Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Juma Othman Hija

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kukushukuru wewe kwa kunipatia nafasi hii ya kutoa mchango wangu kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mheshimiwa Spika, pili, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na wasaidizi wake wote kwa kutayarisha na kuwakilisha kwa umakini vizuri hotuba hii. Katika kuchangia hotuba hii, napenda kuchangia katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, miradi ya ujenzi wa makazi, Ofisi na Vituo vya Polisi; napenda kuipongeza Serikali kwa kutambua na kuthamini uwepo wa upungufu wa makazi na ofisi/vituo vya Polisi katika nchi yetu. Hili ni jambo jema ambalo litasaidia kuwapatia utulivu Askari wetu na kuweza kufanya majukumu yao kwa ufanisi.

Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ametuomba Waheshimiwa Wabunge tushirikiane katika ujenzi wa miradi hii. Ushauri wangu katika suala hili ni kumwomba Mheshimiwa Waziri kututafuta Wabunge katika hatua za awali ili kutambua kwa pamoja maeneo husika. Kwa mfano, katika hotuba yake ukurasa wa 12 ametaja mikoa ambayo itajengwa makazi ya Polisi lakini mkoa ni eneo kubwa ambalo lina majimbo zaidi ya moja. Kwa hivyo, ni vyema Mheshimiwa Waziri angetaja sehemu maalum yanapojengwa ili kutambua ni Mbunge gani anahusika katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, vitendea kazi; napenda kuipongeza Serikali kwa juhudi zake inayochukua kwa kuendelea kuwatafutia vitendea kazi Maaskari wetu. Vitendea kazi ni chachu ya ufanisi mzuri wa kazi zao. Ushauri wangu katika suala hili ni kwamba, Serikali izidi kuwatafutia vifaa vya kisasa kutokana na ukuaji wa matendo ya uhalifu vifaa ambavyo vitawarahisishia Askari wetu kuwatambua wahalifu kwa urahisi zaidi na kwa uhakika bila kubabaisha.

Mheshimiwa Spika, ajira kwa Maaskari; hivi sasa dunia inakabiliwa na tatizo kubwa la ajira kama inavyokabiliwa nchi yetu hivyo ni vyema Jeshi la Polisi likawa ni chanzo cha ajira katika nchi yetu. Ushauri wangu katika suala hili ni kwamba Serikali iwe makini sana katika kuchuja vijana ambao wanaoajiri ili kuepuka kuajiri vijana ambao hawana sifa na ambao huku nje ni wahalifu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.