Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Nataka kuchangia sana kwenye uhuru wa vyombo vya habari; najua kabisa kwamba katika Taifa hili sasa hivi kutoa habari imekuwa ni jambo hatari sana kuliko hata ugaidi.

Mheshimiwa Spika, nizungumze tu ukweli kwamba wako vijana wetu wengi sana ambao wamepata shida kubwa wamepigwa, wamewekwa mahabusu, wameteswa, wamekaa rumande zaidi ya miezi mine na bila kupelekwa Mahakamani na baada ya kupelekwa Mahakamani wameshinda kesi zao zote, lakini bado wana maumivu na vilema wamebaki navyo. Natoa mfano, kwa mfano, kijana mmoja anaitwa Mdude Nyagali ambaye yeye alikuwa anakosa kwenye mitandao, anakosoa utendaji wa Mheshimiwa Rais na kutoa maoni yake, huyu mtu alikamatwa usiku, alipigwa, alisafirishwa kutoka Mbozi mpaka kwenda Dar es Salaam na alikaa Dar es Salaam zaidi ya miezi miwili huku akiwa amepigwa, amevunjwa miguu yake na akiwa hoi kabisa.

Mheshimiwa Spika, pia wako vijana wengi sana ambao wamekamatwa na vijana hawa mpaka sasa hivi wengine hawajapelekwa Mahakamani, lakini mpaka sasa hivi bado wanaendelea kukamatwa. Tunaomba sana wakati Waziri anakuja kuzungumza hapa, aje atuambie ni vijana wangapi ambao wamekamatwa katika Taifa hili kwa sababu ya makosa ya kimtandao wakati wanatoa maoni yao kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanaijenga nchi hii.

Mheshimiwa Spika, vilevile atueleze kwamba ni vijana wangapi ambao wamefunguliwa mashtaka na wamefungwa gerezani kwa sababu wamepatikana na hatia. Yote hii tunataka kujua ni namna gani nchi yetu ilivyoweza kuzuia uhuru wa vyombo vya habari.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, ninataka kuzungumzia, yuko Mwandishi wa habari ambaye anaitwa Ansbert Ngurumo ambaye alikuwa anajaribu kuandika habari, kuwapasha habari Watanzania huyu mtu alianza kutishiwa kwamba anatoa habari ambazo zinaweza zikasababisha utulivu na amani ukatoweka katika nchi hii, huyu mtu aka…

SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka vitu vingine una uhakikanavyo lakini?

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, nina uhakika. Hii ya Ansbert Ngurumo nina uhakika nayo, hayupo yupo Finland na alitoa…

SPIKA: Huko Finland na sisi, si kaenda mwenyewe!!

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: No, analalamika…

SPIKA: Haya andelea kuchangia

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, anazungumza kwenye vyombo vya habari. Haya tunayotoa ni mawazo, tunatoa ushauri humu ndani ya Bunge, nia na madhumuni ni kuona Serikali inafanya mabadiliko, nia na madhumuni ni kuona Serikali inaacha uhuru wa vyombo vya habari, inaacha Watanzania wanatoa habari na wanatoa maoni yao kwenye Taifa letu. Nchi haijaanza leo, nchi imeanza muda mrefu, hii ni Awamu ya Tano ya Serikali katika Nchi hii ya Tanzania. Serikali zote zilizopita sheria zilikuwepo lakini Serikali ya Awamu ya Tano imetunga Sheria nyingi za makatazo, sheria nyingi ambazo zimesababisha…

SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka subiri kidogo. Naamini Waheshimiwa Wabunge mnapotaka kuchangia mnajiandaa. Ukitaka tu kuchangia unasimama tu, Serikali haitungi sheria anayetunga sheria ni ninyi wenyewe. Tunaotunga sheria ni Bunge, ukisema Serikali hii imetunga sheria nyingi, imefanya hivi unakuwa unawasingizia lakini cha muhimu hapa cha kuelewa; uhuru wa kutoa maoni siyo uhuru wa kwamba sisi tukishakuwa Wanasiasa ni kutukanwa na kila mtu, kusingiziwa na kila mtu, yaani ukishakuwa Mwanasiasa basi kosa. Mtu akutukane, akudhalilishe, afanye anachofanya, ukimuuliza nini anasema uhuru wa habari, hapana, hakuna uhuru huo.

Hivi wewe ukitoa maoni yako, ukayatoa tu maoni yako ukapinga jambo, ukafafanua jambo utagombana na nani? Tatizo when they go to the person na ili tuwafundishe vijana wetu wote tuna wafuasi hapa, tuwafundishe namna ya kutoa maoni yao badala ya kutumia kichochoro hicho cha uhuru kutukana watu, kudhalilisha, watu wana familia zao, tuna utamaduni wetu katika nchi, tunaheshimiana. Kitoto kidogo kinatukana mtu kama babu yake au baba yake itakuwa Taifa la aina gani hilo? (Makofi)

Kwa hiyo tunapoilaumu Serikali, mimi sikatai, lakini vilevile tuna jukumu sisi la kuwalea vijana wetu wajue hata kukosoa kwenyewe kuna utaratibu wake, kuna nidhamu yake. Unapotaka kuiambia Serikali iambie katika utaratibu fulani lakini unapomtukana mtu anafunga masikio, hasikilizi. Yaani kuwa kiongozi ndiyo basi utukanwe tu kukicha? Haiendi hivyo.

Ndiyo maana naishia kwa kuwashukuru sana wale wanaoliombea Taifa hili, tumemaliza Pasaka vizuri, nawashukuru sana Watanzania walioliombea Bunge na waendelee kuwaombea viongozi. Ndiyo viongozi tunakosea lakini pia huombewa si lazima uwe unatukana tu kila siku, upige na magoti kidogo tuweze kuiona njia vizuri zaidi kama nchi tusonge mbele. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, nawaonea huruma sana kwani mnatukanwa sana, mnadhalilishwa sana bila hatia. Mtu hata hajui chochote, hana information yeye mwenyewe lakini uhuru wa habari, huu ni utamaduni wa wapi wa kutukana watu hovyo?

Mheshimiwa Mwakajoka, mimi sipingi hoja yako na dakika nazitunza, nachosema ni kwamba tuna wajibu na sisi wa kuwafundisha hawa vijana waache habari ya kutukana watu. Endelea Mheshimiwa Mwakajoka. (Makofi)

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru tu kwa kutoa ufafanuzi, lakini niseme ukweli tu kwamba nachoshangaa ni kwamba mnajitahidi sana kusimamia hali halisi hasa tukizungumza sisi, hebu tuchukulie mfano Gazeti la Jamvi kila siku linatukana Watanzania, Mheshimiwa Waziri yuko hapa, kila siku linatukana viongozi wa Vyama vya Upinzani, kila siku wanazungumzia akina Mheshimiwa Membe na kadhalika yaani kila siku linatukana, hata siku moja hatujaona hatua yoyote inachukuliwa. Sasa yote haya tunavyosema kwamba tunataka tuone nchi yetu inakuwa na utulivu na inafuata misingi hasa ni misingi gani watu wengine wanatukanwa tuko kimya na kila siku tunazungumza humu ndani ya Bunge. (Makofi)

SPIKA: Yaani hilo tunakemea kwa pamoja, mimi na wewe tuko pamoja.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, tunazungumza ndani ya Bunge, Mheshimiwa Waziri yuko pale lakini hakuna hata siku moja kwamba hili Gazeti limefungiwa au limechukuliwa hatua yoyote kwa sababu tu hili gazeti inasemekana kwamba watu wanaolihudumia ni Serikali yenyewe, sasa hatuwezi kufika huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana Mheshimiwa Profesa Shivji amezungumza kwenye mtandao, akasema wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza tulipewa uhuru wa kutoa mawazo na uhuru wa kusema na wakati tunasema Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Kwanza alivyosikia aliwatuma watu wake waje watusikilize, walitusikiliza, tukawaeleza na wakatuelewa vizuri. Leo Tanzania mtu akitoa mawazo na maoni yake amekuwa ni adui, hilo jambo halitawezekana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka Profesa Shivji amezuiliwa na nani kuongea?

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, no, amesema hivyo lakini hata ukisikiliza jana na hotuba…

SPIKA: Kama anasema hivyo anazeeka vibaya Profesa. Endelea Mheshimiwa Mwakajoka. (Kicheko)

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ukisikiliza Maaskofu wote waliohubiri siku ya Pasaka wamezungumzia jambo hili kwamba Tanzania uhuru wa habari kwa kweli imekuwa ni tatizo, ni lazima Serikali ikubali kupokea mawazo na maoni, iache uhuru wa vyombo vya habari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tuko ndani ya Bunge pamoja na kwamba mlipiga kura nyingi humu mkasema Bunge lisiwe live lakini ukweli tu ni kwamba Watanzania wanahitaji sana kuona Wabunge wao wanasema nini lakini jambo hili limefungwa. Mambo mengi ambayo tunayazungumza ndani ya Bunge ambayo ni maslahi ya wananchi yamefungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi tumepata taarifa kwenye mitandao na vyombo vya habari, IMF wamesema kwamba wanatakiwa waruhusiwe tu na Tanzania watoe habari ya jinsi gani uchumi wa nchi yetu unakwenda lakini mpaka sasa hivi kimya. Tunaomba pia Mheshimiwa Waziri aseme hii ni kwa sababu ya kutokuwa na uhuru wa vyombo vya habari. Vyombo vya habari vinaogopa kuandika kwa sababu wanasoma kwenye mitandao lakini wanasema wakiandika na kama hawajaruhusiwa inakuwaje. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka, una uhakika IMF imeomba itoe habari?

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: IMF ndio imeomba?

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, wameomba Serikali ya Tanzania iwaruhusu ili wachapishe ile hali ya uchumi wa nchi yetu kwa jinsi ambavyo wameiangalia. Wamezuiliwa, wameambiwa wasitoe. Sasa kama mmezuia na taarifa hiyo na walipa kodi wanataka kujua kuhusu kinachoendelea.

SPIKA: Yaani Tanzania ina uwezo wa kuwazuia IMF wasichapishe chapisho lao?

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ni sheria lazima nchi husika iruhusu, sasa Tanzania haijaruhusu…

KUHUSU UTARATIBU

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, Kuhusu utaratibu.

SPIKA: Kuhusu utaratibu Mheshimiwa Mwakajoka.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, anatuchelewesha.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika,
kuhusu utaratibu, natumia Kanuni ya 64(1)(a) ambayo inasema kwamba Mbunge hatatoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina ukweli.

Mheshimiwa Spika, ndani ya Serikali tunachojua sisi bado tunaendelea kufanya mazungumzo na IMF kuhusu ripoti hiyo na si kweli Tanzania imezuia ripoti hiyo isitolewe. Sasa naomba kwa kuwa mimi nafahamu na Waziri wa Fedha yuko hapa anafahamu na ana maelezo ya kutosha tu kuhusu jambo hilo ambalo linapotoshwa na Mheshimiwa Mwakajoka, naomba ama Mheshimiwa Mwakajoka afute hizo statement zake za kuituhumu Serikali kwamba imeficha hiyo ripoti na haitaki ripoti hiyo itolewe au alithibitishie Bunge kwamba taarifa anazozisema ni sahihi na ripoti aliyonayo ni sahihi na hakuna jambo lolote ambalo linaendelea kwa sasa ndani ya Serikali. (Makofi)

SPIKA: Alichokisema Mheshimiwa Mwakajoka kidogo tu, unless unisahihishe Mheshimiwa Mwakajoka, alichokisema Mheshimiwa Mwakajoka ni kwamba Tanzania imewazuia IMF wasitoe hiyo taarifa yaani IMF inaomba kibali halafu IMF imezuiliwa Tanzania isichapishe hiyo ripoti, ndio jambo alilolisema. Mheshimiwa Waziri wa Fedha.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Katika majadiliano ambayo yanaitwa Article Four Consultations, Timu ya IMF ilikuwa hapa nchini kuanzia tarehe 26 Novemba mpaka tarehe 7 Desemba, 2018. Baada ya pale walitoa taarifa na kwa utaratibu ni kwamba wakitoa ile rasimu ya taarifa inarudi Serikalini ili tuweze kuitolea maoni na wao waweze kuyazingatia kabla ya kuichapisha ripoti hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ripoti hiyo nilikuja kuiona tarehe 18 Machi. Hata hivyo, baada ya kuwa sisi tumepeleka maoni yetu lakini tuliona hayajazingatiwa kwenye taarifa hiyo. Nilipokuwa Washington juzi zilizungumza na Bwana Abebe Selassie, Mkurugenzi wa African Department na mpaka leo saa tisa bado tutaendeleza majadiliano kuhusu jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa utaratibu ni kwamba baada ya Executive Board ya IMF kuijadili taarifa hiyo, Serikali inakuwa na siku 14 za kuipitia na kusema itolewe au isitolewe. Kwa hiyo, wasiwahishe mjadala Serikali bado inazungumza na IMF na hakuna sehemu ambayo tumezuia ni utaratibu wa IMF yenyewe. (Makofi)

SPIKA: Tuendelee Mheshimiwa Mwakajoka, nafikiri imekusaidia.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, mimi nashukuru tu kwamba Mheshimiwa Waziri wa Fedha amekubali kwamba ni kweli maoni yao hayakuzingatiwa na ndiyo maana hawajaruhusu. Kwa hiyo, sikuwa muongo kama alivyokuwa anazungumza Chief Whip pale Mheshimiwa Mhagama, niko sahihi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, liko jambo lingine ambalo nataka kulizungumza hapa, tumezungumzia uadilifu katika nchi. Kuna gazeti lingine linaitwa Tanzanite. Gazeti hili limekuwa linaandika matusi kila siku ya Mungu, kuwatukana viongozi, kuwagombanisha watu, kuwaita watu magaidi na mambo mengine, mabaladhuri sijui namna gani, wanataka kupindua nchi, hawa watu wanatakiwa kuuwawa lakini Serikali iko kimya inatazama tu. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka, Tanzania Daima nayo mbona hulitaji?

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, aah, aah, unaona sasa?

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, unataka kuniambia kwamba tusizungumze kwa sababu Tanzania Daima hatujalizungumza?

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, lakini haya tunayokuambia unapaswa kuyachukulia hatua.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, kama kuna vijana wanapigwa na wananyanyaswa kwa sababu tu ya kuandika kwenye mitandao lakini leo gazeti …

SPIKA: Mheshimiwa Msigwa unamsumbua Mheshimiwa Mwakajoka dakika zake zinapotea.

MHE. MCH. PETER SIMON MSIGWA: Mheshimiwa Spika, utaratibu ni kanuni.

SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka endelea.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu.

SPIKA: Wewe ulikuwa unataja magazeti nikakuongezea na lingine, endelea Mheshimiwa Mwakajoka.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, gazeti linaandika, wewe unatuambia leo hapa kama Kiongozi wa Mhimili ambapo tulitegemea ungekuwa unatoa maamuzi mazuri kwa sababu umepewa uongozi...

SPIKA: Mimi nimekuongezea kwenye idadi yako tena unanilaumu kwa sababu nimetaja? (Kicheko)

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, umetoa mwongozo mzuri hapa ukasema Mheshimiwa Mwakajoka ulipaswa kuzungumzia kuhusiana na hali halisi kwamba watu wasitukanwe lakini tunaona magazeti haya yanatukana watu, wanasema watu wanyongwe. Wameongeza watu, wanamtaja Mheshimiwa Heche, sijui nani kwamba hawa watu ni hatari wanyongwe, wanataja watu wanyongwe. Hivi kweli nchi hii mnakubali kwamba ni kweli kwa sababu ya mtu kutoa maoni yake, kuzungumza ndani ya Bunge au kwa kuonyesha msimamo wake huyu mtu anastahili kunyongwa? (Makofi)

SPIKA: Bado dakika moja.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, lazima tukubaliane kwamba haya lazima tuyachukulie hatua na tusifananishe na kitu kingine. Ndiyo maana umesema kwamba tusiendelee kufananisha vitu ni lazima tuchukue hatua. Naomba pia hatua zichukuliwe, kama Mheshimiwa Waziri atashindwa kuzungumza kuhusiana na jambo hili tutaona kabisa kwamba hili gazeti ni la Serikali na wanatumwa kufanya hivi. Serikali inayoweza kuwatuma waandishi wa habari wakaandika vitu vya hovyo namna hii, hii Serikali itakuwa dhaifu sana na tunakoelekea kutakuwa siyo kuzuri hata kidogo. (Makofi)

SPIKA: Unakoelekea sasa, Mheshimiwa Mwakajoka. (Kicheko)

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahaa, nimeisema Serikali siyo wewe, siyo mhimili wetu Mheshimiwa, huu nauheshimu. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Endelea, malizia. (Kicheko)

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumza ni kuhusiana na mambo ya michezo. Kwenye nchi hii tunapenda sana michezo na Serikali imekuwa inashangilia sana tunaposhinda.

Mheshimiwa Spika, cha kushangaza hivi juzi Taifa Stars imeingia AFCON tumemsikia Mheshimiwa Polepole anasema kwamba hii ni Ilani ya CCM. Sasa juzi tumepigwa mechi tatu zote mfululizo sijui Ilani ya CCM imeshindwa, maana sasa tunaingiza siasa kwenye michezo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, sasa mimi nataka nijue Ilani ya CCM imeshashindwa tayari maana tumepigwa mechi zote tatu. Tukishinda Ilani ya CCM, tukipigwa hamsemi, yuko kimya Polepole. Naomba pia mumwambie ajitokeze aseme Ilani ya CCM imeshindwa ili Watanzania wajue kwamba Ilani ya CCM imeshindwa kwenye mechi hizi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine …

SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka, mimi Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM. (Makofi)

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ndiyo, ila unajua siasa zikiingia kwenye michezo haiwezi kuwa bora hata siku moja. Tunachohitaji ni kukaa pamoja, ushindi wa Timu ya Taifa ni wa pamoja, ni wa Watanzania wote wanashangilia, wanafurahi kwa pamoja lakini inavyotokea…

SPIKA: Kengele ya pili Mheshimiwa Mwakajoka. (Kicheko)

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Katibu, Katibu, Katibu.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mwakajoka Frank. Mheshimiwa Frank bwana kila akisimama anatupiga kweli kweli bwana. (Makofi/Kicheko)