Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Nataka kuweka mkazo kwa mchango wangu kuhusu umuhimu wa utawala wa sheria na haki, utaratibu wa kukamata watu kwa tuhuma ambazo DPP hana ushahidi si sawa kabisa. Kuwaweka watu rumande kwa muda mrefu halafu mchezo wa “uchunguzi haujakamilika” si sawa kabisa, ni uonevu, hakika. Kama mtu anatuhumiwa kutenda kosa uchunguzi ufanyike na sheria ichukue mkondo wake lakini mtindo mpya wa kubambikiziwa mtu kesi au charge ambazo hazina dhamana kusudi asote rumande miaka nenda, miaka rudi, si haki, si sawa na ni kero kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, magereza zimejaa watu ambao wametuhumiwa makosa ya kawaida mfano,traffic case lakini wamenyimwa dhamana wako jela miezi hata miaka. KatikaGereza la Muleba nimeshuhudia wanawake waliowekwa mahabusu ili wapishe waume zao kuuza mashamba ya familia. Nimeshuhudia watu walio mahabusu muda mrefu kwa sababu ya ugomvi. Hata kesi za mauaji inabidi ziwekewe mkazo na uchunguzi ufanyike na Nolle prosequi zitoke kwa muda muafaka na zisipotoka basi kesi zisikilizwe kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mhimili wa Mahakama uko huru na ni muhimu sana uhuru huo udumishwe. Mhimili wa Mahakama sharti ujitathimini. Tunashuhudia baadhi ya Mahakimu hasa ngazi za Mahakimu waMwanzo na Wilaya wakila rushwa za waziwazi, unakuta Hakimu Mkazi anafanya mtandao na viongozi wenyeji wenye uwezo kuwanyanyasa wananchi kwa kubuni kesi ambazo zinahukumiwa na mtu anashindwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nililalamikia Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Mubunda huko Muleba, Ndugu Omar Musa kwa tabia yake mbaya kutoa hukumu kwa dhuluma. Hakimu huyu alipokuwa Mahakama ya Mwanzo, Kashasha, Wilayani Muleba alisababisha mtoto kumfunga mama yake mzazi katika mgogoro wa shamba. Nililazimika kulipa faini aliyoikosa huyo mama iliatoke mahabusu lakini huyo mama alikufa siku mbili baadaye kwa huzuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hakimu huyo alipohamishiwa Mubunda akajiingiza katika kesi za Diwani wa Kata ya Kashurunga, Ndugu Khalid Swalehe na kuwafunga Mwalimu Mkuu wa Shule huko Kimeyo na mke wake na baadaye Mwenyekiti wa Kijiji cha Nkomero katika mgogoro wa eneo la ardhi ya shule. Diwani anataka kupora eneo la shule na mwalimu na mke wake na Mwenyekiti wanatetea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa juhudi zangu kutetea suala hili hadi leo zimeshindwa. Nimeambulia kutolewa tamko la Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) juu ya matamshi ya Mbunge wa Muleba Kusini dhidi ya Mahakama isiyo na tarehe lakini iliyosainiwa na Rais wa chama hicho, Jaji Wilberforce Samson Luhwago.Ni tamko la pages saba linanilaani mimi kwa kulalamikia Mhimili wa Mahakama mara kwa mara na hatimaye kulalamika katika mkutano wa hadhara mbele ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naambatisha tamko hilo ili liwe sehemu ya Hansard ya mchango wangu. Yaani mimi mtu wa kawaida ninatolewa tamko na Chama cha Mahakimu na Majaji kwa kufanya kazi yangu ya Ubunge ambayo ni kutetea wananchi na kuijulisha Serikali na Mhimili wa Mahakama juu ya mapungufu waliyonayo ili wayafanyie kazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba maelezo juu ya suala hili na hatma yangu nikiwa na kesi Mahakamani nani ataisikiliza kwani tamko hilo lilidaiwa ni la Majaji na Mahakimu wote. Kwa dharau kabisa hadi leo Hakimu Omar Musa bado hajahamishwa kutoka Mubunda hivyo kunipa kazi ya ziada kuwatuliza wananchi wenye hasira wasifanye fujo. Naomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitolee ufafanuzi jambo hili na kunielekeza juu ya utaratibu wa kusikiliza kesi zangu zinapokuwa Mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba Mhimili huu katika kujitathmini waangalie mtindo mpya wa baadhi ya Mahakimu wasio waadilifu kufanya kazi na Mawakili wasio waadilifu. Kwa hiyo, mtuhumiwa unaelekezwa na Hakimu kama unataka kushinda kesi kamlete advocate fulani. Mhimili huu ujitathmini kwani changamoto za rushwa zinawaumiza watu ambao niinnocent.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.