Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Rev. Peter Simon Msigwa

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Na mimi nataka nitoe mchango wangu kuhusiana na Wizara hii ya Viwanda. Mheshimiwa Waziri nashukuru umekuwa unaongea sana na unapojibu maswali kama vile bado tuko kwenye kampeni. Tunatagemea sasa hivi hapa utupe data za uhalisia namna utakavyokwenda ku-earth majukumu yale ambayo Mheshimiwa Rais amekupa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua Mheshimiwa Rais amesema anataka nchi hii, jambo ambalo ni jema, iwe ni nchi ya viwanda kwa maana ya uchumi wa viwanda. Nchi hii wahitimu kwa mwaka ni 800,000. Katika majukumu ambayo Mheshimiwa Rais amekupa wewe kama Waziri amesema 40% ya wahitimu 800,000 anataka waende kwenye viwanda. Katika 40% ya hao watu 800,000 ni watu 320,000 maana yake hawa tunawaingiza kwenye viwanda. Kwa nchi hii kiwanda kikubwa ambacho kimewahi kuajiri watu wengi sana hawazidi 5,000. Sasa twende kwenye hesabu za haraka haraka maana ukija hapa unakuwa kama unafanya kampeni, twende kwenye hesabu za haraka haraka za kawaida tu. Ili lengo lako hilo la kuajiri watu 320,000 kwa mwaka lifikiwe maana yake unatakiwa uwe na viwanda 530 katika kipindi cha miaka mitano ya Ilani yenu ya Uchaguzi ambayo mnajisifu nayo. Hoja inakuja hapa mwaka huu sasa tunakwenda nusu una viwanda vingapi? Naomba utujibu hapo, una viwanda vingapi mpaka sasa? Utatutajia cha Dangote, alikiacha Mheshimiwa Kikwete ambaye sasa hivi mnamzomea, ninyi hamjatengeneza hata kimoja, una viwanda vingapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wafanyabiashara wanataka kuongea na Serikali yako, mnawakatalia, mnawa-frustrate, hamkai nao. Bado mnasema mna wawekezaji kutoka nje wakati hawa hawa waliomo ndani hamuwezi kuwa-handle vizuri. Ningekuomba Mheshimiwa Waziri hebu tuache mbwembwe tuwe realistic, hizi hesabu zinakataa, huna uwezo huo. Saa hizi hata viwanda viwili vipya huna! Ukinionesha viwanda vitatu umetengeneza nitakupa Land Cruiser yangu hapo nje kama unavyo, toka mmeingia Serikali hii, huna hivyo viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mnakuja hapa mnatupa takwimu za uongo, za kutuaminisha matumaini ambayo hayapo, hauna viwanda hivyo. Ukipiga hesabu hawa watu huwezi kuwapeleka, kiwanda kikubwa kinachoajiri watu sasa hivi ni Breweries inapeleka watu 3,000. Hawa watu 320,000 kwa mwaka where are you going to employ them, wapi utaenda kuwaajiri? Tunaomba unapokuja utuambie hesabu za uhalisia, hatuko kwenye kampeni, tunataka utuambie ukweli! Naomba hilo usije na majibu mepesi mepesi, hivyo viwanda hauna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ndugu yangu hapa amezungumza, infrastructure ya umeme iko wapi, umeme wa uhakika uko wapi mpaka sasa unaowaita hao. Umetuambia Jumatatu tuje tugawane hapo, hatuwezi kugawana watu kama njugu wakati hakuna infrastructure yaani mimi nitaondoka na mwekezaji nasema naenda naye Iringa naenda naye wapi! Tukafanye nini? Mazingira yaliyoandaliwa yako wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri mimi ningeomba hebu tuambizane ukweli na ninyi ndio mtakaokwenda kumuangusha Mheshimiwa Magufuli kama mkija na mbwemwbwe ambazo hazina uhalisia. Mtupe mambo ambayo yanawezekana. Nimekupa hii takwimu uikatae! Unahitaji kuwa na viwanda 530 ndiyo uwapeleke hawa 40% kwenye hivyo viwanda unavyosema unakwenda kutupa na kuwaaminisha Watanzania kwamba nchi itakuwa ya viwanda, mambo yatakuwa mazuri, utupe figure ambazo ni za uhalisia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine amezungumza Mheshimiwa mwenzangu hapa kuhusiana na hawa wafanyabiashara wadogo wadogo ambao tumezungumza sana hata miaka mitano iliyopita tunawaona kama ni kero katika nchi yetu badala ya kuwaona ni fursa. Kwa hiyo, hebu tu-change, is a mindset thing. Change what you see by changing how you see. Tunapowaona wale watu ni kero ndiyo tunagombana nao na mabomu badala ya kuweka mikakati ya kuwafanya hawa watu wawe na tija kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu ni wengi sana wangetafutiwa maeneo. Tumezungumza sana na mwaka jana tulitoa mpaka na maazimio kwenye eneo hilo kuhakikisha miji yote yatengwe maeneo walao kila weekend maeneo yale yafunguliwe, haya mambo yamekuwa yakisuasua katika maeneo mbalimbali. Naona hapa kwa mfano Dodoma imeshaanza na maeneo mengine lakini tumekuwa tukiwapiga hawa Wamachinga, tumekuwa tukiwaonea, hatuwatengenezei mkakati mzuri. Kwa sababu wao kama alivyosema ndugu yangu hapa, ndiyo wako kwenye field wengine wote hapa tunaongea nadharia tu lakini wao wako kwenye field ndio wanaliona soko lilivyo.
Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri, tungeomba hili tatizo nalo lipate ufumbuzi wa kudumu na wa moja kwa moja badala ya kuwaona hawa watu ni kero tuone kama ni fursa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi kwenye suala la viwanda, kwa mfano Mwanza kuna kiwanda kilikuwa cha nyama ambacho kilikuwa cha Tanganyika Packers, wakaja wakawekeza wawekezaji hakikwenda vizuri. Wakaja watu wa nje, baadaye wakaja Wamarekani, Wamarekani baada ya matatizo yao ya uchumi, hakipo. Leo Mheshimiwa unasema kwamba watu waje, kile kiwanda kule tatizo ni nini? Vilivyopo vimeshindwa nini na sasa hivi unatuaminisha kitu gani kitasababisha hivyo viwanda vilivyopo kwenda mbele? Vile vilivyoshindwa vilishindwa kwa nini na sasa hivi kwa nini unatuaminisha kwamba hivyo vilivyopo tutasonga mbele? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hebu tuache mambo ya kampeni. Uchaguzi mlishashinda whether mlituibia kwa magoli ya mkono, it is fine, mlishinda, Serikali ni ya kwenu.
Sasa hapa hatuhitaji kampeni, tupeni vitu ambavyo mnakwenda ku-earth. Hatutaki mbwembwe! Mheshimiwa Mwijage acha mbwembwe, tupe vitu ambavyo ni practical. Mwalimu wangu alikuwa anasema how can you earth it?
Tuambie unawezaje kutuambia kwenye ground? Tuna viwanda vingi sana, Iringa tulikuwa na viwanda vingi vya akina-TANCUT vile vyote vimekufa. Ukienda Mbeya hivyohivyo, ukienda Morogoro hivyohivyo. Sasa hivi mnakuja na lugha nzuri sana, very testy lakini ukienda kwenye uhalisia, hii hesabu ni ndogo sana nimekupa, it doesn’t work brother. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba atakaporudi hapa atatupa majibu. Hii ni hesabu ndogo sana huhitaji kuwa na elimu ya Chuo Kikuu, ndogo tu. Utupe majibu namna gani hii kazi aliyokupa Mheshimiwa Magufuli ya kuhakikisha 40% ya wahitimu 800,000 wanaingia kwenye viwanda, ni viwanda vipi? Mpaka saa hizi huna hata kimoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niliweke wazi hilo, tuache mbwembwe, tuambizane ukweli hapa ili tuisimamie Serikali. Nikushukuru sana kwa kunipa nafasi.