Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, jina langu kamili naitwa Emmanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini. Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hotuba nzuri ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Naomba ili kule mbele ya safari nisije nikasahau kuunga hoja, kabla sijaanza kuchangia niseme naunga mkono hoja asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kutoa rai kwanza kwa ndugu zetu kwa Waandishi wa Habari haya wanayofanya ndugu zetu hawa wapinzani nilikuwa naona leo magazeti mengi yameandika kimenuka, na lugha kama hizo naomba waandike pia kwamba hawa wenzetu pamoja na kwamba kimenuka wanaondoka wakiwa wamesaini pesa za walipa kodi ili wananchi waweze kuwaelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba pia nisirudie ya wenzangu kwa sababu Mkoa wa Tabora tuna kitu ambacho ni common interest kama Kiwanda cha Tumbaku na wenzangu walishaongelea. Lakini naomba niongelee Kiwanda cha Nyuzi katika hotuba ambayo ni ya Mheshimiwa Rais. Kiwanda kile tulikwenda kukikagua na Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya kama mwezi mmoja umepita, Kiwanda cha Nyuzi Tabora sasa hivi ni godown.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kubinafsishwa tulikwenda ili wakakifungue lakini tukaambiwa mimi na DC kwamba kiwanda kile funguo zake maana yake tuliambiwa kwamba ile mitambo ya mle ndani ilishauzwa kama vyuma chakavu, tukataka tushuhudie lakini tukaambiwa kwamba funguo ziko India. Sasa kwamba mwekezaji kaondoka na funguo kwenda India hili ni jambo ambalo Mheshimiwa Mwijage, Waziri wa Viwanda na Biashara tuna tatizo hilo, kiwanda kile kimfungwa funguo ziko India. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kama Mbunge wa Tabora Mjini niweze kuongelea suala la hospitali yetu ya Mkoa ambayo ndiyo ya Rufaa ya Kitete. Pale kama alivyoainisha Mheshimiwa mmoja aliongelea suala la Kitete, hospitali ya Kitete ina changamoto nyingi na ndiyo hospitali tunayoitegemea kama ya rufaa. Kweli ina tatizo kubwa la wataalam, Madaktari Bingwa pale wanahitajika madaktari kama nane, nilitembelea ile hospitali kama mwezi mmoja pia umepita, niliongea na Mganga Mkuu, kuna Daktari Bingwa mmoja tu katika Madaktari Bingwa nane wanaohitajika katika hospitali. Lakini niliuliza kwani kuna changamoto gani, nikaambiwa suala ni kwamba hawapendi kukaa pale Tabora kwa sababu ya mazingira, nilimuuliza Mganga Mkuu unadhani ni mazingira gani akaniambia hawapendi kukaa Tabora kwa sababu kwanza maslahi ni kidogo, hawawezi pia kupata nafasi za kufanya kazi zile za ziada part time kama wanavyoweza kufanya Madaktari wengine wa Miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha. Kwa hiyo, ningeomba Wizara iweze kuangalia kwa makusudi ili kuweza kuboresha zile huduma lakini pia kuboresha maslahi ili hao wataalam watakapopatikana waweze kukaa kama hospitali yetu ya Kitete bila kuona kwamba wamesahauliwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna matatizo pia ya Wauguzi wako wachache sana hospitali yetu ya rufaa na wale wachache ambao wanafanya kazi, nichukue nafasi hii kuwapongeza kwamba wanafanya kazi katika mazingira ambayo maslahi siyo mazuri, lakini inapofika suala la muda wao wa ziada manesi wale wanafanya kazi nzuri Madokta lakini muda wao wa ziada amekuwa haupati pesa kutoka Serikalini kwa ajili ya kulipa zile overtime, kwa hiyo, hii inakatisha tamaa, naomba Wizara husika muweze kuliangalia jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye suala la maji nitakwenda haraka haraka kwa sababu ya muda, Tabora tuna bwawa la Igombe linatoa maji lakini tuna bwawa pia la Kazima ambalo sasa limejaa tope, lakini bado kuna maji ambayo yanaweza kutosha hata vijiji vya jirani au kata za jirani kama Manoleo, Itonjanda na Ifucha ambazo zinazunguka lile bwawa. Lakini bwawa lile limeachwa tu kiasi ambacho sasa halihudumii zile sehemu ambazo zina matatizo ya maji.
Mimi ningeishauri Serikali kwamba katika kipindi hiki ambacho bado tunasubiri maji ya Ziwa Victoria waweze kuchukua njia angalau kutoa lile tope, maji yale ni mengi kuliko tunajenga bwawa jipya, tuna bwawa jipya linajengwa sehemu za Inara, Kata ya Ndevelwa, bwawa lile hata maji ya safari hii lile bwawa lilikuwa linakamilika lakini sasa linavuja maji hayakai, na limegharimu zaidi ya shilingi bilioni moja na kitu. Lakini Idara yetu ya maji pale TUWASA bili nyingi hazilipwi na hasa na taasisi za Serikali na ile TUWASA pale Tabora ni moja ya taasisi ambazo zinajitegemea hazipata ruzuku yoyote. Ile taasisi inadai zaidi ya shilngi bilioni 1.3 na wadeni wakubwa ni pamoja na taasisi za Serikali lakini pamoja na shule mbalimbali. Kwa hiyo, naomba Wizara ya Maji muweze kuliangalia hili kwamba tunafanyaje, kwa sababu sasa suala la maji limekuwa ni tatizo kubwa Tabora.
Lakini pia naomba niongelee suala la wenzetu hawa askari na hasa polisi kwa kweli hali za askari wetu hasa polisi kwenye kambi zao zile nyumba zao kwa kweli hata ukiziangalia hazilingani na Jeshi la Wananchi, JWTZ sasa hivi ukiangalia nyumba zao angalau zinavutia. Naomba Wizara inayohusika basi tuwakumbuke na ndugu zetu wa polisi kuwawekea mazingira mazuri wanapokaa pamoja na maslahi yao ili kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Mwisho naomba niongelee kuhusu reli, wenzetu walishaongelea. Kuhusu reli kwanza kabla sijaongea kwa sababu sijajua kama nitafika huko mimi nina interest, tumeambiwa tu-declare interest kama unayo kwenye shirika. Mimi nimekuwa ni mfanyabiashara mmoja wa reli, lakini kuna kitu kimoja kinanishangaza kuhusu reli, kila siku ni Godegode. Kila tunaposikia treni haiendi ni Godegode, sasa pale Godegode kuna nini? Kama imewezekana kujenga daraja la Malagalasi kubwa kiasi kile, kila siku kambi ya reli ni Godegode, naomba Wizara husika tuangalie pale Godegode kuna nini, isije ikawa ni mradi…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwakasaka muda wako umekwisha!
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Ahsante naomba kuunga hoja mkono asilimia mia moja. (Makofi)