Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Marwa Ryoba Chacha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Serengeti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye Wizara hii. Nina mambo machache na ninamwomba ndugu yangu Mheshimiwa Kangi Lugola, Waziri wa Mambo ya Ndani anisikilize. Naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Kangi Lugola, ni moja ya Mawaziri wanaofanya vizuri sana, hilo halina ubishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya Askari ambao hawana nidhamu walikuwa wanajaribu kuharibu Wizara ya Mambo ya Ndani; na Mheshimiwa Kangi Lugola bila aibu amekuwa akisema wazi wazi. Nampongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache. La kwanza naomba Kituo cha Polisi cha Mugumu na nyumba za Askari ni za siku nyingi. Kwa mfano, nyumba ambayo anakaa OCS, OCCID imechakaa sana. Naomba kwenye bajeti hii tusaidieni Polisi Mugumu waweze kukarabatiwa kituo na nyumba za Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge nimejitahidi, kulikuwa na shida ya choo, kupitia fedha zangu za Mfuko wa Jimbo niliwasaidia tukajenga choo na kibanda cha mlinzi. Halikadhalika Magereza walikuwa na nyumba zao tatu, mimi kama Mbunge niliwapa mabati na mbao wakapaua. Sasa Mheshimiwa Waziri niunge mkono tuwasaidie Magereza na Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni Zimamoto. Mheshimiwa Waziri watu wetu wa Zimamoto pale hawana ofisi, hawana vitendea kazi. Gari walilonalo limechoka ni la miaka mingi. Kama tunaweza tukapata msaada pale Serengeti, gari la Zimamoto lenye uwezo la kisasa itapendeza zaidi, maana nyumba zinaungua lakini kwa sababu ya udogo wa gari lile haliwezi kuhimili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa Mheshimiwa Kangi Lugola, Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, ni kuhusu Wakisii wanaoishi Rwamchanga. Jamii hii ya Wakisii imekuwepo kabla ya Uhuru, lakini hawajapewa nafasi ya kuwa raia wa Tanzania, wanaishi kwa vibali na hawaruhusiwi kupiga kura. Namwomba Mheshimiwa Waziri, ifikie wakati hawa Watanzania wenzetu wapewe fursa ya kuwa Watanzania kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma biblia kuna andiko linasema, utawezaje kukitoa kibanzi cha ndugu yako ilhali wewe bado una kibanzi? Labda tu nisome eneo hili, anasema, “basi mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au utawezaje kumwambia ndugu yako, ndugu yangu niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti ya ndani ya jicho lako mwenyewe. Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vyema kukitoa kile kibanzi kilichomo ndani ya jicho la ndugu yako.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewasikiliza kule ng’ambo…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema kuna ufisadi mkubwa ndani ya Jeshi la Polisi, CAG amekagua. Nami niwaulize, lile gari la CHADEMA mnafahamu ufisadi mlioufanya? Kama hamfahamu, acha niwaambie leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema kuna ufisadi mkubwa ndani ya Jeshi la Polisi, CAG amekagua. Nami niwaulize, lile gari la CHADEMA wanafahamu ufisadi walioufanya? Kama hawafahamu, acha niwaambie leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, gari linalosemwa alikopeshwa mwanachama fedha anunue gari ni uongo! Lile gari ni la CHADEMA, lile gari alipewa fedha Mbunge fulani yuko humu simtaji kwa sasa ila wakitaka nitamtaja; akapewa fedha kwamba yeye ndiyo anaenda kununua gari ili akwepe kodi. Kwa hiyo, chama kimekwepa kulipa kodi kwa kumtumia Mbunge kununua gari lile na ndiyo maana gari lile liko mpaka leo pale! Sasa niwaulize, mimi nimekuwa CHADEMA, ni lini chama kimekuwa na utaratibu wa kuwakopesha wanachama wake fedha? Lini? Eh, tuambiane hapa, wamekwepa kodi! (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba…

T A A R I F A

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nampa mzungumzaji anayeeleza kwamba kuna hoja inatolewa humu kwamba askari wameshindwa kulipa mishahara. Sasa kama chama husika na watu husika wanakwepa kodi, mishahara ya watumishi wanaowasema itatoka wapi? Nataka nimpe Taarifa. (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

MWENYEKITI: Ahsante. Endelea Mheshimiwa Ryoba.

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ile Taarifa ya CAG ni ya kweli. Alikopeshwa Mbunge mmoja hapa wa Viti Maalum tena ananiangalia yuko pale, alipewa hela, akaenda kuinunulia CHADEMA gari. Wamekwepa kodi na mkileta mchezo nitamtaja hapa! (Makofi/Kicheko) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

MBUNGE FULANI: Mtaje.

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwani si ni Sophia Mwakagenda?

MBUNGE FULANI: Kuhusu Utaratibu…

MWENYEKITI: Subiri Mheshimiwa Ryoba. Kanuni ya ngapi? Kanuni kwanza niambie. Nitajie Kanuni kwanza.

MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa Kanuni ya 64(1) kwamba Mbunge hatasema mambo ya uongo, yasiyokuwa ya ukweli ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti…

MWENYEKITI: Elezea basi vizuri niweze kuridhika kama kweli ameenda nje maana wewe ndiyo unalijua zaidi hilo suala.

MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa ya CAG inaeleza vizuri kwamba katika moja ya queries ambazo zilitolewa kwam ba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilinunua gari ambayo imesajiliwa kwa jina la mwanachama wake mmoja, lakini aliyetoa fedha ni chama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukweli ni kwamba anachokieleza Mheshimiwa Mbunge anayechangia sasa hivi ni uongo kwa sababu ukweli hauko hivyo, vitabu vya CAG vipo.

Sasa sisi tunamwomba au mimi namwomba athibitishe, alete huo ukweli kwamba chama kilitaka kukwepa kodi ndiyo kikatoa hizo fedha kupitia kwa huyo mwanachama na kama hatafanya hivyo ili taratibu ziweze kutumika, kwa sababu anachosema ni uongo. (Makofi)

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, ni masuala ya kanuni haya 64(1)(a) uliyoisoma lazima uisome na kanuni ya 63 kwa sababu aliyekuwa anaongea alikuwa ni Mheshimiwa Ryoba, amesema kitu ambacho kikafanya wewe ujisikie kwamba usimame kwa mujibu wa Kanuni ya 63(3) Kuhusu Utaratibu kwamba yeye hajasema kitu kilicho sahihi. Wewe kwa mujibu wa Fasili ya (4), Mbunge anayetoa madai kwa mujibu wa Fasili ya Tatu ya Kanuni hii atakuwa na wajibu wa kutoa na kuthibitisha ukweli kuhusu jambo au suala hilo kwa kiwango cha kuridhisha Bunge. Sasa huo wajibu au ule mzigo wa kuthibitisha sasa ulihama kutoka kwa Mheshimiwa Ryoba kuja kwako. Umejaribu kuelezea lakini hukufikia sasa kile kiwango cha kutofautisha pale ambapo yeye yupo tayari kumtaja maana hoja hapa ni kwamba ilikuwa ni scheme ya kukwepa kodi. Sasa tusaidie hapo ili sasa nirejee kwake. (Makofi)

MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, source yake ni CAG kama alivyosema. Katika Taarifa ya CAG hakuna mahali popote ambapo CAG amesema CHADEMA ilitaka kukwepa kodi na CHADEMA imetoa maelezo kwamba kuna mwanachama ambaye aliagiza gari akashindwa kulikomboa, chama kikamkopesha fedha akalinunua na hilo gari liko pale kwenye Chama na CAG ameliona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo suala hapa ni kwa nini halijahamishwa kutoka kwa yule mwanachama aliyekopeshwa kuja kwenye chama, lakini hakuna suala la kukwepa kodi. Sasa hiyo ya kukwepa kodi anatoa wapi? Hiyo ndiyo tunataka athibitishe na akishindwa kuthibitisha afute hiyo kauli, vinginevyo atakuwa anasema kitu ambacho sio sahihi. (Makofi)

MWENYEKTI: Ahsante. Mheshimiwa Ryoba.

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Komu yuko sahihi kabisa na bahati nzuri Mheshimiwa Komu na Mheshimiwa Kubenea wako kwenye matazamio chini ya Kamati Kuu, maana…

MWENYEKITI: Mheshimiwa, jibu tu hilo.

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, amenisaidia. Ni kweli kwamba alikopesha mwanachama na alikwepa kodi, kwani si Sophia Mwakagenda, alilipa wapi? Kama mimi ni mwongo, gari hilo mpaka leo liko kwenye chama, ni la chama sio la mwanachama! Mwanachama katumika tu kukwepa kodi! Kama mimi mwongo thibitisha wapi mlilipa kodi. (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme Komu na Kubenea walitoa tuhuma dhidi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Mbowe, kwamba anakula ruzuku!

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MHE. MARWA R. CHACHA: … na wako chini ya Kamati Kuu kwa uangalizi na wakavuliwa nafasi zao zote! (Makofi)

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, naona huo sio utaratibu mzuri wa matumizi ya muda wetu wa Bunge. Ningependa sasa Mheshimiwa Ryoba, nisaidie tu kwa sababu na mimi lilikuwa linanisumbua sana hilo suala la kwamba kulikuwa na scheme ya kukwepa kodi. Sasa kama kwenye CAG Report hakuna kitu cha namna hiyo, nisaidie tu ondoa hiyo scheme ya kukwepa kodi, tubaki tu katika utaratibu wetu.

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo haina shida kwa sababu jinsi gari lilivyoingia…

MWENYEKITI: Ondoa tu hiyo nanihii. Nisaidie ondoa hiyo ya kukwepa kodi.

MHE. MARWA R. CHACHA: Naondoa, lakini tutafuatilia zaidi. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Kwa hiyo niseme huwezi ukawa unanyoosha tu kidole, ondoa boriti ya kwako kwanza. Sasa wewe hujaondoa ya kwako unasema! Hapa ngoja nikwambie, hawa Wabunge wewe unaowaona kule ng’ambo wana shida! Mbunge wa Viti Maalum kila mwezi shilingi 1,500,000 na hawajui zinafanya kazi gani na tunavyoongea hata matumizi ya ruzuku niambieni Katibu gani wa CHADEMA wa Jimbo au wa Wilaya anayelipwa na ruzuku ya CHADEMA? Hela inaliwa na wachache pale Makao Makuu.

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nashukuru.