Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Zainab Mndolwa Amir

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. ZAINAB M. AMIRI: Mheshimiwa Spika, awali naipongeza hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Kangi A. Lugola. Pia nampongeza Naibu Waziri, Mheshimiwa Eng. Masauni kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kutekeleza majukumu yao.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali kwamba bajeti inayopitishwa ifike kwa wakati ili kuweza kutekeleza shughuli ambazo zimepangwa kufanyika katika kipindi cha mwaka 2019/2020 ili kufikia malengo yaliyopangwa kufikiwa. Upelelezi wa kesi mbalimbali nashauri ukamilike kwa wakati ili kuweza kuondoa msongamano wa watuhumiwa katika Magereza na mahabusu nchini.

Mheshimiwa Spika, Vitambulisho vya Taifa vinachukua muda mrefu hadi mwananchi kupata. Nashauri huduma hii ya utoaji vitambulisho iboreshwe ili kuharakisha; kila Mtanzania anayestahili kupata kitambulisho hiki, apewe kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, vile vile nashauri Jeshi la Zimamoto lipatiwe vifaa vya uokoaji vya kutosha na vya kisasa ili kuweza kuharakisha uokoaji pindi majanga mbalimbali yatokeapo yaweze kushughulikiwa kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali iboreshe nyumba za Askari ili kuweza kuwa na makazi bora na ya kisasa zaidi maana nyumba zilizojengwa kwa mabati (full suit) zimepitwa na wakati.

Mheshimiwa Spika, pia naishauri Serikali kwamba kwa wanawake wafungwa wanaojifungua katika Magereza wapewe muda maalum wa kuwatunza watoto wao, pia wapunguziwe kazi ili kuweza kupata nguvu baada ya kujifungua.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali ipunguze gharama za hati za kusafiria (passport) maana sio Watanzania wote wana uwezo wa kugharamia kupata passport na ukizingatia passport ni haki ya kila Mtanzania bila kujali uwezo wake wa kipato.

Mheshimiwa Spika, pia naishauri Serikali itoe elimu ya kutosha kwa Polisi Jamii. Sungusungu wengi hawana mafunzo na elimu ya kutosha katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku. Hivyo hupelekea migogoro na wakati mwingine husababisha mauaji kwa watu wasio na hatia.

Mheshimiwa Spika, nashauri elimu itolewe kwa wanachi ili kuondoa mila potofu za kuua watoto, vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi kwa njia ya kujipatia utajiri.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali ijenge na iboreshe vituo vya Polisi ili kukidhi mahitaji. Pia kuwe na vitendea kazi hususan magari ili waweze kufika katika matukio kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na msongamano mkubwa katika vituo vya Polisi. Kutokana na shughuli za upotevu wa simu ili mwananchi kupatiwa Loss Report lazima aende Polisi. Hivyo, naishauri Serikali ianzishe kitengo maalum cha kushughulikia wananchi wanaokuja kuchukua Loss Report hususan za simu. Maana watu hujazana CRO na kusababisha wananchi wenye mahitaji ya dharura kushindwa kuhudumiwa kwa wakati, mfano, Dar es Salaam. Pia kiusalama katika vituo hivyo inakuwa siyo nzuri watu wa aina mbalimbali hujazana eneo moja kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, mwisho, namwomba Mungu azidi kuwapa afya njema Mheshimiwa Kangi na Naibu wake Mheshimiwa Masauni, pia umri mrefu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.