Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Joseph Michael Mkundi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ukerewe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia. Kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii ya uhai na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu lakini nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa sababu ni bajeti yangu ya kwanza nikiwa upande huu lakini hasa kwa sababu ni bajeti ya kwanza tokea limetokea tukio baya sana la kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere, nitumie nafasi hii kumwomba Mwenyezi Mungu ampumzishe roho za marehemu wote 228 waliopoteza maisha kwenye ajali ile. Tatu, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa sana anayoifanya kuliongoza Taifa hili na kuwaletea maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Jafo na wasaidizi wake na Mheshimiwa Mkuchika na wasaidizi wake wote. Hakika wanafanya kazi kubwa sana, wanatendea haki Wizara zao na wanawatendea haki wananchi wa Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utakuwa kwenye maeneo mawili. La kwanza niombe tutambue kwamba tunaweza kwenda kasi sana kwa maendeleo katika nchi hii kama tutakuwa na Serikali za Mitaa zilizo imara. Kimsingi tunaposema uimara wa Serikali za Mitaa ni kwa sababu huduma zote za kijamii ziko chini ya Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, kama tutaimarisha Serikali za Mitaa, kasi ya maendeleo kama inavyokwenda sasa itakuwa nzuri na itawagusa zaidi wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingawa mpaka sasa mambo yanaenda vizuri, naipongeza Serikali kwa kazi kubwa sana wanayoifanya kwa mfano Ukerewe kwenye eneo la afya kazi kubwa sana imefanyika, vituo viwili vimepata pesa, vinakamilika. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI lakini nimpongeze zaidi Mheshimiwa Rais kwa sababu baada ya matatizo yale alielekeza pesa zijenge Kituo cha Afya cha Bwisya, kituo kinaelekea kukamilika na naipongeza sana Serikali kwa uamuzi huu. Tatizo kubwa ambalo napenda Serikali itambue, ujenzi wa vituo hivi vya afya iende sambamba na upatikanaji wa watumishi ili viwe na tija, visikamilike halafu vikashindwa kutoa huduma ile iliyokuwa inatarajiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la elimu kazi kubwa sana imefanyika kupitia elimu bila malipo, watoto wengi sana wameweza kusajiliwa kwenye shule zetu za msingi. Kusajiliwa kwa watoto wengi kumeenda sambamba na upungufu wa miundombinu kama madarasa. Niipongeze sana Serikali hivi karibuni imejitahidi kuleta pesa kwa ajili ya kuboresha miundombinu na kwenye eneo letu la Ukerewe kupitia Mfuko wa Jimbo lakini pamoja na wananchi, niwapongeze sana wananchi wa Visiwa vya Ukerewe, tumehamasishana tumejenga maboma zaidi ya 300 kwa ajili ya madarasa, niombe Serikali sasa itusaidie kuezeka madarasa haya. Kwa sababu wananchi wamejitoa sana na Mbunge wao nimejitoa, nimepeleka mifuko zaidi ya 3,000 kwenye shule zetu mbalimbali, basi Serikali itusaidie tuweze kuezeka maboma haya ili angalau watoto wetu wapate madarasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwenye utekelezaji nimeona kuna wazee zaidi ya 700,000 wametambuliwa lakini katika wazee hao ni asilimia 33 tu ya wazee hawa ndiyo waliopata vitambulisho ili waweze kupata huduma ya afya. Kuna tatizo kubwa sana huko chini, wazee wetu wananyanyasika sana wanapokwenda kupata huduma za afya. Niombe Wizara ya TAMISEMI iweke ukomo wa muda ili Halmashauri zetu ziweze kuwatambua wazee hawa na kupata vitambulisho ili wapate huduma za afya kuliko kuendelea kunyanyasika kama ambavyo imekuwa inatokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende eneo la TARURA, wamesema Wabunge wengi sana, niwapongeze TARURA lakini nampongeza sana Mtendaji Mkuu wa TARURA amekuwa msikivu pamoja na changamoto mbalimbali anazokabiliana nazo. Kwa kazi kubwa wanazozifanya TARURA tukizingatia kwamba wana mtandao mkubwa sana wa barabara kilomita zaidi ya 100,000 ni nyingi sana lakini kwa fedha wanazozipata tutaendelea kulalamika. Kwa hiyo, niombe katika bajeti tunayoendelea nayo Serikali ilete pendekezo tuweze kubadili fomula ya ugawaji wa pesa hizi ili TARURA angalau waweze kupata asilima 40 au asilimia 50 tuweze kuwapa uwezo washughulikie barabara zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipoanza kuzungumza nilisema juu ya umuhimu wa kuimarisha Serikali za Mitaa na hasa Halmashauri zetu kwa sababu ndipo sehemu ambapo miradi mingi inayowagusa wananchi inasimamiwa. Tunapoongelea Serikali za Mitaa hasa Halmashauri tunaongelea Madiwani na watumishi. Kuna changamoto kubwa katika suala zima la posho kwa ajili ya Madiwani wetu. Hili ni tatizo kubwa sana ambalo linaathiri utendaji wa Madiwani wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni umetolewa mwongozo juu ya posho za Madiwani katika vikao vyetu vya Halmashauri. Madiwani hawa wanafanya kazi kubwa sana lakini wanapokwenda kuhudhuria vikao wanalipwa Sh.40,000 ni fedha ndogo sana. Kwa hiyo, niombe TAMISEMI muangalie upya suala hili ili angalau kuweza kuwajengea kujiamini Madiwani hawa ambao wanafanya kazi kubwa sana ya kusimamia miradi yetu kule chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji, hawa ni watu muhimu sana lakini malipo wanayopata; posho zao za kila mwezi lakini hata baada ya kutoka kwenye nafasi zao wanazotumikia ni kitu gani wanakipata? Nashauri TAMISEMI aingalie eneo hili pamoja na kwamba inawezekana wakawa wengi sana Serikali isiweze kuwalipa wote lakini tuangalie kama inawezekana baada ya kipindi chao cha utumishi kuwe na package fulani ambayo wanaweza kuipata ili wawe na moyo wa kuendelea kufanya kazi na kusimamia maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano Ukerewe, Mwenyekiti wa Kitongoji analipwa Sh.3,000 kwa mwezi. Tafsiri yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba kwa siku analipwa Sh.100 kwa ajili ya kusimamia shughuli za maendeleo, inawavunja moyo. Kwa hiyo, niombe Serikali iliangalie sana suala hili.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)