Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kwa masikitiko makubwa nimepitia hotuba ya Wizara hii lakini sikuona mahali ambapo wamepongeza jitihada za wananchi wa Kata ya Mtae, Tarafa ya Mtae Wilaya ya Lushoto ambao kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wameweza kukarabati jengo la Serikali ya kijiji na kuwa Kituo Kidogo cha Polisi katika Tarafa. Wananchi kwa kushirikiana na Mbuge pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa na Wilaya kwa pamoja kituo kimeanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, aidha, vilevile kwa kuzingatia utawala bora na utawala unaozingatia sheria, wananchi wa Mtae wamewapatia nyumba ya kuishi familia mbili za Askari kati ya watatu waliopo katika eneo la kituo hiki. Napenda kuona Wizara hiii ikitoa japo neno la shukrani kwa wananchi hata kama ni wajibu wao katika kujiletea maendeleo.

Mheshimiwa Spika, mimi Mbunge wa Mlalo na timu yangu kupitia Mfuko wa Jimbo tumeweza kuchimba kisima katika Gereza la Kilimo Mng’aro ambalo lina uhaba mkubwa wa maji. Tumeweza kutumia takribani shilingi milioni 20 kuwawekea kisima kirefu pamoja na tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 5000. Tunatamani kuona Wizara ikishirikiana nasi katika kuboresha miundombinu ya Gereza hili ambalo limejengwa kwa tope na miti. Tunaomba Wizara itembelee Gereza hili la Kilimo cha Mpunga na Mbogamboga lenye uwezo wa kulisha wafungwa walioko katika Magereza ya Mkoa wa Tanga kwa asilimia 75.

Mheshimiwa Spika, bado jengo la Polisi katika Makao Makuu lipo katika hali mbaya na ujenzi wa jengo jipya ulisimama kwa muda mrefu. Tungependa kuona ni kwa kiasi gani jambo hili linafikia mwisho.

Mheshimiwa Spika, mwisho, napenda pia kushauri kuhusu Katibu Mkuu wa Wizara hii kusimamia mafungu mengi, hivyo kushindwa kuleta ufanisi katika Wizara hii. Afisa Masuuli wa Wizara hii ambaye ni Katibu Mkuu anasimamia Idara ya Uhamiaji, Idara za Zimamoto, Jeshi la Magereza, Jeshi la Polisi pamoja na NIDA.

Mheshimiwa Spika, naomba niwasilishe haya kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mlalo, basi angalau Wizara hii iweze kuwaunga mkono katika jukumu hili zito la ulinzi wa raia na mali zao.