Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Sonia Jumaa Magogo

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuipongeza Wizara kwa wasilisho zuri, lakini pamoja na hilo, bado kuna changamoto kadhaa ambazo zinahitajika zaidi kuangaliwa na kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, nianze na vitambulisho vya uraia. Ni haki ya kila Mtanzania kupata kitambulisho hiki ambacho kimekua ni mojawapo ya sifa za kupata baadhi ya huduma za muhimu kabisa. Upatikanaji wake umekuwa ni changamoto sana. Ili kufanya zoezi hili kuwa rahisi, kwa nini vitambulisho hivi visiwe zoezi endelevu mfano mashuleni, vyuoni, sehemu za kazi hata Ofisi za Kata kiasi kwamba mtu anapotaka kupata kitambulisho hiki ni zoezi jepesi kuliko ilivyo sasa. Pia mianya ya rushwa iangaliwe sana ili kuondoa uzoroteshaji wa zoezi hili. Elimu itolewe kwa wananchi jinsi ambavyo anaweza kupata kitambulisho na umuhimu wake.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni wageni wanaokuja katika nchi yetu kufanya kazi za mikataba. Watu hawa mara nyingi wanajenga mahusiano na Watanzania wanawazalisha, mwisho wa siku wanaacha watoto bila malezi ya kueleweka na kuongeza watoto wa mitaani katika Taifa letu. Serikali iangalie inawasaidiaje hawa watoto wasio na hatia ili wapate malezi wanayostahili toka kwa wazazi wao.

Mheshimiwa Spika, pia wengine wamekuwa wakifunga miradi yao ghafla na kuacha wale waliowaajiri katika wakati mgumu na kukosa stahiki zao ikiwemo michango yao ya kila mwezi kwa Mifuko ya Hifadhi za Jamii. Mara nyingi kesi za namna hii zimekuwa zikichukua muda mrefu sana na hivyo kuwafanya waishi maisha magumu sana. Serikali iangalie ni namna gani inawabana katika mikataba yao ikiwemo aidha kuwa na bima ambazo zita-take off linapotokea tatizo kama hili.

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine ni suala la bima hasa za magari. Unapokwenda kukata bima, kunakuwa hakuna milolongo wala kucheleweshwa kwa namna yoyote ile. Ila unapopata ajali sasa ndiyo balaa juu ya balaa. Inachukua muda mrefu sana na wakati mwingine hadi watu wanaghairi kufuatilia, jinsi usumbufu unavyokuwa mkubwa. Mimi tayari nimepata ajali, sina usafiri na inachukua mwaka hadi miaka miwili mtu unafuatilia tu malipo. Sasa hamwoni kama badala ya kumsaidia huyu mtu mwenye matatizo, tayari ndiyo kwanza unamwongezea gharama ambazo hata baada ya malipo anakua amepata hasara kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, suala la ulinzi shirikishi ni muhimu sana kwa jamii zetu. Serikali isisitize zaidi juu ya suala hili ikiwezekana kuwe na utaratibu rasmi wa kuhakikisha ulinzi shirikishi unafanyika ipasavyo. Tumeona kumekua na matukio ya wizi majumbani hasa vifaa vya magari na magari yenyewe pamoja na matukio ya ujambazi na mauaji ambayo yanaweza kupungua zaidi au kutoweka kama suala la ulinzi shirikishi litawekewa mkazo.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuiomba Serikali izidishe elimu hasa Zimamoto majumbani, maofisini na mashuleni ili kupunguza au kuondoa kabisa majanga haya ya moto, wakati huo huo pia mazingira ya kazi ya maofisa wetu wa ulinzi yaboreshwe maana hawa watu ni muhimu sana kwa ustawi wa nchi yetu ili akili zao zitulie katika kazi ya ulinzi wa nchi yetu na wafanye kazi zao wakiwa na furaha.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.