Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe na Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama na kutoa mchango katika hoja hii muhimu ya Makadirio ya Mapato na Matumishi ya Ofisi ya Rais, Utumishi kwa mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kuunga mkono hoja kwa sababu Serikali inafanya kazi nzuri ya utawala bora unaozingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nampongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wengine kwa kazi nzuri wanayofanya na kwa kuandaa na kuwasilisha vizuri hotuba yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi, napenda kutoa ushauri katika maeneo machache yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kuhusu uhaba wa wafanyakazi. Pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ya kuajiri wafanyakazi katika sekta mbalimbali kama ilivyoelezwa kwenye hotuba ya Waziri bado tatizo la wafanyakazi ni kubwa sana na hasa katika sekta za afya, elimu na kadhalika. Nashauri Serikali iendelee kutafuta fedha kwa ajili ya kuajiri watumishi hasa katika sekta ya afya na elimu na hasa walimu wa sayansi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili niwatumishi wa kujitolea.Nashauri Serikali ianzishe mpango wa wafanyakazi wa kujitolea katika kada mbalimbali kama ilivyokuwa ikifanyika zamani. Hii ni kwa sababu wataalam tunazalisha wa kutosha na hawana ajira, hivyo, wakipata hata kazi ya kujitolea wataendelea kuongeza maarifa na uzoefu na kutoa mchango kwa taifa na nafasi zikipatikana wao ndiyo wapewe kipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu ni kuhusu vibali vya kuajiri watumishi kupitia vyanzo vya ndani. Zipo taasisi ambazo zina uwezo wa kuajiri watumishi kupitia vyanzo vya ndani. Nashauri taasisi hizo zitambuliwe na kutoa nafasi za kuajiri watumishi kupitia vyanzo vya ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika,nne ni upekuzi kwa viongozi na watumishi (vetting). Zoezi la upekuzi kwa watumishi wanaostahili kuongezewa madaraka lifanyike kwa wakati ili kupunguza tatizo la upekuzi kufanyika kwa muda mrefu na hivyo Halmashauri nyingi kukumbwa na tatizo la kuwa na watu wanaokaimu. Zoezi la upekuzi liendelee kufanyika kwa umakini na uadilifu ili kutotoa mwanya kwa watendaji na viongozi wasio waaminifu na waadilifu kupenya na kupewa nafasi katika vyombo mbalimbali vya maamuzi na umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nne ni mpango wa TASAF.Naungana na Kamati kuwa uhakiki wa kuondoa kaya zisizostahili ufanyike kwa umakini na uadilifu mkubwa ili wasiostahili waondolewe na wanaostahili wanufaike na mpango wa kuhudumia kaya masikini ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo kwa kaya zingine zinazostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, tano ni kuhusu TAKUKURU kudhibiti mali za umma. Napongeza TAKUKURU kwa kuendelea kufuatilia vitendo vya rushwa katika kutekeleza miradi ya maendeleo na katika taasisi za umma za kutoa huduma. Nashauri jitihada ziendelee ili kuokomesha vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya mali za umma ili nchi yetu iweze kufikia maendeleo tunayoyataka.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.