Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Freeman Aikaeli Mbowe

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niungane na wenzangu kuchangia katika hoja hii ya Ofisi ya Rais TAMISEMI na Utumishi na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanzia hapo ambapo amemalizia Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe, kuzungumzia hoja ya utoaji haki katika Taifa na hilo suala amelizungumza vilevile Mheshimiwa Mama Tibaijuka. Nalizungumza kama mhanga ambaye nimekaa Magereza kwa siku 104 na Mheshimiwa Matiko na fursa ile ya kuishi Magereza imetupa nafasi kubwa sana ya kujua hali halisi ya nchi yetu. Imetupa nafasi ya kujua hali halisi sisi Wabunge tunapotunga sheria tunafikiri sheria hizi hazituhusu, kwa hiyo, tunatunga sheria nyingine ambazo ni ngumu na mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umekuwa ni utamaduni wa Serikali kugeuza kesi za money laundering kama chanzo cha mapato ya Serikali, yaani inaonekana kama kesi za money laundering ni mkakati mpya wa kukuza mapato ya Serikali. Watu wanakamatwa, uchunguzi unaendelea miezi sita au mwaka mzima, Magereza za Dar es Salaam zimejaa mahabusu zaidi ya 5,000 ambao kesi zao zinaendelea hawapewi haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wamekaa ndani miaka mitatu, wengine wamekaa miaka minne, kesi zao wengine hawazijui. Sasa tunalundika Magereza zetu kwa watu ambao kwa kweli walistahili kuwa nje kwa misingi ya dhamana. Utamaduni huu unaharibu investment climate ya nchi kwa sababu watu wanaokamatwa wanatoka kwenye Makampuni na Mashirika makubwa ambayo yanatoa mapato makubwa kwa Serikali yetu. Lazima Serikali iangalie namna ya ku-leverage haya mambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema kweli tukasimamia sheria na kukawa na haki katika Taifa, lakini upande wa pili tujue athari zake kwa uchumi wa nchi. Sasa tunakamata watu na watu wengine mnaowakamata, wanaoshtakiwa kwa makosa mbalimbali ya rushwa ni watu ambao wako katika miradi ambayo iko chini ya PPP. Leo Mkurugenzi na mke wake na viongozi wengine wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam wako mahabusu kwa kesi za money laundering na huyu mtu ni mbia wenu, mngeweza mkakaa nao kwenye Vikao vya Bodi mkamaliza mambo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiendelea na utamaduni huu, ni nani atakuwa na confidence ya kuwekeza na Serikali wakati Serikali yenyewe inawaweka ndani wabia wake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema nilizungumze hilo. Waheshimiwa Wabunge, tunatunga sheria nyingine ambazo zinawaumiza sana watu. Kuna watu kule wamekutwa na msokoto mmoja wa bangi, siungi mkono hoja ya bangi, lakini wanafungwa miaka 30. Kuna watu wamekutwa na mirungi kifurushi kimoja wanafungwa miaka 30. Ukienda Kenya, mirungi ni biashara halali. Hebu tujiangalie katika sehemu ya dunia, tuko wapi katika kusimamia mambo haya ili kuhakikisha kwamba tunapotunga sheria, tusitunge kwa ushabiki, tutambue kwamba zinawaumiza sana watu na Bunge linalaaniwa sana katika Magereza zetu zote kwa sababu halisimamii utoaji wa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo, nizungumze suala la utawala la bora, yote haya nayazungumza katika mwamvuli wa utawala bora. Mheshimiwa Mkuchika wewe ni Waziri mzoefu sana, mnajua kwamba Vyama vya Siasa vimeruhusiwa kufanya kazi katika nchi hii katika misingi ambayo ni ya kweli kabisa. Jambo hili limezungumzwa na wengi, mimi kama Kiongozi wa Upinzani nilizungumze kulisisitiza. Ukiulizwa Serikalini, hivi mmezuia kazi za Vyama vya Siasa, kwa sheria gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi mnaona sifa kutangaza kwamba tuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwishoni mwa mwaka huu; mnaona sifa kusema tutashinda uchaguzi wa mwaka ujao, wakati mnazuia Vyama vya Siasa visifanye kazi zake za Kikatiba. Hivi vyama ambavyo havina Wabunge, havina Madiwani, vitajitanua vipi? Vitaeleza vipi sera yake viweze kushiriki uchaguzi wa mwaka ujao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maisha ya siasa ni maisha yetu ya kila siku. Mnazuia Mikutano halafu mnakuwa proud kwamba tunawashinda Wapinzani. Mnaogopa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hofu hii, unaiona hofu katika Taifa, watu wanaogopa. Leo nimekutana na msafara wa Mheshimiwa Rais, nimeogopa, nini kinaendelea nchi hii? Ni lazima Rais wetu alindwe, nakubali; na sipuuzi kabisa umuhimu wa ulinzi wa msafara wa Rais, lakini ukiangalia uzito wa ulinzi wa ule unaona kwamba hata hawa wanaomchunga Rais wanagundua kwamba kuna tatizo mahali. Kwa hiyo, ulinzi unawekwa wa ziada sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, msururu wa magari karibu 80, helikopta ziko angani. Sasa unajiuliza, ile nchi yetu ya amani na utulivu tumegeuka tena! Kile kisiwa chetu cha amani na utulivu kinakuwaje sasa? Tulizoea kuona viongozi wetu wakiwa huru, wakiwa wana-mix na watu wetu bila hofu yoyote, lakini kwa namna mambo yanavyokwenda sasa, tunaona kuna tatizo kubwa la msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaitaka Serikali na Mheshimiwa Waziri atupe kauli, ruhusuni tukafanye kazi ya siasa. Msiwe marefarii na wakati huo huo mkawa wachezaji. Mnatufunga mikono halafu mnaringa hapa! Ruhusuni tufanye mikutano ya siasa, tukutane kwenye majukwaa ya wananchi tukaone haki iko wapi? Hilo ni jambo moja ambalo ningependa sana kulizungumza kwa sababu naona tuna- restrict sana democracy. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo nizungumzie Tume Huru ya Uchaguzi. Hoja ya Tume Huru ya Uchaguzi imezungumzwa kwenye Bunge hili tangu mfumo wa Vyama Vingi umerudi kwa mara ya pili mwaka 1992, hakuna mwaka unapita Tume Huru haizungumzwi. Mnaogopa Tume Huru ya kazi gani? Tume Huru ndiyo inatupa misingi ya utawala bora, tunapata viongozi ambao wametokana na utashi wa wananchi, kila kiongozi anayeingia ndani ya Bunge hili ajione yuko proud, akiwa wa CCM au wa Upinzani ajione yuko proud kwamba amechaguliwa katika uchaguzi ambao ulikuwa huru na haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi mnakwenda kwenye uchaguzi na Tume yenu, Mheshimiwa Rais ambaye naye mdau; kuna conflict of interest hapa, anamchagua Mwenyekiti wa Tume, anachagua Makamishna, anawachagua Watendaji wake, anachagua Wakurugenzi ambao wanatokana na Chama cha Siasa, kitu ambacho Sheria ya Utumishi wa Umma inakataza. Hatuheshimu tena sheria wala katiba yetu, tunalipeleka Taifa hili wapi? (Makofi)

Mheshimwia Mwenyekiti, sisi tunapendekeza very strongly kwamba ni wakati muafaka sasa, kama tunataka amani sustainable katika Taifa hili, tutafakari suala la kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi. Tusisubiri tuingie kwenye machafuko kama Mataifa mengine, halafu tukajiona kwamba tumeingia kwenye machafuko kwa sababu hatukujua tunafanya nini? Ningependa... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)