Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi wa kwanza, hasa nikiwa kwenye Kwaresma hii na wiki hii ambayo ni ya mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na utawala bora katika hii wiki ya mateso, tumesikia kwenye vyombo vya habari Mkuu wa Majeshi alikuwa anamwambia Rais Magufuli kwamba yeye aachiwe kazi anachunguza mambo ya uchochezi kwa wanasiasa kwa kauli ambazo zinaenda kuvunjisha amani. Sasa katika utawala bora nataka Serikali inipe majibu, je, Mkuu wa Majeshi wa nchi hii amekuwa DPP? Anasema anafanya uchunguzi yeye anajiingiza moja kwa moja kwenye siasa? Y44eye ndiyo anataka kuiingiza nchi katika matatizo makubwa. Nakemea kwa nguvu zote na ashindwe katika Jina la Yesu. (Makofi)

WABUNGE FULANI: Amen. (Makofi)

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda katika masuala ya TAMISEMI kwa sababu nina dakika tano, niende moja kwa moja kuhusu masuala ya walimu.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, dakika zangu ni tano tu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jenista.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu kumpa taarifa ili tuliweke suala hili vizuri. CDF hakusema kwamba anachunguza wanasiasa, yeye alizungumzia masuala ya amani, utulivu, ulinzi na usalama kwa ujumla wake na hakusema wanasiasa, ni lazima tuliweke vizuri jambo hili. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, wakati mwingine kauli zile hasa ambazo hatuna uhakika, zinazohusu viongozi wengine…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Tusikilizane vizuri, hasa ambazo hatuna uhakika nazo tuwe waangalifu kwa sababu mimi nilikuwepo na alisema wanafuatilia siyo wanachunguza. Kwa hiyo, ndio maana nasema tuwe waangalifu, sisi wenyewe ni viongozi na kauli wanazotoa wengine tunapotaka kuzisema kwa namna fulani tuwe na hakika na kile kilichosemwa. (Makofi)

Mheshimiwa Susan Kiwanga, endelea.

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nadhani umenilindia muda wangu. Hata kama nimekosea kusema lakini kufuatilia, yeye kwa mujibu wa Katiba anafuatilia masuala ya watu mbalimbali hapa nchini? Je, DPP atafanya kazi gani? Kifungu kipi cha Katiba
kinamruhusu yeye aseme anafuatilia wachochezi? Yeye alinde mipaka bwana ya nchi yetu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu masuala ya walimu, katika vitabu vyao TAMISEMI wanasema wanaenda kuajiri walimu elfu nne lakini ndani ya Wilaya ya Kilombero tuna upungufu wa walimu 1,018. Kati ya hawa walimu elfu nne watakaoajiriwa, je, elfu moja na zaidi ndiyo wanaenda Kilombero na wilaya nyingine watapata nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba wajiri walimu, tumechoka kusubiri, elimu haisubiri. Watu wanazidi kuwa mambumbumbu huko chini, tunazidi kuliangamiza Taifa. Leteni haraka ajira za walimu na mishahara, posho na madaraja yao wapandishwe. Wafanyakazi nchi nzima hawajapandishwa madaraja, wanasoma lakini hawabadilishiwa mishahara. Naomba TAMISEMI na Utawala Bora mshughulikie masuala haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyakazi nchi nzima hawajapandishwa madaraja, wanasoma lakini hawabadilishiwa mishahara. Ninaomba katika Utawala Bora na TAMISEMI mwelekeze hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu masuala maalum. Ndani ya Jimbo la Mlimba kuna masuala mengi ambayo yanahusu TAMISEMI. Kuna madaraja kuhusu TARURA. Naomba TARURA waongezewe hela ili tupate kujengewa madaraja na barabara katika maeneo yetu, kwa sababu tumechoka kusubiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuhusu masuala ya maji, pale Mlimba hakuna maji, kuna kisima kimoja tu na ule mji unazidi kukua. Kwa hiyo, tunahitaji maji ya kutosha ili wananchi wapate maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Mlimba, ni miji. Ndani ya Jimbo la Mlimba kuna miji kadhaa ambayo inakua ovyo ovyo. Ilishatamkwa kwamba kuna Mji Mdogo wa Mlimba, lakini mpaka leo unatamkwa vijiji. Katika bajeti hii na uchaguzi unaokuja, tunaomba Mlimba tusitoe tena vijiji, tunataka tuchague vitongoji. Kwa hiyo, TAMISEMI nawaomba chonde chonde angalau mtupe mji mmoja wa Mlimba ili tuone tunapanga vizuri mji wetu usiwe ovyo ovyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu masuala ya uendeshaji wa miji midogo. Sasa kama Mlimba hakuna miji midogo, miji haipangwi tutaendeshaje hiyo miji. Kwa hiyo, naomba chonde chonde haya mambo yafanyike. Nitafurahi sana na wananchi wa Mlimba watafurahi sana kama mtatangaza Mji Mdogo wa Mlimba uanze kazi katika Serikali ya Mitaa hii inayokuja, wachague vitongoji siyo viji tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu masuala ya Tume Huru ya Uchaguzi. Tume Huru ya Uchaguzi ni muhimu sana. Kiatu usichovaa huwezi kujua kinabanaje. Nimeshuhudia mwenyewe kule Malinyi, Sophy, Mkurugenzi anamtangaza Diwani wa CCM aliyeshindwa kwa kula 29 anamtangaza wa CCM anamwacha wa CHADEMA. Mpaka leo nina kesi Mahakamani. Ili kuvunja soo, wakanikamata wakanipeleka mahabusu ili nisifuatilie hiyo kesi Mahakamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, huo utawala bora sisi ndio tunaumia, sio ninyi mlioko upande huo. Nilisikitika sana na Kwaresma hii, ndugu yangu Mheshimiwa Jenista akisema Tume iko huru, sijui nini. Uhuru gani? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)