Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Juma Selemani Nkamia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kwanza namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuniamsha salama leo, lakini pia nichukue fursa hii kumpongeza Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli, pamoja na wasaidizi wake Mheshimiwa Jafo pamoja na Naibu Mawaziri wote wawili, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nianzie pale alipomalizia pale Mheshimiwa Bura kwenye suala la Madiwani. Madiwani tusiwaone ni wa maana tu pale tunapokwenda kwenye uchaguzi. Nazungumza hili kwa nini? Nataka nitoe na mifano. Madiwani wengi Tanzania, kwenye Halmashauri nyingi hata posho zao za kisheria hawajalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, visingizio vingi vimekuwa ni mifumo ime-bust, lakini kumbe Halmashauri nyingi ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Chemba wameshindwa kupeleka fedha za maendeleo, wamejikuta expenditure imekuwa kubwa na matokeo yake Madiwani toka mwezi wa Kumi mpaka tunavyozungumza, hata posho za vikao vyao vya kawaida wanakopwa. Mheshimiwa Waziri Jafo anajua, Mkuu wa Mkoa anajua na RAS wa Dodoma anajua. Kwa hiyo, nilikuwa nadhani kwamba ipo haja ya kuangalia hili suala kwa kina sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Waziri, nitumie fursa hii kuwapongeza sana. Leo Chemba tuna Vituo vya Afya vitatu; viwili Alhamdulillah vimejengwa vizuri; kimoja ndiyo hivyo, tia maji tia maji, lakini tunashukuru. Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri tulikwenda naye pale Hamai, na akakuta ile hali ya pale na hakuchukua hatua yoyote, japo kauli yake pale alisema hajaridhishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najiuliza, nimekuwa nikiona Waheshimiwa Mawaziri wanatembea sana Tanzania hii kwenda kutatua kero za wananchi, lakini juzi nilipokuwa Kanda ya Kusini kwenye ziara ya Mheshimiwa Rais, nimeona yeye ndiyo anatatua matatizo hata yale ambayo ninyi mngeweza kuyatatua. Sasa mnazunguka kufanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nadhani ni vizuri mkachukua hatua pale mnapoona kuna kasoro. Kwa mfano, pale kwa Mtoro, mtu amepewa tenda ya kutengeneza milango akalipwa shilingi milioni 15 zote hajapeleka hata frame moja. Watu wa Chemba wanajua, Ofisi ya TAMISEMI inajua na Mungu anajua. Chukueni hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tukisema hapa na ninyi pale TAMISEMI kuna majungu yanaletwa sana kule, kwamba ooh, unajua Mbunge wa Chemba, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mwenyekiti wa CCM wanataka posho tu. Posho za nini? Watu wenu pale TAMISEMI wakishasikia hivyo, sisi tunaomba Mheshimiwa Waziri aunde tume ikachunguze matatizo ya Chemba, hatutaki kumwonea mtu. Chemba imekuwa shamba la bibi. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri achukue hatua. Tuliomba aunde tume apeleke pale ikachunguze. Tatizo ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Chemba tunaomba tupatiwe pesa mwaka huu. Pia hata tukipewa hizo pesa, hata zile 1.4 billion mlizotupatia, yule Boya ameshajenga lile jengo anadai fedha zake shilingi milioni 150, Halmashauri haina hizo fedha. Zimeenda wapi? Hata mkitupa leo, mimi sioni faida yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya. Dakika 20 zilizopita alinipigia engineer mmoja ambaye anajenga Hospitali ya Wilaya pale Chemba, wameingia mkataba toka mwezi wa Pili, leo walikuwa wanataka kugoma kuendelea kujenga, hawajalipwa hata senti tano na fedha mmeleta. Sasa tatizo liko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, chukua hatua, hii inakusaidia kukujenga pia kwa siku zijazo. Ya Mungu mengi, huwezi kujua. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba sana kaka yangu, chukua hatua. Leo wanataka kugoma kujenga Hospitali ya Wilaya kwa sababu hawajalipwa, fedha mmeshaleta. Kuna tatizo gani? Mkataba toka mwezi wa Pili. Au mpaka wasikie Mheshimiwa Rais anakuja? Kwa hiyo, naomba mtusaidie juu ya hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye vitambulisho vya Mheshimiwa Rais. Hili ni wazo zuri sana sana sana, lakini huko Wilayani operesheni yake inakwenda tofauti. Baadhi ya watu wanamchukia Mheshimiwa Rais kutokana na baadhi ya Watendaji walioko huko Wilayani kulifanya hili kama vita. Wewe unawezaje kugawa vitambulisho hivi vya wajasiriamali chini ya ulinzi wa Polisi? Nani atakuja kuchukua? Hivi wewe kiongozi unaanza kukurupushana na akina mama unabeba masufuria ya pilau, unawalazimisha wanunue vitambulisho, nani atachukua? Chukua hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma kwa kuzuia Polisi wa Chemba wasiende kugawa vitambulisho vya Rais. Sasa hivi vitambulisho vinauzika sana. Yule Mkuu wangu wa Wilaya alisema, mimi na Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya tunazuia. Ashindwe kwa Jina la Yesu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekwenda mimi na Naibu Waziri wa Maji Mheshimiwa Kakunda wakati ule, mradi wa maji wa Lahoda uliojengwa na Mkandarasi Mrimi Construction akalipwa shilingi milioni 451, hautoi hata tone moja na maji. Hata tone hakuna, wala kisima hakikuchimbwa na mtu kalipwa fedha zote. Tukisema sisi, kesho wanakuja watu TAMISEMI pale, aah, unajua Mbunge anataka rushwa. Nendeni mkachunguze ili mjue kuna rushwa kweli?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapakaziana tu! Mtu anaandika taarifa huko, unajua Mbunge anataka rushwa, unaitwa TAKUKURU. Nenda kachunguze, kama kuna tone la maji, kama sio mimi na Mwenyekiti wangu kwenda kuwaomba watu wa RIC watusaidie pale, lakini Mrimi Construction amelipwa milioni 450…

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Keissy, usinijaribu.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa Mheshimiwa Nkamia, mzungumzaji, kwamba kule kwangu Wakandarasi walimfuata Mheshimiwa Nkamia ili tuonane nao wanipe rushwa. Nikawaambia siwezi hilo jambo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nkamia, taarifa hiyo.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, kuna watu walinifuata hapa wanasema, bwana tusaidie kwa Mheshimiwa Keissy. Nikamtafuta Mheshimiwa Keissy mwenyewe, nikajua ndio hao hao. Nimeipokea kwa mikono 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naomba Mheshimiwa Waziri aunde Tume Maalum ichunguze matatizo yaliyoko Wilaya ya Chemba. Nashukuru Mheshimiwa Mkuchika upo wewe ni mtu mzima, naomba mtusaidie. Matatizo ya Chemba yanaweza kutuletea matatizo mengine makubwa. Haiwezekani Mkuu wa Wilaya anasimama saa sita barabarani anasimamisha magari kama traffic, yuko peke yake. Haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani Mkurugenzi wa Halmashauri anajenga kwa miezi miwili na anataka kuchimba kisima cha kuuza maji pale Chemba wakati watu wanakunywa maji kwenye kisima nilichochimba mimi. Where do you get money? Halafu anakwenda TAMISEMI pale, aah unajua Mbunge anataka rushwa, unajua Mwenyekiti wa Halmashauri anataka rushwa. Rushwa gani mimi? I have got my own investment bwana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwaambieni ninyi, hamtaki kuchukua hatua. Mnasubiri mpaka Mheshimiwa Rais aje? Eeh, mnapokea majungu mnayaona ya maana. Tunayowaambieni, mimi nimesema, undeni Tume ikachunguze ili mjue nani mwongo? Unapiga chapa ng’ombe milioni 290 senti tano haipo. Unatuambia mfumo ume-bust, benki una shilingi milioni 40 tu, zimeenda wapi hela? Halafu Mbunge akisema hapa, aah, unajua wale wana majungu sana wale, wale wana majungu sana wale! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda mahali wako, ukaone. Mnatuambia aah, mnajua wale ni wanasiasa tu, wanasiasa tu wale. Hata hao wote wawili pale kwangu waligombea Ubunge wakashindwa; wote ni wanasiasa. Ooh, unajua tutahakikisha Nkamia uchaguzi ujao jina lake halirudi. Kwani lisiporudi, kwa Mungu haliendi? (Kicheko/Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Nkamia.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)