Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. January Yusuf Makamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbuli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba nishukuru kwa fursa uliyonipa ya kuja kuhitimisha hoja hii hapa siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwashukuru wachangiaji wote, kwanza kwa Kamati zote mbili: Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Kamati ya Katiba na Sheria kwa taarifa nzuri walizozitoa pamoja na ushauri, maoni na mapendekezo ambayo wameyatoa katika taarifa zao. Pia napenda niwashukuru wachangiaji wote waliochangia kwa maandishi walikuwa 25, waliochangia kwa kuzungumza walikuwa 9, jumla watu 34.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuipongeza Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa taarifa yao waliyosoma na maneno yao walitueleza na yote tumeyapokea na yote ni ya kujenga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimshukuru Naibu Waziri wa Fedha ambaye ametusaidia kuelezea baadhi ya mambo na kujibu baadhi ya hoja. Pia namshukuru Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mheshimiwa Mwalimu Sima naye kwa mchango wake na majibu aliyoyatoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kwenye masuala machache ya jumla ambayo Waheshimiwa Wabunge waliyachangia. Kwanza suala la biashara kati ya Zanzibar na Bara ni jambo ambalo limejitokeza katika michango ya Waheshimiwa Wabunge wengi waliochangia masuala ya Muungano. Bahati nzuri Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha ametusaidia kujibu kwamba changmoto za kikodi ndiyo zilizokuwa zinakwamisha biashara kati ya Bara na Zanzibar zilitokana na mfumo tofauti wa ukadiriaji wa kodi kwa bidhaa zinazoingia katika vituo vya forodha vilivyoko upande wa Zanzibar na vituo vya forodha vilivyoko upande wa Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hilo sasa linashughulikiwa kwa kuweka mfumo mmoja wa ukadiriaji wa kodi kiasi kwamba bidhaa itakayoingia kwenye kituo cha forodha cha Zanzibar ikadiriwe kodi sawa na kituo chochote ambacho bidhaa hiyo imeingia kwa upande wa Bara. Imani yetu ni kwamba hilo litapunguza malalamiko na maelezo kwamba kunakutozwa kodi mara mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua haja ya kushughulikia masuala ya fedha na biashara kwa wakati wote, Kamati ya Pamoja ya kushughulikia changamoto za masuala ya Muungano iliunda Kamati Ndogo ya Fedha, Biashara na Uchumi ya Mawaziri, Makatibu Wakuu na wataalam ambayo itakuwa inakutana mara mbili kwa mwaka kushughulikia masuala ya fedha, uchumi na biashara yanayojitokeza mara kwa mara. Imani yetu ni kwamba mfumo huu na Kamati hii sasa itasaidia kusukuma mambo haya kwa haraka zaidi na kutatua changamoto za biashara zinazojitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imani yetu sisi tuliopo katika Ofisi ya Makamu wa Rais ni kwamba uchumi wa Tanzania Bara ni mkubwa kuliko uchumi wa Zanzibar na Zanzibar lazima ifikie soko la Bara na Bara vilevile lazima iwe na uwezo wa kufikia soko la Zanzibar bila vikwazo vyovyote. Muungano huu ni wa kisiasa, kijamii pia kiuchumi. Kwa hiyo, imani yetu ni kwamba moja ya shabaha za Muungano ni kuleta ustawi wa watu wa pande zote na Muungano usionekane kikwazo cha ustawi wa upande mmoja au mwingine. Sisi katika Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa maelekezo ya Mheshimiwa Makamu wa Rais ni kwamba tufanye jithada zote ili fursa za uchumi, biashara na ustawi na zenyewe ziendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Bara na Zanzibar wamekuwa wanafanya biashara hata kabla ya Muungano kwa miaka mingi, hata kabla ya Uhuru, hata kabla ya Mapinduzi. Imani yetu ni kwamba kuwepo kwa Serikali kusiwe kikwazo kwa biashara ya asili ambayo imekuwepo kwa miaka mingi kati ya watu wa pande zote mbili. Hiyo ni dhamira yetu kwamba ukubwa wa soko la Bara usaidie kujenga uchumi wa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Tume ya Pamoja ya Fedha, nadhani Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha amelijibu lakini nitapenda niongezee machache. Ni kweli Tume ya Pamoja ya Fedha imeundwa kwa mujibu wa Katiba na vilevile Mfuko wa Pamoja na wenyewe umeundwa kwa mujibu wa Katiba. Hili suala linajirudia mara kwa mara hapa Bungeni kuhusu lini Mfuko huo utaanzishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtakumbuka kwamba kwa mujibu wa Katiba, moja ya kazi za Tume ya Pamoja ya Fedha ni kuchunguza kwa wakati wote mfumo wa shughuli za fedha wa Jamhuri ya Muungano na pia uhusiano katika mambo ya kifedha kati ya Serikali mbili. Hiyo ni moja ya majukumu matatu ya Tume ya Pamoja. Tume hiyo ilifanya kazi kubwa sana kuanzia miaka ya 90 na mwaka 2006 ikawasilisha ripoti Serikalini, nakumbuka ilikuwa tarehe 9 Oktoba, 2006 kwa Waziri wa Fedha wakati huo Mama Zakia Meghji na ripoti ile Tume ilikuwa ni ya mapendekezo ya vigezo vya kuchangia na kugawana mapato ya Muungano. Ni ripoti iliyotokana na study ya muda mrefu kwenye nchi nyingi kuhusu mfumo sahihi, bora na na sawia (equitable) wa kugawana mapato na kuchangia mapato ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ripoti ile kupokelewa, Serikali zote mbili ziliahidi kuifanyia kazi na kweli baada ya pale ikapelekwa kwenye Baraza la Mawaziri wataalam wakaifanyia kazi, Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mara kadhaa mapendekezo yale yalitengeneza cabinet paper ili yaweze kupitishwa na tuwe na mfumo bora ikiwemo kuanzisha Akaunti ya Pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya hilo halikutokea kwa sababu moja au nyingine hadi tukaanza mchakato wa Katiba ambapo ndiyo ulionekana kwamba utakuwa mfumo bora zaidi wa kushughulikia jambo hili. Kwa hiyo, imani yetu ni kwamba mchakato wa Katiba utakaendelea basi suala hili pia litaendelea kushughulikiwa. Tunashukuru kwamba pia Wizara ya Fedha inaendelea kulishughulikia suala hili. Kwa hiyo, Akaunti ya Pamoja ni takwa la Kikatiba na lazima litekelezwe na lazima litatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vikao vya Kamati ya Pamoja, tumesikia kwenye taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani ikisema kwamba vikao hivi havina maana yoyote kwamba vinakaa, hatuoni matunda na hakuna utekelezaji na kadhalika. Labda niseme tu kwamba mwaka 2006 tulipoanzisha utaratibu mpya wa Kamati ya Pamoja ya Fedha kulikuwa na changamoto 15 za Muungano na kwa kutumia mfumo huu wa vikao zimetatuliwa changamoto 11 zimebaki changamoto tano (5).

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto hizi zimetatuliwa katika vikao na siyo kwa njia nyingine na siku zote mambo yote yanamalizwa kupitia vikao. Kwa hiyo, sisi hatuamini kabisa kwamba vikao hivi havina maana kwa sababu tumeona matunda yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu wanapokuwa na mambo wanayamaliza kupitia vikao. Kwa hiyo, ingependeza kama wenzetu Waheshimiwa wangetueleza zaidi ya vikao ni ipi namna bora zaidi ya kuzungumza mambo ya Muungano. Sisi tunaamini vikao ni namna bora zaidi. Bahati nzuri katika kikao cha tarehe 9 Februari, 2019, hapa Dodoma cha Kamati ya Pamoja tuliamua kurasimisha na kuimarisha mfumo wa vikao hivi ili tuweze kufuatilia maelekezo na maagizo yake na kuhakikisha kwamba yanayoamuliwa yanatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa kwamba vikao vinakaa na changamoto za Muungano haziiishi. Naomba niseme hapa kwamba changamoto za Muungano hazitakuja kuisha hata siku moja na dhana kwamba kwa sababu kuna changamoto basi Muungano haufai ni potofu kabisa. Siku ya kwanza Muungano umepitishwa, siku ya pili kulitokea changamoto ya namna ya kuunganisha majeshi, mfumo wa fedha na masuala ya ushirikiano wa kimataifa na mambo mengine, siku ya pili tu ya Muungano. Nakumbuka wakati ule tulikubaliana kwamba masuala ya fedha yatakuwa ya pamoja lakini kukawa na mkanganyiko kuhusu nafasi ya Peoples Bank of Zanzibar na BoT lakini mambo haya yalimalizwa kwa vikao na leo changamoto ile hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka ya 55 ya Muungano changamoto ambazo leo hatuzizungumzii kwa sababu zimemalizwa ni nyingi. Kwa hiyo, sisi tunaamini kwamba Muungano huu kikubwa ni mfumo na utaratibu ambao tutauweka wa kumaliza changamoto na hilo ndio ambalo tunalifanya sasa. Kudhani kwamba hakutakuwa na changamoto ni ndoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imeongelewa kuhusu mainstreaming ya masuala ya Muungano, utaona ni hoja iliyotolewa na Mheshimiwa Saada Mkuya. Sisi tunadhani kwamba ni hoja muhimu na ya msingi. Wewe unafahamu na Waheshimiwa Wabunge wanafahamu kwamba kwenye kila bajeti ya kila Wizara iwe ni ya Maji, Miundombinu au Maliasili kuna mambo huwa hayakosi UKIMWI na rushwa siku zote hata kama hayahusu sekta hizo lakini yamo kwenye bajeti zote za Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaamini kwamba tufike mahali kwamba kwenye kila bajeti ya kila Wizara iwe ya Muungano isiwe na Muungano basi suala la Muungano na lenyewe liwepo kama ripoti ambayo inatolewa. Hili tunalizungumza Serikalini kwa sababu kwa Wizara za Muungano kuna ulazima wa kushirikiana na mambo ya kutekeleza lakini kwenye Wizara ambazo siyo za Muungano tunahamasisha ushirikiano. Kwa hiyo, itapendeza hapa kwenye hotuba za bajeti kila Wizara ikasema imeshirikiana vipi na upande wa pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda na wenzetu wa Zanzibar kama tutazungumza na kukubaliana pia katika bajeti zao na wenyewe waseme katika mwaka uliopita wa fedha kama ambavyo kwenye masuala ya rushwa na UKIMWI wanaripoti basi vilevile kwenye masuala ya Muungano kuwa na ripoti. Tunaamini hatua hii itasaidia kuimarisha Muungano na italazimisha wenzetu na wengine waripoti kuhusu masuala ya muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme tu kwamba watu wengi hawajui lakini hakuna Wizara isiyo ya Muungano kwenye Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iwe ni Wizara ya Maji ambayo siyo jambo la Muungano au Wizara ya Utalii ambayo siyo jambo la Muungano, Wizara zote ni za Muungano. Mheshimiwa Dkt. Kibwangalla anaitwa Waziri wa Maliasili na Utalii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu hakuna Wizara ya Bara, Wizara zote ni za Muungano. Kwa hiyo, kila Wizara ina wajibu wa kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba angalau tunashirikiana na upande wa pili kuhusu masuala ya Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imetoka hapa hoja kwamba Serikali ya CCM haina nia na Muungano huu. Mimi huwa sipendi kuingia kwenye mambo ya kushambuliana kwenye vyama na mambo ya siasa za aina hiyo, lakini kauli hii lazima ijibiwe. Katika mambo ambayo yanapaswa kuwa nje ya siasa ni masuala ya Muungano. Kwenye nchi zote kuna baadhi ya mambo ambayo siasa haipaswi kuingizwa. Kwenye nchi za wenzetu kuna mambo ambayo yamemalizwa siyo tena mjadala na kwenye nchi yetu mimi imani yangu ni kwamba Muungano ni jambo ambalo tunapaswa kuwa tumelimaza halipaswi kuwa na u-CCM, u-CUF, u-ACT wala namna nyingine yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa mfano wa nchi ya Marekani, wao ni Muungano wa Kifederali na ule Muungano uliletwa kwa vita, kuna nchi zilikuwa hazitaki kuwa sehemu ya Muungano na vita ikapiganwa na wale ambao hawakutaka kuwa sehemu ya Muungano wakaingizwa kwenye Muungano kwa kushindwa kwenye vita hasa Majimbo ya Kusini. Tangu wakati ule leo United States of America, aidha, iwepo au isiwepo siyo tena hoja ya siasa wala kampeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani tunapaswa kufika hapo kwamba wakati wa uchaguzi haipaswi Muungano wetu kuwa kwenye referendum. Kwa sababu kilichopo sasa hivi ni kila uchaguzi unapofanyika Muungano ni kama vile upo kwenye kura ya maoni. Kwa hiyo, kama nchi tunapaswa kuondoka huko. Wenzetu ambao wameungana kila mahali, hata Marekani Muungano wao una miaka zaidi ya 200, lakini kila siku wana kauli yao wanasema, to strive for a more perfect union. Kwamba, Muungano wao wa miaka 200 bado hauko perfect. kwa hiyo, nasi leo tukija hapa Bungeni tukataka leo miaka 55 tuwe na a perfect union tutakuwa tunaomba mambo ambayo hayako tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Muungano huu kazi yetu ni kuendelea kuujenga na namna ya kuujenga siyo kuusimanga na kuchukulia changamoto ndogo na kuupaka matope na kuupa jina baya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia zaidi ya 94 ya Watanzania wamezaliwa ndani ya Muungano, hawajui Tanganyika, wanajua wamezaliwa ndani ya Muungano na hawana pengine pa kwenda na utambulisho wao ni wa Muungano. Kwa hiyo, nawaomba na kuwasihi Waheshimiwa Wabunge ambao huwa tunarushiana vijembe na maneno na wale wanasiasa ambao wanatumaini changamoto za Muungano zitasaidia kuwabeba, basi tuache hivyo, wote tufanye kazi pamoja kuuimarisha Muungano wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi Rasmi ya Upinzani imezungumzia kuhusu muundo wa Muungano na kwamba ndiyo chanzo cha changamoto na kwamba haufai na ndiyo umetuletea matatizo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa kwenda kwenye mjadala huu kwa sababu ni mrefu na wote tunajua mjadala huu tuliufanya wakati tunafanya mchakato wa Katiba. Ambacho naweza kusema ni kwamba, Waasisi wa Muungano, Mwalimu Nyerere na Mzee Karume, kabla hawajaamua Muungano wa aina tuliyonayo leo, walitafakari miundo yote ya kila aina, wakatazama dunia nzima, wakatazama mazingira yetu, wakatazama haiba ya watu wetu, wakatazama ukubwa wa pande zote mbili na wakaamua kuwa na Muungano wa kipekee duniani ambao ndiyo tulionao leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiniuliza mimi sababu ya kudumu kwa Muungano huu, tofauti na Muungano wa Senegal na Gambia, tofauti na Muungano wa Misri, Syria na kwingineko ni kwa sababu ya muundo wake. Tunatofautiana; wengine wanadhani Muungano wetu una shida kwa sababu ya muundo wake, lakini sisi tunaamini Muungano wetu umedumu kwa sababu ya muundo wake. Kwa hiyo, kikubwa ni kuendelea kuimarisha mifumo na taratibu za kushughulikia masuala yanayojitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna bahati kwamba Muungano wetu una bahati ya kuundwa katika misingi ya kijamii, kwa sababu mahusiano ya kijamii ya watu wa pande zote yamekuwepo kabla ya mapinduzi, yamekuwepo kabla ya uhuru na yamekuwepo kabla ya Muungano. Kikubwa tu ni sisi kuendelea kuimarisha masuala ya kitaasisi na kisheria na kiutaratibu ili tuendelee kuwatendea haki watu ambao ni ndugu wa pande zote mbili za Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumziwa hapa suala la vyombo vya moto, kwamba haipendezi ikawa kuna ugumu wa kuingia na gari lako kutoka upande wa pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kabisa kwamba ni jambo linalokera, linaloudhi kwamba gari kutoka Zambia au Malawi, linavinjari kwa urahisi katika nchi yetu, lakini gari kutoka Zanzibar linapata bughudha. Hilo jambo halikubaliki kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri sasa Serikali imeanza kulishughulikia jambo hilo na Mwanasheria Mkuu wa Serikalin anafahamu kwamba kulikuwa tayari na mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria ya Usajili wa Magari na Sheria nadhani ya Polisi na ilishafika kwenye Mkutano wa Kamati ya Baraza la Mawaziri ya Katiba na Bunge ili mabadiliko yafanyike kuhakikisha kwamba jambo hilo linakwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya tukashauriwa kwamba ili utaratibu huo udumu na uwe imara, tuhakikishe kwamba zinawekwa taratibu ili wale watu ambao wanaweza kutumia mwanya kuingiza magari na badaye kuyauza kwa upande mwingine, basi wasifanikiwe. Sasa study hiyo iliyofanywa na TRA na wengine imekamilika, nasi tunaamini kwamba wachache ambao wanaweza kutumia fursa hiyo vibaya wasiwaharibie watu wengi wema ambao wanataka kusafiri na vyombo vyao vya moto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaratibu huo utawekwa na ni imani yangu kwamba mabadiliko hayo ya sheria yatafywa mapema kupitia kwa wenzetu ili jambo hilo tulimalize. Ni kero kubwa na ni aibu kusema kweli. Kwa hiyo, imani yetu ni kwamba litakwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa suala la mifuko ya plastic. Naomba niseme, tumezungumza kwa kirefu kwenye hotuba yetu, lakini naomba niseme tu kwamba dhamira hii ni njema. Kwenye hili tumejipanga vizuri kwa sababu tumeshirikisha wadau mapema zaidi. Tunaamini kwamba suala hili ili tufanikiwe ni lazima twende hatua kwa hatua. Kwa sasa hatuwezi kupiga marufuku kila kitu; kuna baadhi ya vifungashio vinavyotumia plastick ambavyo ni lazima vitumie plastick, kwa mfano, mikate, maziwa, madawa na vinginevyo. Imani yetu ni kwamba, kwa sasa vitaruhusiwa ili tusilete bughudha na mtikisiko kwenye uchumi na kuongeza bei za bidhaa kwa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaanza na mifuko hii ambayo ni kero, hata hivyo kwa vifungashio tutaweka standards ili viweze kukusanywa na kurejelezwa. Hiyo, tunaamini tutafanikiwa. Hata wale wenye chupa za plastick vile vile imani na mpango wetu ni kuweka ulazima wa wao kushiriki kwenye mipango ya recycling, kwamba huwezi kuwa unazalisha chupa za Kilimanjaro halafu huna habari hiyo chupa inaishia wapi? Lazima ushiriki kwenye utaratibu wa kuirejesha na kuirejeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kanuni mpya pia zitatoa mahitaji hayo. Naomba Waheshimiwa Wabunge tusaidiane, kwa sababu tutakapofanikiwa jambo hili tutakuwa tumefanya jambo la kihistoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shaka kuhusu mbadala kwamba, je, mbadala upo na unatosha? Naomba niwaambie kwamba wenzetu Wakenya ambao wamepiga marufuku mifuko ya plastic, mifuko yao ya karatasi wanaitoa Tanzania. Wenzetu Warwanda, ukienda kule Mufindi Paper Mills, malighafi yote ya mifuko ya karatasi ya Rwanda inatoka Mufindi na Rwanda inasifika, Kigali, kama mji safi kabisa hapa Afrika, sababu ni nini? Sababu ni sisi ndio tunawapa karatasi, wanapata mifuko ya karatasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wale wametuhakikishia kwamba uwezo wa ku-supply mifuko ya karatasi hapa nchini wanao na kwamba, changamoto yetu kubwa kwa sasa ni kuhakikisha wanaongeza production na usambazaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni tunazotoa zitatoa adhabu kwa wanaouza mifuko, wanaoweka na kwa wanaoingiza ndani ya nchi. Kunaweza kukatokea mtikisiko na malalamiko kidogo kwenye zoezi hili, naomba Waheshimiwa Wabunge muiunge mkono Serikali kuhakikisha kwamba, jambo hili linafanikiwa. Kwa sababu, siku zote hakuwezi kukosa malalamiko kwenye masuala makubwa ya mabadiliko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu matumizi ya mkaa na ukataji wa miti, hii ni changamoto kubwa sana sana. Kila dadika moja inayoenda hapa nchini, misitu inayofyekwa ni sawa na kiwanja cha mpira. Tangu niongee hapa nadhani ni dakika 15, misitu iliyofyekwa ni sawa na viwanja vya mipira
15. Tena hizi ni takwimu za chini na sehemu kubwa ni ukataji wa mkaa, kilimo kisicho endelevu, uzururaji wa mifugo, na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wataalam wa mazingira hapa, akina Mheshimiwa Dkt. Sware wanafahamu kwamba misitu ina thamani katika mifumo ya kiikolojia na utajiri wa nchi unapimwa kwenye mambo mengi; kuna utajiri wa watu wenyewe, utajiri wa vitu na utajiri wa maliasili. Katika nchi zinazoongoza duniani kwa utajiri wa maliasili, wanaita Natural Resources Wealth Per Capita. Tanzania ni moja kati ya nchi zinazoongoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka 20 iliyopita utajiri wa Tanzania kwa maliasili kwa maana thamani ya mito, maziwa, misitu, na kadhalika, thamani yake per capita inashuka kwa asilimia 35 kwa miaka 20 iliyopita, ingawa GDP per capita inapanda, lakini natural resources per capita inashuka chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dalili pekee ya kwamba maendeleo siyo sustainable ni pale utajiri wenu wa maliasili unaposhuka wakati utajiri mwingine unaenda juu. Kuna wakati hata ule unaenda utashuka utakutana na ule wa chini. Kwa hiyo, tuna wajibu mkubwa kuhakikisha kwamba maendeleo tunayoyatafuta ili yawe endelevu, hatuna budi kulinda maliasili zetu kwa nguvu zetu zote kwa sababu, ndiyo utajiri tulionao. Kwa hiyo, sisi ndani ya Serikali tunazungumza na wenzetu wa Wizara ya Maliasili na Wizara nyingine husika ili kuwa na makubaliano kuhusu mwenendo wa kulinda rasilimali za nchi zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, hili jambo tunazungumza na wenzetu kwamba sisi tunaamini msitu uliosimama na miti iliyosimama ina thamani hata kwenye kilimo kwa sababu hata mahindi ili yazae lazima kuwe na wale wadudu na nyuki wanaofanya polination nao wanatoka kwenye misitu. Ukipewa shamba sasa hivi lenye msitu, usipokata msitu unanyang’anywa kwa sababu hujaliendeleza, ehee! Nasi tunaamini kwamba msitu vilevile unaposimama na wenyewe una thamani yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili tunalizungumza kwamba kuna mwenzetu mmoja akiona mti umesimama anauona ni gogo na lenyewe ni chanzo cha mapato. Kwa upande mwingine ule mti pia unaweza kuuweka nyuki na kuzalisha. Kwa hiyo, ni mambo ambayo tunazungumza ndani ya Serikali ili kuhakikisha kwamba tunatunza nchi yetu; na maelekezo ya viongozi wetu, mmemsikia Mheshimiwa Rais alipokuwa Njombe alisema tulinde misitu yetu kwa nguvu zetu zote na mapori yetu yote. Imani yangu ni kwamba tutaendelea kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge tumewasikia kilio chenu kuhusu kasi ya ukataji wa miti na kasi ya nchi yetu kuwa jangwa. Ukombozi haupo kwenye kupanda miti, ukombozi upo kwenye kutunza miti iliyopo isikatwe, kwa sababu miti iliyopandwa haifiki asilimia nane ya miti yote iliyopo nchini. Tusipokata miti ni bora zaidi kuliko kuhangaika kupanda miti mingine. Kwa hiyo, huko ndiyo ambako jitihada zitaelekezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa kuhusu utendaji wa NEMC na nilizungumza asubuhi kuhusu reforms ambazo tunafanya. Tumepokea kabisa malalamiko kuhusu utendaji wa NEMC na malalamiko hayo ni ya kweli kwa sababu, kulikuwa na changamoto kubwa za ucheleweshaji wa vibali, gharama za vibali na mambo mengineyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeeleza kwa kirefu asubuhi hatua tunazochukua. Bahati nzuri tumepata uongozi mzuri, tunaye Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC ambaye tuko naye hapa, Profesa Asnath Chagu, tuna Mkurugenzi Mkuu mpya, anapanga safu yake vizuri. Tumesikia changamoto ya watumishi wachache wa NEMC, bahati nzuri wenzetu wa Utumishi wametusaidia, wametupa kibali cha kuajiri watu 30 mwaka huu, lakini zaidi ya hapo tumewaelekeza watu wa NEMC kwamba, kuna vijana wengi sana wamesoma mazingira na jiografia kwenye vyuo vikuu na hawana kazi na ni vijana wazuri na wasomi. Tumesema kwa sababu kazi za NEMC ni nyingi, wawachukue kwa mkataba kama interns na kuwatumia kwenye kazi za kwenda kufuatilia, kusimamia, na kadhalika, wapate posho na uzoefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa hivi tunao 40 na miezi michache tutaongeza 100 na mwaka ujao tutaongeza 100 wengine kuhakikisha kwamba footprints ya NEMC nchi nzima inakuwa kubwa. Tunafungua Ofisi za Kanda ili kuhaklikisha kwamba NEMC inatoa huduma kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, NEMC sasa hivi inabadilisha mtazamo wake kutoka taasisi ya kipolisi na kuwa taasisi ya huduma zaidi kwa wawekezaji na kwa wananchi. Nimewaambia watu wa NEMC, nyie mkionekana mnafunga viwanda, mnatoza fine, mnakusanya pesa, sawa ni kazi zenu, lakini ukisoma sheria mna kazi kubwa na muhimu zaidi ikiwemo utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, sheria inasema NEMC inapaswa kuweka orodha ya milima na vilima vyote nchini. Sheria ilisema, ndani ya miaka mitano baada ya sheria kuundwa kuwe na orodha iliyochapishwa kwenye Gazeti la Serikali kuhusu milima na vilima vyote nchini na hatari ya mazingira kwa vilima hivyo. Hiyo ni kazi ya NEMC. NEMC inaruhusiwa kumiliki maeneo yaliyolindwa kwa Sheria ya Mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutabadilisha mwelekeo wa NEMC ionekane ni taasisi kubwa na yenye heshima na yenye hadhi, siyo ya kufukuzana na watu na kuchelewesha vibali, na kadhalika. Kwa hiyo, mtaiona NEMC tofauti na tutaendelea kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niseme kwamba, tunataka uwekezaji na uwekezaji ni muhimu, lakini tunaamini uwekezaji lazima uende sambamba na hifadhi ya mazingira. Sasa nataka kusema, mtu yeyote ambaye anacheleweshewa kibali na NEMC au anaamini NEMC inamcheleweshea kibali, aje kwetu sisi moja kwa moja tutamsaidia papo hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho limezungumzwa suala la UNHCR Kigoma na madhara ya wakimbizi kwenye uharibifu wa mazingira. Tumeongea na wenzetu wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi kuhakikisha kwamba kwanza makambi yetu yanafanyiwa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) na hali ya mazingira inarejeshwa na kwamba wananchi pia wanapata manufaa na huduma ambazo wakimbizi wanazipata ikiwemo maji, na kadhalika. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge wa Kigoma hili tunalishughulikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la mfumo mzima wa usimamizi wa mazingira. Sheria ya mazingira imetengeneza architecture, mfumo wa usimamizi wa mazingira. Sheria ya Mazingira imetoa maelekezo kwa Wizara na Taasisi nyingine za Umma na binafsi, lakini hususan na Serikali za Mitaa kuhusu mambo ya kufanya. Kwa hiyo, Maafisa wa Mazingira wanaajiriwa na Halmashauri na kamati zinapaswa kuundwa kwenye ngazi ya Halmashauri. Kwa hiyo, kikubwa tunachofanya sisi ni kushirikiana na TAMISEMI kuhakikisha kwamba ule mfumo wa usimamizi wa mazingira ambao unahusu Wizara zote unasimamiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Mazingira inasema kila Wizara iwe na mratibu wa mazingira na kila Halmashauri iwe na Afisa Mazingira na kila Sekretarieti ya Mkoa iwe na Mratibu wa Mazingira. Kila kijiji kiwe na Kamati ya Mazingira, kila Kitongoji, kila Mtaa, kila Kata, kila Wilaya. Hapo ndipo mfumo mzima wa usimamizi wa mazingira utakuwa umekamilika na kwamba NEMC peke yake haiwezi kuwa kwenye kila Mtaa, kila Kijiji na kila Kitongoji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa tumeifanya katika mwaka uliopita kuhakikisha kwamba mfumo huu unakuwepo, kuna baadhi ya mikoa imefanya kazi nzuri sana ya kuhakikisha kwamba Mitaa yote, Vijiji vyote vina Kamati ya Mazingira na matunda tunayaona katika usimamizi wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala limezungumzwa la kutotosha fedha. Labda niseme tu kwamba fedha siku zote hazitoshi na hasa kwenye nchi kama yetu. Sasa ambacho nataka kusema ni kwamba kuna Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais ya Mazingira, pia kuna fedha za mazingira zinazokuja nchini katika ujumla wake. Ukiangalia Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais na ukaichukulia kwamba ndiyo fedha za mazingira hapa nchini utakuwa umefanya makosa. Nitatoa mfano kwamba, sisi Ofisi ya Makamu wa Rais tumewatafutia Wizara ya Maji fedha kwenye Mfuko wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabia-Nchi (Green Climate Fund). Tumehakikisha wamezipata. Fedha zile ni shilingi bilioni 250 ambazo zinaenda kuleta maji Simiyu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa zingekuwa kwenye bajeti yetu, si ajabu kusingekuwa na maneno. Kuna fedha zimepitia kwetu lakini ziko Wizara ya Kilimo; kuna fedha zimepitia kwetu, lakini ziko Wizara ya Mifugo. Kwa hiyo, inawezekana fedha zikaonekana hapa kidogo, sisi kazi yetu wakati mwingine ni kuwatafutia wengine fedha kupitia mikataba ya Kimataifa ambayo sisi ni wanachama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutaendelea kufanya hivyo. Tunaamini kwamba ni kweli rasilimali zinahitajika zaidi na tunaamini pale Mfuko wa Mazingira utakapokuwa umeanza kazi, basi na wenyewe utachangia katika kuhakikisha kwamba fedha zaidi zinapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala mengine yamezungumziwa ya GMO, Mheshimiwa Chiza; masuala ya matumizi ya maji kwenye umwagiliaji, masuala ya matumizi ya gesi na Mheshimiwa Ruth Mollel, ameongea kuhusu suala la nafuu ya kodi kwenye mitungi ya gesi ili kuokoa misitu. Hilo tutazungumza na wenzetu wa Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba linafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho ni kikubwa na cha msingi ni kwamba tunaona na tunafarijika sana na kupanuka kwa nishati mbadala ya mkaa. Kiwango cha gesi ya mitungi kinachotumika mwaka huu ni kikubwa mara mbili ya kilichotumika mwaka jana 2018 na tunaamini kadiri miaka inavyoenda na tunaona uwekezaji katika eneo hilo, imani yetu ni kwamba tutafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mita 60 nilizungumzia asubuhi kwamba tunaweka kanuni na utaratibu wa kuweza kuhakikisha kwamba tunafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani mambo yale makubwa na ya msingi, suala la elimu ya Muungano ni kweli lazima nikiri kwamba hatujafanya vizuri, wakati mwingine tunafanya mambo makubwa lakini hatuyazungumzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja kwamba vikao vya Muungano ni vya siri kwamba hakuna transparency, hiyo siyo kweli. Udhaifu wetu ni kwamba labda baada ya kikao tulipaswa kuitisha press conference ili watu wajue. Kwa hiyo, tumechukua maoni na ushauri kuhusu namna ya kuelezea wananchi kuhusu nini kinafanyika na ofisi zetu hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nirudi tena kwenye suala la Muungano kwa kifupi kwamba, kuna kazi nyingi sana kwenye Muungano zinafanyika hasa kupitia kwa viongozi wakubwa, hasa kupitia kwa wataalam, miradi, uhusiano na ushirikiano uliopo lakini mjadala wetu kuhusu Muungano umejikita kwenye changamoto. Sisi tunadhani kwamba tunayo kazi ya kuonyesha kwamba definition ya Muungano sio vikao vya changamoto bali ni mambo mengine mengi yanayofanyika ambayo hayaonekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nitoe ahadi kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba wale ambao hoja zao sijazigusa na hata wale ambao nimezigusa basi tutaziandika vizuri, tutatoa majibu vizuri na tutawapatia kabla Bunge la bajeti hii halijakwisha ili waweze kusoma majibu yao kwa sababu muda wa kujibu hapa wakati mwingine hautoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.

MWENYEKITI: Toa hoja.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima na taadhima kubwa, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.