Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mungu kwa kunijalia kusimama hapa nami niweze kutoa mchango wangu. Kwa kuanza, kwa masikitiko makubwa sana nami naungana na Wabunge wenzangu wote kwa lile suala wanalolilia la vyanzo vya mapato vya Halmashauri vyote kuchukuliwa na Serikali Kuu, jambo ambalo litapeleka Halmashauri zetu kuendelea kudorora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa umekuja mpango huu wa vitambulisho vya wajasiriamali, ile ni sehemu moja muhimu ambapo Halmashauri zilikuwa zinajikusanyia mapato yake. Yalianza mabango, yakaja majengo na sasa wamemalizia kwenye wafanyabiashara au wajasiriamali wadogo wadogo. Nami naungana na wenzangu kulitaka jambo hili liangaliwe upya kwa sababu Halmashauri zina majukumu makubwa na lazima zijiendeshe kwa kuwa na vyanzo hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, mimi leo nashukuru sana, kwanza nilisahau hapo mwanzo nilitaka kusema kwamba nilishukuru Bunge letu kwa kukubali kuipokea ile ripoti ya CAG. Nashukuru sana kwa sababu jambo hili tayari lilikuwa limeleta mjadala mkubwa huko lakini kwa umahiri imepokelewa na nashukuru ina sign ya mwenyewe Profesa Assad, kwa hiyo, ni jambo la kufurahisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yaliyopita, iko methali ya Kiswahili inasema: “Funika kombe mwanaharamu apite. Hata hivyo, katika hili la CAG tutafunika kombe lakini mwanaharamu hapiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie utawala bora. Hii dhana ya utawala bora ni pana sana na Mzee wangu Mheshimiwa Mkuchika amepewa Wizara hii kwa umahiri wake, nampongeza sana. Hata hivyo, mambo yanayotendeka ndani ya hchi hii yanakwenda kinyume kabisa na utawala bora. Nataka niseme wazi, Mheshimiwa Waziri umepewa jukumu la kuhakikisha utawala bora unaendelea ndani ya nchi lakini kuna mambo yanayofanyika hayaendani kabisa na dhana ya utawala bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa ni moja kati ya jambo ambalo mnakiuka masharti ya utawala bora. Tanzania imesaini mikataba mbalimbali ya dunia kusimamia haki za raia wake lakini leo sheria, Katiba na vitu vyote vinasema wazi haki ya vyama vya siasa ya kufanya mikutano ya hadhara lakini mmezuia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnajua kuna vyama zaidi ya 20 ndani ya nchi hii na mnajua kuna Wenyeviti wa vyama vingine hawana Mbunge hata mmoja, vyama hivyo vitawezaje kujitangaza kwa wananchi kama mmewazuia wasifanye mikutano ya hadhara? Lengo lenu ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Jeshi la Polisi limejipa mamlaka hata vikao vya ndani ya vyama vya siasa wanazuia, kitu ambacho hakihitaji kibali wala ruhusa ya mtu yeyote vyama vya siasa kufanya vikao vya ndani. Hebu hili liangalieni kwa umakini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili linaumiza watu, tunakwenda kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa hivi karibuni tu leo vyama ambavyo vinatikiwa kushiriki katika chaguzi hizo haviruhusiwi kufanya siasa ndani ya nchi hii lakini mshindani wetu mkuu Chama cha Mapinduzi mnapiga jaramba mtakavyo. Ndugu Humphrey Polepole anafanya mikutano anavyojisikia yeye lakini Makatibu Wenezi na Makatibu Wakuu wa vyama vingine hilo ni haramu, mnatenda dhambi Mungu anawaona, si haki. Zuio hili linahusu opposition lakini ninyi kwenu hakuna marufuku yoyote (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe tahadhari yangu, tunapokwenda mbele, ziko lugha zinasemwa na wenzangu wametangulia kusema kwamba kwenye Uchaguzi Mkuu Wapinzani hawatarudi. Sawa, hakuna tatizo. Tusiporudi kwa maamuzi ya wananchi, hiyo hakuna kesi; lakini msitarajie ule upuuzi uliofanyika Korogwe na uliofanyika Majimbo mengine; Msimamizi wa Uchaguzi anachukua fomu anakwenda kujificha halafu anatangaza kwamba Mgombea wa Upinzani katika eneo hili hakurudisha fomu. Huo ni upuuzi, hatutakubali, lazima tutahadharishane mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako huku Waheshimiwa Wabunge wameingia kwa njia hizo, wamejificha na ushahidi uko, kwamba Wagombea wa Upinzani wanarejesha fomu, Wakurugenzi wa Halmashauri wanajificha kukataa kupokea fomu za Wapinzani. Haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wanaotegemea kurudi kwa njia ya mkato ya aina hiyo, wale wanaotegemea mteremko wa aina ile, mwaka 2020 tutapeana tahadhari kabisa. Tanzania ni yetu sote, Vyama vya Siasa vipo kwa mujibu wa sheria na tutasimamia sheria mpaka tone la mwisho la damu yetu. Hatutakubali Mkurugenzi yeyote au msimamizi wa uchaguzi apokee amri haramu kusimamia uharamu wa kuwabatilisha Wagombea wa Upinzani. Hilo never, never never. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea tena kwenye Utawala Bora. Kwenye Magereza wamejaa watu wengi sana. Wamejaa watu ambao hawastahili kuwepo kwenye Magereza kwa sasa. Kuna watu kesi zao zimechukua zaidi ya miaka sita. Kosa moja tu, upelelezi haujakamilika. Jamani, wale walioko kule ndani ni wazee wetu, ni ndugu zetu, ni watoto zetu. Hatupiganii makosa yao wasamehewe, tunataka kesi zao siendeshwe, ushahidi utolewe, wahukumiwe kwa mujibu wa sheria. Siyo uhodari wa kuwachukua watu mkawalundika ndani halafu mkasema upelelezi haukamiliki. Lini upelelezi utakamilika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema especially kesi ya Mashehe wa Uhamsho wa Zanzibar, hili suala linatukera sana. Wazanzibar wanakereka na hakuna Mtanzania yeyote aliye radhi kuona kesi ile inaendelea kukaa ukiambiwa tu kwa sababu ushahidi haujakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama yuko aliye radhi, mfano kwenye Bunge hili, aseme mimi niko radhi watu wale waendelee kukaa kwa kisingizio tu ushahidi haujakamilika. Leo ni miaka sita wazee wa watu wanasota ndani ya Magereza. Aliye radhi asimamie Mbunge mmoja aseme mimi niko radhi dhuluma ile iendelee. Asimame humu ndani ya Bunge!

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ina sheria. Kama kesi zinaonekana hazina ushahidi, ziko sheria za kuyaahirisha mashauri ili ushahidi mwaka wowote ukipatikana mashauri yale yarudi tena Mahakamani. Kwa nini hazitumiki hizo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wananyimwa fursa. Wako wale walioshitakiwa kwa kesi za ubakaji, wakahukumiwa jela wakafungwa. Wamefaidika na fursa ya Mheshimiwa Rais ya kutoa msamaha kwa wafungwa. Leo wazee wale yalaiti wangekuwa wamehukumiwa kwa makosa yao, nina hakika Mheshimiwa Rais hawezi kusamehe wabakaji akaacha kuwasamehe Mashehe Wana wa Zuoni. Nina hakika wangehurumiwa na leo wangekuwa huru wakaendelea kulea familia zao. (Makofi)

Mheshimiwa Menyekiti, tuna hasira sana na tunajisikia uchungu sana kwa Mashehe wa Uhamsho na Watanzania wengine wowote wanaoendelea kulundikwa Magerezani kwa kisingizio tu cha ushahidi haujakamilika. Ushahidi utapatikana lini? Mheshimiwa Waziri wa Utawala Bora, nakuomba sana, wewe ni mzazi, wewe ni mzee, yafikirieni tena haya, Serikali liangalieni, viambieni vyombo vyenu vya upelelezi; suala la Mashehe wa Uamsho wa Zanzibar lifikie mwisho. (Makofi)

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Taarifa.

Hiki kidonda kinachotutonesha, naomba sana suala hili lifikie mwisho.

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)