Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ndiyo uliozaa jina Tanzania na ni wa kihistoria Afrika na duniani kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo nchi zinataka kufanya Muungano kama huu lakini zimeshindwa na pia zipo nchi ziliungana na baadaye muungano huo ulivunjika na sasa zinafanyika bidii za kujiunga upya na mfano ni Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika mwaka 1977 na sasa bidii na juhudi zinafanyika kuunda upya muungano huo (East Africa Community) kwa nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Southern Sudan. Ni mategemeo yangu Muungano wa watu wa pande hizi (Tanganyika na Zanzibar) utadumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, faida, changamoto na mustakabali; Watanzania kwa miaka mingi wamekuwa na umoja na mshikamano katika nyanja mbalimbali ambapo kwa kutekeleza haya ndiyo tunapata neno Muungano. Kihistoria tokea miaka mingi iliyopita tangu dunia iumbwe, makabila na watu wa maeneo mbalimbali katika Tanganyika, wamekuwa na ushirikiano na mahusiano ya karibu. Mfano ni katika harakati za kuondoa uonevu, ukandamizaji na ubaguzi uliokuwa ukifanywa na Wakoloni Wajerumani mnamo mwaka 1905 hadi mwaka 1907.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Vita ya Minonge katika maeneo ya Ukanda wa Pwani Tanga, Pwani, Dar es Salaam na Zanzibar, mikoa hii makabila yake yalishirikiana kuondoa uonevu hali iliyopelekea kutokea Vita ya Kwanza ya Dunia (1st World War 1914-1918). Hii yote ni kuonesha namna muungano ulivyokuwa na umuhimu na faida kwa jamii. Hivyo, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulianzia miaka mingi na hadi katika Mapinduzi ya Zanzibar 1964. Mchango mkubwa ulitokea Tanganyika (Tanzania Bara) na kufanikiwa kuondoa ukandamizaji uliokuwa ukifanywa na Wakoloni wa Kiarabu katika Visiwa vya Unguja na Pemba (Zanzibar).

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi na ushauri; Serikali izifanyie kazi kero zote za Muungano na kuzipatia ufumbuzi wa haraka; Sera ya kulinda viwanda vya ndani ifanye kazi pande zote za Muungano, mfano Kiwanda cha Sukari Mahonda kiruhusiwe kupata soko la sukari na bidhaa zake upande wa Tanzania Bara. Magari yaliyosajiliwa Zanzibar yaruhusiwe kutumika Tanzania Bara bila vikwazo vyovyote; kero na changamoto zinazofanyiwa kazi, taarifa zake ziwekwe wazi na isiwe siri; gawio la Pato la Taifa, deni la TANESCO, suala la FIFA, Exclusive Zone katika Bahari Kuu yafanyiwe kazi na yaishe; suala la mafuta ya gesi, zote hizi ni sekta ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi na kupata ufumbuzi. Mfumo wa Serikali tatu (Serikali ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Shirikisho ndio ufumbuzi wa kudumu).

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira ni neno lenye maana pana sana ambalo bado Watanzania wengi hawajalielewa maana yake na bahati mbaya bado Serikali haijatoa elimu ya kutosha kwa kutumia vyombo vya habari, vipeperushi na Taasisi zake katika jamii ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira katika Tanzania yanaingiliana sana na shughuli za uzalishaji mali (kutafuta riziki) kwa wananchi wake kama vile kilimo, uvuvi, ufugaji na shughuli za viwandani. Sheria nyingi na Kanuni zinatungwa bila kuwashirikisha wananchi ili wazielewe na kuzifanyia kazi, badala yake Sheria zinatumika kuwakandamiza wananchi na pale wawakilishi wao tunapotetea (Wabunge, Madiwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa) tunajibiwa ignorance of laws is not a defence na inaonekana Serikali inatumia makosa yanayofanywa na wananchi kujipatia faini (fedha) na kuwa chanzo cha mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji, wakulima na wawindaji wamekuwa wahanga wakubwa katika suala zima la mazingira, hivyo Serikali katika hili ifanye kazi ya ziada kwa kutoa elimu ya kutosha. Sheria ya kuacha mita 60 ya vyanzo vya maji katika shughuli za uzalishaji mali ni mpya, iwekwe vizuri na itolewe elimu ya kutosha ili kuondoa mkanganyiko uliopo hususan pale ambapo sheria imekuta mwananchi ameshaanza kufanya kazi (kabla Sheria kuanzishwa), Serikali imfidie kwa eneo litakalotwaliwa na sheria hii katika ngazi za Serikali za Vijiji, Serikali za Mitaa, Halmashauri za Manispaa na Halmashauri za Majiji kwa thamani ya fedha katika soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira inatengewa fedha ndogo sana na mfano katika bajeti ya 2018/2019, bajeti iliyotengwa hadi mwaka wa fedha unaoishia ni shilingi bilioni 1.7 tu ndiyo iliyopokelewa hali inayoonesha Serikali haitilii maanani suala la Mazingira.