Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nami namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kusimama hapa kuchangia katika hoja hii iliyo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilimsikia Waziri wa Mambo ya Nje, Mheshimiwa Profesa Kabudi akiisifia nchi yetu juu ya mafanikio na sifa waliyoipata duniani kutokana na uhuru wa vyombo vya habari. Juzi alikuwa akizungumza hapa na aliisema nchi yetu kwamba imepokea sifa kwa uhuru wa vyombo vya habari. Moja kati ya eneo alilolizungumzia ni kwamba Tanzania imesifiwa kwa kuwa na idadi kubwa sana ya magazeti. Kwa hiyo, hiyo ilikuwa ni sifa moja kubwa sana kwa Taifa letu, nadhani alikuwa akieleza aliyokutana nayo huko nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, siku mbili baadaye tumemsikia Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo akiyataka magazeti yaliyoripoti taarifa aliyoitoa Kiongozi wa Chama cha ACT cha majirani, kwamba waende wajieleza kwa namna walivyochambua taarifa ile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo kwa kweli limetupa mashaka. Anakwenda duniani anapata sifa juu ya uhuru wa vyombo vya habari, lakini nyumba yake Serikali, vyombo vya habari kuripoti taarifa ambayo ilitolewa siyo taarifa ya msituni, ni taarifa iliyokuwa public na ya wazi ambayo vyombo vya habari wana haki na ni moja katika kutimiza majukumu yao katika kuwaelimisha Watanzania ni nini kimezungumzwa na kiongozi yule wa chama cha siasa. Hilo limekuwa ni kosa; na wenzetu wahariri wa wahabari wanakiwa wajieleze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaposifiwa, ni kwa lipi? Tunaporudi, tunafanya nini? Maana inakuwa hatueleweki. Leo vyombo vya habari vinatakiwa vijieleze kwa kosa lao, lipi? Watu wa habari, wanalipwa mishahara, wanafanya kazi kwa kutengemea habari zinazotoka wawaelimishe Watanzania ni kipi kinachoendelea katika nchi. Inatokea sasa tayari Msemaji Mkuu na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Dkt. Hassan anavitaka vyombo vya habari vileze hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kusikitisha zaidi; na Mheshimiwa Waziri naomba unisikilize; yapo mambo ambayo kama Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na wewe Waziri, mngevitaka baadhi ya vyombo vya habari vijieleze, ni muhimu zaidi. Kwa mfano, kuna vigazeti fulani hapa, kimoja kinaitwa Jamvi la Habari na kingine kinaitwa Fahari yetu na kingine kinaitwa Tanzanite. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi vigazeti kazi yake kubwa kuchafua watu, kufitinisha watu, kuleta ugomvi baina ya watu. Mheshimiwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari hajawahi kuviita, hajawahi kuwaita Wahariri wa Magazeti haya akawaambia njooni mjieleze kwa namna namvyowachafua watu. Wamewachafua watu wengine tunaowaheshimu sana ndani ya nchi hii. Mfano, Comrade Kinana, huyu mtu muhimu kwenye nchi hii, lakini amechafuliwa na watu hawa, lakini hakuna Mkurugenzi wa la Waziri ambaye amemwita Mhariri wa Gazeti hili, Mkurugenzi wake Musiba mkamwambia ajieleze kwa namna ambavyo anawachafua watu. Kwa nini haitwi? Yuko nyuma ya nani anayejiamini mpaka aweze kumchafua yeyote? Yeyote kwenye nchi hii Musiba akiamua kumchafua anachafua na hakuna lolote linakuwa. Yupo nyuma ya nani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilidhani watu kama huyu ndio wangeitwa wakajieleza, wakaelekezwa, TCRA wakamwelekeza kama anachofanya sicho, lakini yeye yupo huru. Watu wengine wakitoa kwenye mtandao maoni tofauti kidogo na Serikali, wao wataishia kupelekwa sehemu kushitakiwa na wengine kwenda kufungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa tunafanya nini? Mimi nataka hili lizingatiwe.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. KHATIB S. HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khatibu kuna taarifa. Mheshimiwa Mlinga.

T A A R I F A

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Anayoongea Mheshimiwa Khatib ni kweli, ila amesahau kuna kijigazeti kimoja kinaitwa Tanzania Daima na chenyewe kazi yake ni kuchafua Serikali pamoja na watu. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khatibu Haji, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. KHATIB S. HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wapemba tuna mila moja, yule kijana Bunge lililopita tuliishi na mama yake, kwa hiyo, mimi namchukulia kama mwanangu, siwezi kumjibu. (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khatib, mama yake alikuwa ameshafariki wakati huo, nadhani una hiyo taarifa. Sasa sijajua umekuwa umeishi naye wakati gani.

Waheshimiwa Wabunge, kuna mambo ambayo mnaweza mkafanya utani na kuna mambo ambayo siyo ya utani. Kwa hekima kabisa na heshima ambayo mnaitwa Waheshimiwa, Mheshimiwa Khatib tafadhali, huyo mama amefariki na ninaamini wewe ni sehemu ya watu ambao umefanya naye kazi.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tuwe tunasikilizana. Hata wewe angekuwa ni mama yako anayezungumziwa hapa ningesema vivyo hivyo ninavyozungumza sasa hivi. Mheshimiwa Khatib, tafadhali mtunzie Marehemu heshima yake.

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, sikuwa na nia mbaya, lakini kama limekwaza, naomba nifute hilo neno. Naomba kuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niendelee na fungu kuhusu mgao wa fungu na fedha zinazotoka FIFA kwa Tanzania. Kuna siku nimewahi kuuliza swali; na katika hili Naibu Waziri alinijibu sijui kwa makosa au kwa bahati mbaya; akasema ZFA ipo chini ya TFF, jambo ambalo siyo kweli. TFF ni chombo mbali, Wizara ya Habari na Michezo Zanzibar, ni kitu mbali; na Wizara ya Michezo Bara na TFF ni kitu mbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ZFA ipo Zanzibar chini ya Wizara ya Habari na Michezo Zanzibar na TFF ipo hapa chini ya Wizara ya Michezo. Ni vyombo ambavyo havina mwuingiliana wa kisheria wala kikatiba. Hapa linalojitokeza ni kwamba mara nyingi sana tunapolilia juu ya haki ya Zanzabar katika vitu vinavyopatikana ambavyo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati mwingine tunahisiwa kama sisi ni walalamishi sana, lakini hayo tuliyoyapata na faida zilizotokana na mengine tuliyoyalalamikia, bila shaka kulikuwa na haki ambayo labda ilikuwa imejificha sehemu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kazi yetu moja iliyotuleta hapa Wabunge wa Zanzabar ni kutetea maslahi ya Zanzibar kwenye Muungano. Kama wapo Wabunge wametoka Zanzibar wamekuja hapa, mfano ndungu yangu Ally King, kama yeye amekuja kucheza taarab, atacheza taarab; lakini sisi tuliokuja kutetea maslahi ya Zanzibar, tutatetea maslahi ya Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hakuna mgao halali kutoa fungu la FIFA. Mheshimiwa Mwakyembe hili naliomba leo anapohitimisha aliweke wazi, kwa sababu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inajumisha nchi mbili; Zanzibar na Tanganyika.

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mattar.

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpe taarifa kaka yangu Mheshimiwa Khatib, Mheshimiwa Ali King hakuja Bungeni kucheza taarab, Mheshimiwa Ali King ni Mbunge ambaye kachanguliwa na wananchi wake wa Jimbo la Jang’ombe kuja kuwatetea. Namwomba sana Mheshimiwa Khatib aweze kurekebisha maneno yake ambayo ameyasema na afute kauli yake ahsante.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khatib.

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, najua Mheshimiwa Ali King aliletwa hapa kama nilivyoletwa mimi, lakini pia nami nimeletwa hapa kuwakilisha, lakini navuta Mchezo wa Kamba na tunachukua kombe kule Burundi na nchi nyingine tofauti. Kwa hiyo, hii ni michezo na hii michezo imo humu, unakataa nini? Kwa hiyo, kama yeye nyanja yake ni taarab, mimi nipo kwenye kuvuta kamba, timu simika. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili jambo namwomba Mheshimiwa Waziri, hebu akutane na wenzie wa Zanzibar tuone kile kidogo kinachopatikana kutoka FIFA na sisi Wazanzibar tunafaidika nacho vipi? Ile ni haki ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hiyo, Watanzania wote wanapaswa kufaidika na mgao ule wa FIFA kwa Zanzibar. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

T A A R I F A

MHE. KHATIB SAID HAJI: Leo hamtanipa nafasi, Pasaka hii. Naomba nimalizie muda wangu.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge hii itakuwa taarifa ya mwisho kwa Mheshimiwa Khatib, Mheshimwa Nyongo.

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Khatib kwamba ZFA ni mwanachama wa TFF (Tanzania Football Federation) kama mikoa mingine ya Tanzania ilivyokuwa wanachama. Kila Chama cha Mpira ni mwanachama wa Tanzania Football Federation; na vilevile, kwa mfano, naomba nitoe mfano…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Mpeni nafasi amalize, Mheshimiwa Zitto naomba ukae, unazifahamu kanuni. Mpeni nafasi amalize, naomba mkae anazungumza. Kaa chini Mheshimiwa Juma tafadhali. Mheshimiwa Khatib, wewe unapewa taarifa, kwa hiyo, kaa utapewa fursa. Wewe kaa, amalize. Mheshimiwa Nyongo…

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mfano mzuri ni kwa United States of America. California wana Chama cha Mpira, ukienda Majimbo mengine yote yana Chama cha Mpira; na wote ni Wanachama wa Football Federation of United of States America. Kwenda World Cup haiendi California, haiendi nchi nyingine, inakwenda United States of America na kuna more than 50 sets of United State of America. Wasipotoshe wananchi, ZFA ni Mwanachama wa TFF.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khatib, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshangaa sana. Hayo maandishi umetoa wapi, hata unakuja kusimama hapa unasema ZFA ni mwanachama wa TFF? Kwanza…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khatib zungumza name. Nimeuliza swali, unaipokea ama huipokei? Zungumza na Kiti, usizungumze naye. Zungumza nami, atakusikia ukizungumza nami.

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nipokee nini hapo utumbo huo anaozungumza yule! Mheshimiwa TFF, TFF…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khatib, una uwezo wa kukataa hiyo taarifa bila kuiita majina ambayo unataka kutuaminisha hapa kwamba ndiyo hayo aliyoyasema. Wewe ikatae taarifa yake, endelea na mchango wako, ndiyo kanuni zetu zinavyosema. Sasa hii habari ya nyama, ya utumbo umefanyaje, hebu ondoa hiyo habari ya utumbo hapo. Siyo lugha ya kibunge, ondoa maneno “utumbo” uendelee kuchangia kama umeikata taarifa yake.

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakuheshimu sana, mimi nakataa hiyo taarifa yake ni rubbish kabisa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.

KUHUSU UTARATIBU

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kuna kanuni inavunjwa. Mheshimiwa Jenista, kanuni iliyofunjwa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu
Spika, kuhusu utaratibu, nakwenda kwenye kanuni ya 64 (1) (b) ambayo inakataza Mbunge ama Wabunge kutokuzungumzia jambo ambalo halipo kwenye mjadala.

Mheshimiwa Naibu Spika ninaanza kuona sprit ya majadiliano yetu leo inahama kutoka kwenye hoja iliyopo mezani, sasa watu wanataka kuwachanganya Wabunge na kulichanga Taifa kuhusu Muungano wetu katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, wakati tukiendelea na mjadala huu, Wizara iiliyokuwa inashughulika na masuala Muungano tulishaifunga jana. Watu wajikite kwenye maudhui ambayo yanaenda sambamba na Wizara ambayo hoja yale iko mezani, lakini masuala nyeti yanayohusu Muungano naomba...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Zitto, Mheshimiwa Zitto! Mheshimiwa Jenista.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, masuala yanayohusu tafsiri za Kikatiba kuhusu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Muungano yasiwe ni part ya mjadala huu katika siku ya leo.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisisitize jambo hili ili kuondoa mkanganyiko wa mtazamo wa Kimuungano katika mjadala unaondelea hapa Bungeni.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, amesimama Mheshimiwa Jenista akitukumbusha kwamba kanuni ya 64(1)(a) na (b) na ameweka mazungumzo yake kwa kirefu na sikusudii kuyarudia; ametupeleaka kwenye fasili ya (b) kwamba Mbunge hatazungumzia jambo ambalo halipo kwenye mjadala.

Waheshimiwa Wabunge, nadhani hii kanuni ya 64 sote tunaifahamu, kwa hiyo, Mheshimiwa Jenista ametukumbusha. Mheshimiwa Khatib na Waheshimiwa Wabunge wengine waliotoa taarifa na waliochangia tuendelee na mjadala wa Wizara hii kwa yale mambo ambayo yanahusika. Wapo wengine hawajapewa fursa ya kuzungumza, lakini namna wanavyoyazungumza kwa kuwa yale wanayoyasema mengine yanasikika, basi yanaleta upotoshaji kwenye hoja nzima, hata ambayo alikuwa anazungumza Mheshimiwa Khatib. Wakati hoja yenyewe ni ya wazi na imenyooka.

Kwa hiyo, nawaomba Waheshiwa Wabunge tufuate kanuni zetu, mambo yasiyoruhusiwa tusiyafanye. Kwa sasa mjadala ulioko mbele yetu tunaufahamu, ni hoja ya Mheshimiwa Waziri; na yale aliyoyasoma Mheshimiwa Waziri na yaliyosomwa na Kamati ndiyo ambayo tunapaswa kujikita katika hayo ili tutoe maoni katika kuhakikisha tunaboresha ama tunataka Wizara kwenye yale mambo ambayo imeyaleta irekebishe wapi. Ndiyo maana Kamati imetuletea kwenye yale maoni yake.

Kwa hiyo, nawaomba tufuate hiyo kanuni ya 64 tujikite kwenye mjadala hasa kwa kuzingatia maoni….

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: …ya Kamati ili tutakapokuwa tunasonga mbele tuone wenzetu wametuongoza mambo gani ambayo tunapaswa kuishauri Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Khatib.

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu Utaratibu.

MHE. KHATIB SAID HAJI: Eeeh, hee!

KUHUSU UTARATIBU

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Najma ukisimama sasa hivi, maana yake mimi ndio nimekosea tena.

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, hapana siyo hiyo.

NAIBU SPIKA: Kama hilo siyo lengo lako, inabidi nimpe fursa Mheshimiwa Khatib.

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Haya ahsante.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khatib.

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nitaendelea kwa lugha ya upole kabisa.

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. KHATIB SAID HAJI: Eeeh!

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba unipe muda nimalize.

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa, alinitaja.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ali King, kwa kuwa nilikuwa nimeshasema taarifa ya Mheshimiwa Nyongo itakuwa ni ya mwisho kwa Mheshimiwa Khatib, utapewa fursa wakati wa kuchangia. Mheshimiwa Khatib. (Makofi)

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nadhani nitakuwa sijatoka nje ya mada na sitaki kutoka nje ya mada. Hapa nilichokieleza ni kwamba tulikuwa tunalilia lile fungu la mgao unaotoka FIFA kwa Zanzibar. Ni ukweli ambao nitaendelea kuuamini kwamba Zanzibar sio Mwanachama wa TFF na Zanzibar ni chombo huru, kipo kiko chini ya Wizara ya Habari kwa Zanzibar.

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khatib, kuna kanuni inavunjwa, Mheshimiwa Najma.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie Kanuni ya 64(1)(a) ambayo hairuhusu humu ndani mtu kuzungumza jambo ambalo si la kweli.

Mheshimia Naibu Spika, Mheshimiwa Nyongo wakati anatoa taarifa alizungumza kauli ambayo inasema kwamba Zanzibar ni sawasawa kama mikoa mingine. (Makofi)

Kwa hiyo, naomba tu Mwongozo wako kwamba hili suala aliweke sawa au aondoe kauli yake kwa sababu Zanzibar ndani ya Tanzania ni nchi, nje ya Tanzania ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, nimetoka kuzungumza hapa na kama kuna mtu mwingine hakumsikia sawasawa Mheshimiwa Nyongo anaweza akapewa fursa ya kuangalia Hansard. Amezungumzia chama cha michezo sio Zanzibar kama mkoa.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kila mtu ana masikio na amesikia na kwa kawaida walimu wapo wengi sana humu ndani. Kuna watu ambao huwa wana kitu kile ambacho kwa kiingereza kinaitwa selective listening, yeye anasikiliza anachotaka kusikia yeye. Kwa hiyo, tuelewane vizuri kwenye hili Mheshimiwa Nyongo hajasema Zanzibar ni mkoa, amesema chama cha mpira cha Zanzibar ni mwanachama wa TFF kama ambavyo vyama vingine. Kwa hiyo...

Mheshimiwa Zitto naomba utupe fursa tafadhali tuendelee na shughuli nyingine.

Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge mimi nampa fursa Mheshimiwa Khatib amalizie mchango wake, mtu yeyote mwenye taabu na mchango wa Mheshimiwa Nyongo ataenda akaisome Hansard yale aliyoyasema Mheshimiwa Nyongo. Kwa hiyo, hajaasema Zanzibar ni mkoa, tuelewane vizuri.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khatib nimeshamjibu Mheshimiwa Najma naomba tusirudi pale, malizia mchango wako.

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kosa alilolifanya Nyongo ni kubwa sana, hawezi kuifananisha Zanzibar na mkoa hata siku moja na kama ni mchango bora niishie hapa, haina haja ya kuchangia tena. (Makofi)