Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. John John Mnyika

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora aya ya 37(xii), madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi wa Umma 34,346 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 79 inaonyesha hayajalipwa mpaka sasa. Hata ya shilingi bilioni 29 ambayo yamehakikiwa nayo hayajalipwa mpaka sasa. Serikali iache kutumia kisingizio cha uhakiki mwingine wa Wizara ya Fedha kuendelea kuchelewa kuwalipa wafanyakazi madai yao ya mishahara. Hivyo katika majumuisho, Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge, ni lini hasa madai hayo ya wafanyakazi yatalipwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, katika aya ya 51 na 78 zinazohusu Bodi ya mishahara na masilahi katika utumishi wa Umma, zinaonesha kwamba Serikali haijafanya maamuzi ya kupandisha mishahara ya watumishi wa Umma. Bado Serikali inajificha katika kivuli cha kufanya utafiti wa hali ya maslahi ya watumishi wa Umma na kuandaa taarifa za gharama za maisha, kukwepa kupandisha mishahara ya watumishi wa Umma. Visingizio kama hivi vimetolewa katika hotuba za 2016/ 2017, 2017/2018 na 2018/2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo ni vyema ripoti ya utafiti iliyotajwa kwenye aya ya 51 na taarifa mbili za gharama za maisha ziwasilishwe Bungeni na Bunge katika majumuisho ya mjadala wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora itangazwe kwamba mishahara ya watumishi wa Umma itaongezwa katika bajeti hii ya mwaka wa fedha 2019/2020. Pia ili kukabiliana na gharama za maisha, ni vyema Serikali ikawapunguzia mzigo wafanyakazi wote wa Sekta ya Umma na Binafsi kwa kupunguza kiwango cha kodi ya mapato kwa wafanyakazi (PAYE) kama ilivyowaahidi wafanyakazi kwa nyakati mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu agizo la Serikali la watumishi wa Umma wa Wizara na Taasisi zake kuhamia Dodoma. Kuna umuhimu kwa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na wakala zilizo chini yake kufanya utafiti juu ya athari za maamuzi hayo yaliyofanyika bila maandalizi ya kutosha kwa maisha ya watumishi wa Umma. Watumishi wa Umma walipokuwa Dar es Salaam wapo ambao wenzi wao wanafanya kazi katika sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Dodoma Sekta Binafsi haijapanuka kwa kiwango cha kuwezesha wenzi wa wafanyakazi hao nao kuweza kuhamia Dodoma kwa haraka haraka. Matokeo yake ni kuwa, kuna familia nyingi zimetenganishwa hali ambayo italeta athari za muda mrefu na kuathiri utendaji wao kwa kipindi cha muda mfupi. Aidha, kwa wafanyakazi wa kada ya chini na kati, hali hii ya kuwa na Miji miwili; Dar es Salaam na Dodoma kwa mishahara yao midogo, imeleta madhara ya kiuchumi kwa watumishi wa Umma.