Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. John John Mnyika

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Leo asubuhi tulipoingia hapa, tulianza na dua, kwa hiyo tulianza na Mungu kwanza, sio kilimo kwanza au elimu kwanza, tulianza na Mungu kwanza na tulisali; “Ewe Mwenyezi Mungu Mtukufu, muumba mbingu na Dunia, umeweka katika Dunia Serikali za wanadamu na Mabunge ya Mataifa ili haki yako itendeke. Twakuomba ibariki nchi yetu idumishe uhuru, umoja, haki na amani. Umjaalie Rais wetu hekima, afya njema na maisha marefu ili pamoja na wanaomshauri wadumishe utawala bora.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaomba mchango wangu wa leo kwa kweli uongozwe na hii sala ambayo tumeisali leo. Kwa sababu tunachangia Ofisi ya Rais nitaomba bila kuvunja kanuni ya kujadili mwenendo wa Rais, nitaomba niguse maswali mbalimbali kuhusiana na Ofisi ya Rais, lakini ambalo naliomba sana Ofisi ya Rais, Utawala Bora na TAMISEMI, walitoleee kauli, hivi ilikuwa ni halali kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora kusema kwamba anakwenda kufanya nini Mheshimiwa Selasini?

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Kumwomba Mungu amshukuru Rais.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani anamwomba Mungu amshukuru Rais, hii ni kufuru!

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mnyika, ongea na kiti.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongee na kiti kwamba Ofisi ya Rais, Utawala Bora na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ituambie hivi ni halali kwa Wakuu wa Mikoa na viongozi wa Kiserikali kukufuru na kufanya dhihaka dhidi ya Mwenyezi Mungu? Wengine utasikia wanajiita Mungu wa Dar es Salaam na mambo mbalimbali. Serikali itoe kauli juu ya jambo hii ndani ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imeelezwa hapa kwamba Mheshimiwa Rais atakuja kesho kuzindua Makao Makuu, ujenzi wa Mji wa Serikali. Ningeomba sana sana Ofisi ya Rais imshauri Rais kama ambavyo anapata wasaa wa kuzunguka kuzindua majengo pengine kupatikane wasaa wa siku moja wa Taifa letu na siku ya sala A National day of prayer tuiombee nchi yetu. Pengine tutaponya majeraha ya Kibiti, majeraha ya watu kupigwa risasi kama Mheshimiwa Tundu Lissu, majeraha ya miili kuokotwa Coco beach na mambo mengine ambayo kwa kweli, Mheshimiwa Selasini anasema kipindi cha Kwaresma yatatusaidia kutuweka pamoja kama Taifa, kwani Taifa linalokwenda pamoja ni Taifa linaloweza kwenda kwa kasi zaidi kuliko kasi tuliyonayo ya maendeleo ya nchi yetu kwa sababu kasi yetu tunapewa takwimu za uongo Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa kwamba uchumi wa nchi utakua kwa asilimia saba huku Shirika la Fedha Duniani linatoa taarifa kwamba hiyo asilimia inayosemwa na Serikali haiwezekani sanasana tukijitahidi ni asilimia nne. Taifa la namna hii linahitaji uponyaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kulizungumza, tumeapa kulinda Katiba, naelewa wenzetu tukisema kuhusu Katiba wanasema kipaumbele cha msingi cha wananchi ni maji, umeme na miradi mingine ya maendeleo, lakini tulipoapa na Mheshimiwa Rais aliapa cha kwanza tuliapa juu ya katiba kwa sababu Katiba ndiyo nyenzo ya kusimamia mambo yote na ndiyo nyenzo ya kuleta maendeleo ya nchi. Kwa hiyo, nasema Katiba ni jambo la pili muhimu sana kwa nchi yetu na kwa sababu Katiba ni jambo la pili ningependa kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Rais alipokuja kuhutubia Bunge wakati anazindua Bunge aliahidi hapa Bungeni kwenye hotuba yake kwamba ataendeleza na kukamilisha mchakato wa Katiba mpya. (Makofi)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Hebu subiri tu Mheshimiwa Mnyika, taarifa.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimkumbushe mzungumzaji anayeongea kwamba siku Rais amekuja hapa kutoa maelekezo yake ya nchi yeye hakuwepo Bungeni, alijuaje hayo maneno? (Makofi)

MWENYEKITI: Endelea Mheshimiwa.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Mbunge wa wapi ambaye hajui kwamba kila kinachojadiliwa Bungeni kinawekwa kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge? Kwa hiyo analiaibisha Bunge tu. Naomba niendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Rais akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenye kongamano, kinyume na kauli yake ya Bungeni, Rais amesema eti hataki mchakato wa Katiba mpya kuendelea kwa sababu kuna watu wanataka wapewe posho ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema Ofisi ya Rais ikamkumbusha Rais. Wao walikaa kwenye Bunge Maalum wakapitisha Katiba inayopendekezwa kinyume na Katiba na wananchi kwa Sheria ya Kura ya Maoni na Sheria ya Mabadliko ya Katiba, hatua inayofuata ni kura ya maoni dhidi ya hizi rasimu mbili uamuzi wa wananchi kufanyika, jambo hilo halihusu Wabunge kukaa kikao, jambo hilo halijusu Wabunge kupewa posho.

Kwa hiyo kauli ya Rais ilikuwa inataka kupotosha tu mjadala wa Katiba mpya ni muhimu katika majumuisho. Ofisi ya Rais ikasema ni kwanini katika Bunge hili hakijatengwa pesa kwa ajili ya kura ya maoni na kukamilisha mchakato wa Katiba mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusikubaliane kwa namna yoyote na kauli ya kwamba eti hakikuwa kipaumbele chenu wala kipaumbele cha Rais. Nimeisoma Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Ilani ya Uchaguzi ya CCM imesema bayana, CCM itaendeleza na kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya, tekelezeni Ilani yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitarudi kwenye haya mambo…

T A A R I F A

MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimtaarifu mzungumzaji anayezungumza kwamba Katiba inayopendekezwa tulishiriki wote Wabunge tuliokuwepo Bunge lililopita na mchakato ule ulipofikia hatua, wenzetu wa upinzani hatukuwa nao mpaka hatua ya mwisho waliikataa. Leo hii wanakuja hapa kusema wanataka mchakato uendelee wa kupigia kura, Katiba ipi mpya inayopendekezwa wakati wao waliikataa na hawakushiriki zoezi mpaka mwisho? (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Mnyika taarifa.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Kura ya Maoni inasema Katiba inapendekezwa ikishapitishwa kwenye Bunge Maalum hatua inayofuata ni kura ya maoni bila kujali nani alikuwepo na nani hakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuendelea. Nitaomba kupata ufafanuzi kutoka kwa Ofisi ya Rais, ripoti iliyopita ya CAG sio ya sasa, ripoti ya mwaka uliopita iliibua madudu mengi kwenye sekta mbalimbali na Wizara mbalimbali na kati ya mambo yaliyoibuliwa ni pamoja na suala la 1.5 trillion ambayo baadaye ilipanda mpaka kuwa 2.4 trillion. Katika ufafanuzi wa Serikali juu ya 1.5 trillion kuna taarifa zilitolewa toka 1.5 mpaka 2.4 kwamba bilioni 976.96 zilihamishwa kwenye Mafungu mbalimbali zikapelekwa kwa maana ya kibajeti reallocation zikapelekwa kwenye Fungu la 20 la bajeti ambalo ni sehemu ya hotuba yetu ya leo Ofisi ya Rais, Ikulu. Sasa mimi kama Mbunge naamini moja, Bunge halikupitisha uamuzi wa kufanya reallocation ya bilioni 976.96 kupeleka Fungu namba 20 Ikulu. Pili… [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mnyika, hebu nisaidie Sheria ya Bajeti kuhusiana na reallocation inasemaje? Nisaidie?

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya interests…

MWENYEKITI: Ni Bunge linafanya au mamlaka husika inafanya?

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa interest ya time nijikite zaidi kwenye hoja yangu.

MWENYEKITI: Hapana.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitaka kujadili hilo tuta…

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, utalinda muda wangu?

MWENYEKITI: Naulinda! Mheshimiwa Mnyika na Waheshimiwa Wabunge, tusifanye generalization ambazo huwezi kuzi-defend hapa. Sisi wote hapa tumeshiriki, baadhi yetu tumeshiriki katika utungaji wa sheria hiyo.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Shut up!

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Nawaombeni Waheshimiwa Wabunge, kiwango ambacho kimetajwa na Sheria ya Bajeti kama kuna Mbunge anataka ku-challenge hiyo, warrant ya reallocation inapowekwa na Serikali hapa wewe unapaswa sasa useme kwamba reallocation hiyo imezidi kiwango ambacho kimewekwa na Bunge, ukomo, lakini hatuwezi hapa kuja tunafanya generalization tu ili -m-get away na hiyo, hapana si kweli! Waziri wa Fedha, jamani Wizara hiyo ni makini sana. Endelea. (Makofi)

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuondoe utata kuhusu jambo hili la bilioni 976.96 kwa kuwa CAG anabanwa banwa kidogo kukagua Ikulu, Ofisi ya Rais ikija kwenye majumuisho hapa itueleze hizi bilioni 976.96 Ikulu zilitumika kwa matumizi gani? Tupewe mchanganuo wa kina…[Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kusubiri kuja kujibu kuwaachia Watanzania wanapotoshwa. Lazima watu wanaosema uongo ndani ya Bunge lako Tukufu wathibitishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiomba kiti chako kimwelekeze Mheshimiwa Mnyika aweze kuthibitisha kwamba CAG anabanwa banwa kukagua Fungu 20 la Ofisi ya Rais, kwa sababu kinachofahamika kila Fungu lina Resident Auditor kutoka Ofisi ya CAG including Fungu 20. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hiki kinachoelezwa kisiwapotoshe Watanzania kule nje. Naomba iwekwe wazi kwamba hakuna Fungu hata moja ambalo CAG anazuiwa kulikagua na Fungu hili lilikaguliwa na CAG hakuja na hoja hizi zinazoletwa kuwadanganya Watanzania humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kiti chako kitende haki kwenye jambo hili ili Watanzania wasiendelee kudanganywa na Mheshimiwa Rais wetu asiendelee kuchafuliwa bila sababu za msingi. (Makofi)

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini ulilinda muda wangu, lakini mimi bado naomba katika majumuisho Ofisi ya Rais ilete mchanganuo hizi pesa zimetumika kwenye kitu gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea. Hotuba hii ya…

MWENYEKITI: Una dakika mbili.

MHE. JOHN J. MNYIKA… Utumishi wa Umma inahusu maslahi ya wafanyakazi wa umma…

KUHUSU UTARATIBU

MWENYEKITI: Kanuni namba ngapi?

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 64(a).

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni iliyovunjwa ni ya 64(a). Kanuni inasema hivi; Mbunge hatatoa ndani ya Bunge Taarifa ambazo hazina ukweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la 1.5 trillion limeendelea kuongelewa humu ndani ya Bunge tena limeongelewa kwa uongo. Kwa sababu nitahitajika kuthibitisha kuwa huo ni uongo, Ripoti ya PAC Mwenyekiti wake ambaye ni Mpinzani, Mheshimiwa mama Kaboyoka, Mbunge wa CHADEMA inasema hivi ukurasa wa 35; “Mheshimiwa Spika katika kuhitimisha suala la tofauti la 1.5 trillion kati ya mapato ya Serikali na makusanyo kwa mwaka 2016/2017, naomba kuweka kumbukumbu sahihi katika Bunge lako Tukufu kuwa tofauti hiyo haikuwepo baada ya marekebisho ya mahesabu kufanyika.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Bunge lako limeendelea kutumika kama jukwaa la kuichafua Serikali kuwa imefanya matumizi ya 1.5 trillion na Bunge lako limekaa kimya bila kuwakemea hawa. Watanzania wameendelea kupotoshwa na Bunge lako limekubali. Naomba likemewe suala hili na utoe maelekezo. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mlinga, umesimama kuhusu utaratibu, umetaja hiyo Kanuni ya 64(1)(a)…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, please. How can you get to (a) without reading 64? (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, naendelea, hatatoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina ukweli. Sasa Kanuni hii lazima uisome pamoja na Kanuni ya 63, Mbunge aliyekuwa anaongea hapa alikuwa ni Mheshimiwa Mnyika, kwa hiyo, ni Kanuni ya 63(2), inasema, Mbunge yeyote anapokuwa akisema Bungeni, hutachukuliwa unasema uongo kama unafanya reference. Fasisli ya (3) inasema, Mbunge mwingine yeyote anaweza kusimama mahali pake na kutamka “kuhusu utaratibu’, tumemsikiliza Mheshimiwa Mbunge kafanya hivyo na Mheshimiwa Mnyika kwa mujibu wa fasili ya (4), aliketi, lakini sasa huyu aliyesema wewe husemi ukweli anapaswa aseme kitu, atoe maelezo kwa kiwango ambacho kinaliridhisha Bunge kwamba kuna uongo umesemwa. Ameenda mbali zaidi amesema Taarifa ya Kamati ya PAC kuhusiana na amount hiyo, kwamba Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ilisema suala hilo si hoja tena, kwa hiyo, hiyo ni rekodi ya Bunge. (Makofi)

Kwa maana hiyo Mheshimiwa, kwa mujibu wa Kanuni zetu, kwa sababu ya maamuzi ya Kamati ya Bunge ya PAC, kwa hayo iliyoyasema, wewe sasa ndiyo unatakiwa uthibitishe kweli au si kweli. Kwa maana hiyo, nakupa options mbili tu, ya kwanza, ufute tu kauli yako kuhusiana na hayo maelezo yako, yale uliyosema ya bilioni ambazo zilikuwa summarized zote, wewe umesema bilioni 900 lakini ukasema ni trilioni 2.4 kwa maana kwamba 1.5 trillion kujumlisha na hizo bilioni ndiyo unapata hiyo. Sasa maelezo ya 1.5 trillion yapo kwenye ripoti ya PAC. Maana wewe umefanya majumuisho, sasa nakupeleka ufute kauli yako au nikupe muda wa kuja kuthibitisha Bungeni hapa, chagua mojawapo.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshmiwa Mwenyekiti, kwanza niweke rekodi sawa, nimesema…

MWENYEKITI: Tunabishana tena?

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshmiwa Mwenyekiti, naomba niseme, naomba niweke rekodi sawa. Nimesema, nataka maelezo ya Serikali Bungeni juu ya shilingi bilioni 976.96 zimetumika kwa matumizi gani? Nimesema jambo hili liko outstanding na hili ndilo linasababisha mjadala wa 1.5 trillion na 2.4 trillion kuendelea. Kwa hiyo, kama ni uthibitisho, nitakiwe kutoa uthibitisho kuhusu suala la shilingi bilioni 976.96 za Vote 20 ya Ikulu. Nipewe nafasi ya kuzungumza kuhusu hilo. (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge, huna hoja yoyote, unatupotezea muda wetu wa Bunge. Kwa sababu kama issue yako ilikuwa ni 1.5 trillion kama ulivyoanza, usingekimbilia kutafuta 900 billion shillings. Ulifanya majumuisho ya 2.4 trillion na ndiyo maana Mheshimiwa Naibu Waziri akasimama. (Makofi)

Kwa hiyo, kama unataka tupitie Hansard ili tuone mtiririko wa argument yako. Mimi naagiza watu wa Hansard kabla ya sasa saba tupate Hansard hiyo halafu nitatoa uamuzi wangu kuhusiana na hoja ya Mheshimiwa Mnyika. Ahsante. (Makofi)

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshmiwa Mwenyekiti, naomba…

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha, si nilikwambia dakika mbili.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshmiwa Mwenyekiti, muda wangu umekwisha wakati nimekuwa interrupted!

MWENYEKITI: Umekwisha!

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshmiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie muda wangu, nilikuwa nazungumza nikawa interrupted.

MWENYEKITI: Sasa kama hutumii vizuri muda wako, umekwisha. Nimekulindia muda nikakwambia zilikuwa zimebaki dakika mbili, umeongezewa nyingine mbili.