bado haijafanya vizuri katika eneo hili, kwa nini msikae na hao wadau wa sekta binafsi ninyi mkawa tu kama mwongozo kama ilivyokuwa kwenye ile Bodi ya EMAC zamani ambapo wachapishaji binafsi walikuwa wanapewa miongozo wanaandaa, EMAC inafanya approval na mwisho wa siku kitabu kinakwenda sokoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake sasa hii ndiyo imetutia hasara kubwa ile ya vitabu ambavyo vimeondolewa katika mfumo, kwamba mamlaka yenyewe imechapisha vitabu, imeharibu na vimeondolewa katika mfumo. Lakini mpaka leo hatuambiwi ni hasara kiasi gani tumepata na nani amewajibika kwa hasara ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri hebu hili lione kwa sababu tumepitisha Sheria ya PPP tuboreshe hii idara vizuri, Taasisi hii ya Elimu Tanzania iwe na majukumu mahususi ili majukumu mengine tuwaachie sekta binafsi waweze kufanya ili kama kutatokea hata kama kuna makosa tunaondoka kwenye risk. Maana yake sasa hivi tatizo ni kwamba taasisi inapofanya yenyewe inachukua pia na risks zinapotokea. Kwa hiyo, nikuombe sana kama mwanzo kulikuwa na nia njema lakini kwa nia njema hiyo hiyo tukae na hao wadau tuwashirikishe tuone katika eneo hili tunatokaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)