Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza niwapongeze sana Mawaziri wanaosimamia Wizara hii kwa namna ambavyo wanajitoa kuhakikisha wanasimamia Muungano, lakini pia upande wa mazingira. Waendelee kufanya ziara nyingi kwa sababu mazingira kwa kweli yameharibika kwa kiasi kikubwa na Muungano unahitaji kusemewa kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwangu kuna tatizo moja; kuna mtaro mmoja unatiriri nafikiri ni maji ya sumu, nimeshawahi kulizungumza hili hapa Bungeni na leo ni mara ya pili. Kwenye Kata ya Sandari kule Temeke Mikoroshini, kuna mtaro wa mfereji wa Mpogo, yake maji yanaoneka yanatoka kwenye moja kati ya viwanda vilivyoko Vingunguti, nyumba zilizokuwa pembeni bati zinaharibika na matofali yanamung’unyuka. Hali hii inaonesha kabisa kwamba pale kuna sumu inatembea na kama matofali yanamung’unyuka maana yake afya za watu wanaoishi pale ziko kwenye hii changamoto kubwa. Kwa hiyo, naomba hili jambo walichukue na walifanyie kazi kwa haraka. Sisi kama Halmashauri tumeshatenga fedha ya kuujenga ule mfereji, lakini haiondoi ukweli kwamba maji yanayotiririka yanakuwa na sumu. Hilo moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naitaka Wizara wawe wanatupa taarifa za mara kwa mara za uchafuzi wa mazingira katika Jiji la Dar es Salaam. Tunapata taarifa ambazo zinaleta sintofahamu kidogo, kuna wakati tunaambiwa kwamba mabonde yale hayafai hata kwa kulima mbogamboga za majani, kuna wakati tunaambiwa water table ya Dar es Salaam yote imechafuka hata maji ya visima tunayoyatumia si mazuri. Sasa ni vizuri wakawa wanatuandalia taarifa za wazi na za kina ili tujue kitu kipi tufanye na kitu kipi tusifanye. Maana yake sasa tukienda sokoni tunaogopa michicha tunaogopa matembele, tunahisi yamelimwa kwenye yale maeneo ambayo yana sumu. Ikiwezekana waweke hata mabango tujue kwamba eneo hili linastahili, eneo hili halistahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, sheria ambazo zinatumika na NEMC kwa kuwaadhibu wanaochafua mazingira, ziangaliwe upya, inawezekana ni za Ulaya sana. Kwa mfano, mtu mwenye garage anatakiwa awe amesakafia na kuwe na system ya kutofautisha maji na oil. Garage zetu nyingi hazijasakafiwa, kwa hiyo kinachofanyika ni kama tumetengeneza mwanya wa watu kupiga fedha. Leo mtu anapelekewa notice kwamba hii garage uisakafie ndani ya siku 14, jambo ambalo haliwezekani. Akija siku ya pili, yule mtu atakachofanya ili asitozwe faini ya milioni tano, atamuona tu pembeni huyu mtu, kwamba bwana usiniandikie, chukua hii milioni moja, chukua hii laki mbili, sasa watu wataishi hivi mpaka lini? Lazima tuwe na sheria ambazo zinaendana na mazingira yetu, je tuna uwezo kwenye kila car wash kuwa na hiyo system ya kuchuja maji na oil. Magari yetu yenyewe ya mitumba, likisimama tu hapo linavuja oil, mtu anatakiwa awe na system ya kuchuja hiyo kitu, hii inawezekana vipi? Kwa hiyo, tuziangalie hizi sheria kama kweli ni rafiki na zinaweza kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ni la Muungano; nimeshtushwa sana, mtu aliyesimama hapa kusema kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi haiutaki Muungano tena na yeye anasimama akitoka CUF. CUF wanaamini kwenye madaraka kamili, mamlaka kamili, mamlaka kamili maana yake Zanzibar isimame kama nchi tofauti na Tanzania Bara isimame kama nchi tofauti, sasa hapa ni nani asiyeupenda Muungano? Kwa hiyo, nafikiri kwenye jambo hili la Muungano, ni vizuri tukawa wakweli, kwamba hizi nchi mbili, Tanzania Bara na Tanzania Visiwani, zinahitajiana sana whether tuko ndani au nje ya Muungano. (Makofi)

MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumekubali tuko ndani ya muungano ni vizuri….

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mamlaka ya Zanzibar ambayo ni kupata fursa zaidi za kiuchumi hususan katika nyanja za kimataifa, haliharamishi kutokuwepo Muungano. Tuna mifano mingi, tuna European Union, ni Muungano una nchi kadhaa, lakini kila nchi si ina mamlaka yake! Kwa hiyo, suala la kujadili, Mheshimiwa Mtolea, suala la kusema kwamba eti kwa sababu kuna watu wanazungumzia suala la kwamba Zanzibar iwe na mamlaka kamili, hawataki Muungano, hii siyo sahihi. Suala la mamlaka kamili ni suala la kuwepo kwa Serikali tatu….

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Mtolea endelea.

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siipokei hiyo taarifa yake. Tunapozungumzia Muungano wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, tunazungumzia kitu tofauti sana. Huwezi kufananisha na miungano mingine hiyo sijui ya European Union na sehemu nyingine. Huu ni muungano wa kipekee, una historia ya kipekee na mazingira yake ni ya kipekee. Sasa ukianza kusema kwamba tunakosa fursa, si kweli na wakati mwingine eti mtu anasema kwamba tumechoka kubebwa kwenye koti la Muungano, hivi aliyebebwa anaweza akaanza kuchoka kabla ya aliyembeba? Maana yake aliyekubeba anavumilia kwa sababu anafahamu thamani ya anachokifanya. Mama akimbeba mtoto, si kwamba eti mtoto aanze kuchoka eti mama hajachoka, lakini Mama anaendelea kumbeba kwa sababu anajua ni jukumu lake na ndicho Tanzania Bara wanachokifanya… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)