Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Mahmoud Hassan Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri ya kizalendo anayoifanya katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Jafo na Mheshimiwa Mkuchika, kwa kazi nzuri wanazozifanya, bila kuwasahau Naibu Mawaziri; mjomba wangu Mheshimiwa Kandege na ndugu yangu Mheshimiwa Mwita Waitara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajielekeza katika maeneo makubwa manne. La kwanza ni barabara. Sisi Wabunge tunaotoka vijijini ndio tuna mtandao mkubwa sana wa barabara kuliko wanaotoka mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti inayopelekwa TARURA ni ndogo sana kuliko bajeti inayopelekwa kwenye miundombinu. Ifike wakati sasa hizi bajeti ziwe 50 kwa 50. TARURA wapate asilimia 50 pamoja na miundombinu wapate asilimia 50.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna sababu za msingi kusema hayo. Kwenye vijiji ndiyo kwenye wakulima na ndiyo kwenye wananchi waliokuwa wengi. Kwa hiyo, malighafi na chakula vinatoka vijijini. Kwa hiyo, tusipoboresha barabara za vijijini ni tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jafo ni shahidi, nimekwenda Wizarani kwake nikiwa na Mwenyekiti wangu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Mufindi kumlalamikia miundombinu ya barabara iliyoko katika vijiji vyetu. Barabara ya kutoka Mtili – Ifwagi – Mdabulo – Ihanu – Isipii mpaka Tazara mpaka Mlimba ni barabara mbaya sana. Toka TARURA wameingia madarakani hawajawahi kutengeneza zaidi ya kilometa 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii inaunganisha mikoa miwili, Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Iringa. Tumemwomba Waziri aje kwenye barabara hii, lakini hajafika, lakini najua leo atakapokuwa ana-wind up atatuambia lini atafika Mafinga, atafika Mufindi kukagua barabara hii, kusudi aweze kuwasaidia wananchi wa maeneo yale wapate usafiri wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili watu wanakufa kwa sababu miundombinu imekatika. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri alione hili jambo. Kwenye eneo hili tuna vijiji zaidi ya 30, tuna kata zaidi ya tisa, miundombinu haipitiki, kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Jafo afike kwenye eneo hili. Bahati nzuri alipata nafasi ya kufika Mdabulo Sekondari, akaona hali halisi ya hiyo barabara, yeye ni shahidi. Kwa hiyo, tunamwomba afike kwenye eneo hili na watu wa Mufindi wanataka kusikia kauli yake kuhusu barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine la barabara ni la Tambalang’ombe, Uyole, Ugwenza, Ikweha na Kwatwanga, nalo ni tatizo. Ukienda kwenye Jimbo la Mufindi Kaskazini, haya maeneo hayapitiki kwa sababu yanasimamiwa na TARURA na TARURA hawana fedha hatuwezi kuwalaumu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri afike kwenye maeneo haya aone hali halisi na aone malighafi za wananchi zinavyoharibika kwenye maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matumaini yangu Waziri atatembelea kwenye maeneo haya na atajionea hali halisi. Hata hivyo, tunamwomba sana Waziri atuletee upya tuiangalie Sheria ya TARURA, kwa sababu sisi kama Wabunge hatuna control ya TARURA, Madiwani hawana control ya TARURA, TARURA hawawajibiki kwa Madiwani, hawawajibiki kwa Wabunge, kwa hiyo, TARURA wenyewe ndiyo wanaamua barabara gani itengenezwe. Sisi tuna matatizo ya barabara kama wangekuwa wanahusika kwa Wabunge au kwa Madiwani, tungewaambia anzeni na barabara hii, hii acheni. Kwa hiyo, kwa utaratibu huu, wanatengeneza barabara wanazozitaka wao, siyo tunazozitaka sisi wawakilishi wa wananchi. Kwa hiyo, Sheria ya TARURA, ibadilishwe, tuiangalie upya, kwamba wawe wanawajibika kwenye Kamati za Fedha za Halmashauri, kusudi tuweze kuwashauri tuanze na barabara gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo naomba kuchangia ni eneo la afya. Jimbo la Mufindi Kaskazini lina tarafa nne (4), lakini tuna kituo kimoja tu cha afya na mwaka jana tuliahidiwa kupelekewa milioni 300 kwenye kituo kimoja cha afya, lakini mpaka leo hazijafika. Kwa hiyo, pamoja na kazi nzuri aliyoifanya Mheshimiwa Jafo ya kutupelekea milioni 400 kwenye kituo cha afya cha Ifwagi, tunaomba kwenye kile kituo kiwepo, tupelekewe milioni 300 na hii ilikuwa ni ahadi ya kipindi kilichopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tusiishie hapa, kwa sababu tuna tarafa nne, at least kwenye kila tarafa tupate kituo kimoja cha afya, tutakuwa tumefikia jinsi gani ya kuwasaidia wananchi. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Jafo kwenye kila tarafa moja, tupate kituo kimoja cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka kuchangia...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)