Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Raphael Michael Japhary

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kwa kupata nafasi hii ya kuchangia. Naomba nichangie hotuba zetu mbili za Kambi ya Rasmi za Upinzani naeneo kubwa ambalo nataka nichangie la kwanza, ni kuhusu kanuni ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Katika hotuba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, ukurasa 17, kifungu cha 18, imeonesha kwamba kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zimeshakamilika lakini jambo la kushangaza ni kwamba tarehe 1, 2 na 3 Aprili, wadau wa vyama vya siasa na NGO’s na Asasi Zisizo za Kiserikali waliitwa kwa ajili ya kutoa maoni yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 4 Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuwa anahutubia Bunge hili alisema kwamba tayari kanuni zimekamika wakati wadau waliitwa kwa ajili ya kutengeneza rasimu. Sasa tunachojiuliza hapa nikwamba wadau waliitwa kufanya nini, kwa sababu haiwezekani tarehe 1-3wadau waitwe halafu tarehe 4 Aprili, kanuni zionekane kuwa zimeshakuwa tayari wakati waliitwa kwa ajili ya kuandaa rasimu. Sasa rai yetu, tunaomba Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha hotuba yake atusaidie kupata nakala zile za kanuni ya uchaguzi ili tuone kama mawazo na maoni ya wadau yamechukuliwa kwa kiwango gani ili kufanya uchaguzi huu uwe ni uchaguzi ambao ni huru, utakaofanya kila mtu aliyeshiriki aone ametendewa haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ninalotaka kuzungumza kuhusu kujenga taasisi kuliko kujenga mtu katika nchi yetu. Tulidhani kwamba ni vizuri katika nchi yetu tuhakikishe kwamba taasisi zetu zinakuwa imara kwa sababu watu wanapita, lakini taasisi zitaendelea kubaki. Lazima tuwe na taasisi ambazo zinahakikisha kwamba watendaji wanaoteuliwa katika nchi hii wanateuliwa kwa sababu ya uwezo wao na sio kwa sababu ya uswahiba wao na viongozi wa juu. Hawateuliwi kwa sababu wana mahusiano yoyote na viongozi wa juu bali kwa sababu wana maadili ya kuweza kuwasaidia Watanzania, taasisi zetu lazima zioneshe hivyo. Pia taasisi zetu lazima zioneshe kwamba kiongozi wa nchi hii ni mlinzi wa fedha za wananchi na sio mwenye fedha za wananchi. Kwa sababu hali ilivyo sasa walipakodi ni wananchi, lakini fedha inaonekana inayokusanywa katika nchi ni fedha ya kiongozi wa nchi. Kwa misingi hiyo ana uwezo wakuamua anavyotaka kuipeleka, ana uwezo wa kutembea nayohata kwenye maboksi akagawa barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunadhani ni vizuri tujenge mfumo ambao utafanya kiongozi wa nchi afahamu fedha aliyonayo ni fedha ya wananchi kwa hiyo kila mwananchi katika nchi hii ana haki ya kupata maendeleo kwa kadri ya mchango wake.

T A A R I F A

MWENYEKITI: Taarifa.

MHE. MAULID S. A. MTULIA:Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na heshima yangu kubwa kwa kaka yangu Mheshimiwa Mbunge, nataka nimpe taarifa kwamba kiongozi wa nchi yetu anatambua fedha zote ni fedha za wananchi na ndio maana bajeti ya nchi inaletwa hapa kila mwaka na ndio maana tupo hapa ndani ya miezi mitatu kujadili bajeti ya nchi. Kwa hiyo,asipotoshe umma kwamba kiongozi anasema pesani za kwake, pesa za wananchi, ndio maana Wabunge tupo hapa. Taarifa hiyo nampa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Japhary.

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema ni kwamba nasema tutengeneze mfumo katika Taifa letu utakaowafanya viongozi wote watambue kwamba fedha za nchi sio za kwao ila ni za walipakodi. Kwa hiyo wana haki ya kuwapelekea wananchi maendeleo kwa kadri wanavyostahili na sio kwa kadri ya utashi wake na sijazungumzia kiongozi wa nchi aliyepo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri mifumo hii ikawepo ili iheshimu demokrasia. Ndani ya nchi yetu hii leo demokrasia haipo, na kila wakati ukisema demokrasia haipolinaonekana hili ni suala la upande mmoja,lakini leo Mungu angeweza akageuza kibao, upande huo ukawa upande huu, halafu kwa mifumo hii hii tuliyonayo, Tume za Uchaguzi tulizonazo na mazingira haya tulionayo, upande huo ungelalamika kuliko upande huu.

T A A R I F A

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Nimpe Taarifa muongeaji pamoja na kwamba wenzetu wakiambiwa kwamba ipo siku moja inaweza kugeuka wanakataa, lakini katika Qurani Tukufu ipo aya inayosema hivi;Innama amruhu idha arada shay-an an yakuula lahu kun fayakuun (hakika Mwenyezi Mungu jambo analolitaka huliamrisha na kuwa).Sasa msijidanganye kwamba haiwezekani ipo siku, ipo siku.

MWENYEKITI:Mheshimiwa Japhary, huyo anachanganya.

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni muumini mkubwa sana wa Mungu na kwa bahati mbaya wana siasa wanajitoa kwenye uelewa wa kumwamini Mungu, kwa taarifa iliyotolewa na Mheshimiwa Mbunge naipokea kwa mikono miwili, kwamba kilichowaweka huko mkatawala ndicho kitakachoweza kuwaweka watu hawa huko wakatawala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi ambao tunatakiwa tuujenge kwenye Taifa hili ni wote tutambue kwamba tunapaswa kuliona Taifa hili kama letu wote pamoja. Akitawala huyu aheshimu wengine anaowatawala. Sasa bahati mbaya katika Taifa hili imeonekana kwamba kuna upande ambao hili Taifa ni la kwao wengine sio Watanzania yaani tunaonekana tupo Tanzania kwa bahati mbaya tu lakini si kwamba nasi tuna haki ya kuwa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninachosema kwamba ni vizuri tutengeneze mfumo ambao utaheshimu haya, demokrasia iwe part ya maisha yetu. Haiwezekani leo Mheshimiwa katika Taifa hili CCM wanafanya mikutano ya hadhara ya ndani, wanafanya maandamo, wanalindwa lakini kila siku Wapinzani wanaandamwa ndani ya Taifa moja na Wapinzani hawajavunja sheria kwa sababu hawajawaWapinzani kwa sababu wametaka kuwa hivyo bali katiba imewaruhusu kuwa hivyo. Vyama vingi vya siasa vimeruhusiwa na Katiba ya nchi yetu. Hivyo,ni wajibu wetu sote sisi tuheshimiane kwa sababuKatiba inaruhusu kuwe kwetu sisi na kuwepo kwenu nyie.

Mheshimiwa Mwenyekiti,Katiba inakuwepo ili sisi tuwakosoe nyie na sio tuwasifu nyie, hatupo hapa kwa ajili ya kuwasifu, ingekuwa kuwasifu tungekuwa upande wenu. Tupo upande huu ili tuwakosoe ili siye tuwe kioo kwenu ili mfanye vizuri, mnatulazimisha tukae Bungeni kuwasifu inaonekana as if kuwakosoa ni kumchukia Rais, si kweli. Hatumchukii Rais bali tunatimiza wajibu wetu wa kuwakosoa, tunam-shape Rais aweze kuongoza vizuri, ndio maana ya kuwa huku. Sasa ninyi mnadhani kumkosoa Rais ni kumkosea adabu Rais, si kweli na ubaya zaidi mnamfanya Rais ahisi kwamba sisi tuna ugomvi na yeye, tuna chuki na yeye, baadala ya kumsaidia kwamba hawa ni wenzako wanaku- shape ukae vizuri. Kwa hiyo nadhani mfumo mzuri wa utawala ndani ya nchi hii utatufanya tukae vizuri. Kwa hiyo,hiyo ndio rai yangu kwaWaheshimiwa viongozi.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la tatu, nataka nizungumze suala la TARURA, Bunge lako Tukufu liliridhia kuanzishwa kwaTARURAkatika nchi hii, lakini TARURA malengo yake ya msingi kama yalivyofikiriwa hayawezi kuwa msaada sasa kama TARURA haitaangaliwa vinginevyo. Sasa hivi Wakala wa Ujenzi wa Barabara Vijiji na Mjini hajawa msaada sana wa kuhakikisha barabara zetu zinakuwa kama zilivyokuwa zimetegemewa ni vizuri Mheshimiwa Waziri tuone namna gani tunahakikisha kwamba moja tunapeleka bajeti ya kutosha kwenye wakala huyu ili afanye vizuri kwenye barabara zetu,otherwise barabara ni mbaya zaidi kuliko hata wakati zikisimamiwa na Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri wakati Halmashauri zikisimamia barabara zilikuwa zinauwezo wa kutenga fedha kwenye Kamati zao za dharura zikahakikisha barabara zao zinatengezwa. TARURA hawana hiyo fedha mpaka wasubiri fedha kutoka kwenye Mfuko Mkuu, matokeo yake wanashindwa kufanya kazi yao inayotarajiwa. Barabara nyingi zinakuwa mbovuna yakitokea majanga ya mafuriko na mambo mengine inakuwa vigumu sana barabara zetu kutengenezwa kwa hiyo hali inakuwa ni mbaya zaidi. Ni vizuri tuongeze bajeti ya kutosha nani vizuri tutafute vyanzo vingine kwa TARURA ili waweze kuhakikisha kwamba wanasimamia zoezi hili vizuri na malengo ya Wabunge kuomba agency hii iundwe yawe na maana. Kwa hiyo, nashauri sana tuangalie hili katika uzito wake wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti,la pili, katika TARURAni vizuri tuone jinsi gani Madiwani wanashirikishwa, Madiwani wanakuwa kama sio sehemu ya Halmashauri husika wala miji husika, matokeo yake maamuzi ya watendaji wa TARURAyanakuwa ni wao wenyewe. Sasa tuangalie sheria yetu itafanyaje Madiwani washirikishwe ndani ya TARURA hata kama angalau Kamati za Fedha zipewe taarifa ya namna gani TARURAinaendelea na pia TARURA iheshimu vipaumbele vya Halmashauri. Ingesaidia sana suala la kuzisaidia mamlaka hizi kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ni D by D kumekuwa na hoja nyingi sana kwa upande huu zaidi kwamba Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya wamekuwa wakigombana na Halmashauri, lakini kama mfumo huu D by D Policy yake ingezingatiwa vizuri Wakuu wa Mikoa wakaelewa vizuri na ndio maana nikasema ni vizuri hata wanaochaguliwa, wachaguliwe kwa ethics zao, wachaguliwe kwa uwezo wao na sio kwa ukada wao, leo hii migogoro isingekuwa inaendelea katika Halmashauri zetu. Ipo hivi kwa sababu viongozi wetu wengi wa Mikoa na Wilaya wameshindwa kufuata maadili yao, wamekwenda kwa ukada, wamekwenda kwa ajili ya kuwaumiza Wapinzani au kuumiza watu waliopo chini yao. Matokeo yake imekuwa vurugu kila siku mpaka kila siku…

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Japhary.

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL:Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.