Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Azza Hilal Hamad

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijaalia afya na uzima na hatimaye nimeweza kusimama ndani ya ukumbi wako huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami nianze kuchangia bajeti ya Ofisi ya Rais TAMISEMI. Leo nitakuwa tofauti sana na mlivyonizoea, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi kubwa ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya Kitaifa ndani ya miaka mitatu. Ununuzi wa ndege, reli ya standard gauge, mradi mkubwa wa umeme wa Mto Rufiji, Vituo vya Afya 352 na elimu bure shilingi bilioni 20.8 kila mwezi. Mheshimiwa Rais anastahili pongezi kubwa. Kikubwa kwake tumwombee dua kwa Mwenyezi Mungu, ampe afya njema, umri mrefu aende kuwatumikia wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo, Naibu Mawaziri na Watendaji wote katika ofisi yake. Mmekuwa mkifanya kazi kubwa ndani ya ofisi ya TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejionea mambo makubwa ambayo yamefanywa katika Mkoa wa Shinyanga na Serikali ya Awamu ya Tano. Nianze kwenye elimu. Mkoa wa Shinyanga katika Shule za Sekondari na Shule za Msingi kila mwezi tunapata shilingi milioni 594, kwa nini nisisimame na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Mkoa wa Shinyanga kwa mwaka huu wa fedha uliokwisha tumepata fedha za kujenga na kukamilisha maboma shilingi bilioni tatu ndani ya Mkoa wa Shinyanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haitoshi, nimetazama ndani ya kitabu cha Mheshimiwa Jafo, hata mwaka huu tumepangiwa fedha tena kwenda kukamilisha maboma kwenye shule zetu, shilingi milioni 425. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye ujenzi wa Vituo vya Afya. Katika vituo 352 vilivyojengwa nchi nzima, Mkoa wa Shinyanga tumepata vituo tisa ambavyo vimejengwa. Thamani yake ni shilingi bilioni 3.9. Naishukuru sana Serikali na ninampongeza sana Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Jafo, peleka salamu za wananchi wa Shinyanga kwa Mheshimiwa Rais. Wananchi wa Shinyanga na wanawake wa Mkoa wa Shinyanga tunamshukuru sana kwa kazi kubwa ambayo ameifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kusema kwamba toka nimeingia ndani ya ukumbi huu wa Bunge, mitaa hii hapa ninayokaa nilikuwa nikisimama tu kuchangia TAMISEMI wanasema, Hospitali ya Wilaya. Hilo ndilo lilikuwa neno langu kubwa. Hakuna mwaka ambao nilisimama na nisiseme ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Shinyanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia fursa hii kuishukuru sana Serikali, imetupatia fedha, shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga. Haitoshi, katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu tumepatiwa pia shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Haitoshi, Halmashauri ya Msalala tumepewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Shinyanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado nimetazama katika kitabu cha Hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, tumetengewa shilingi milioni 400 kwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kwenda kuboresha Vituo vyetu vya Afya. Nitumie fursa hii kuishukuru Serikali na kuipongeza kwa kazi kubwa ambayo wameifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aombaye hupewa na abishae hufunguliwa. Baada ya shukurani zangu hizo, namwomba sasa Mheshimiwa Jafo, kwa yale mambo yote makubwa ambayo wameyafanya ndani ya Mkoa wa Shinyanga na Halmashauri zake zote, kuna zahanati ambazo zilianzishwa kwa lengo la kuwa Vituo vya Afya; na alipokuja Makamu wa Rais, Mheshimiwa Mama Samia nilizisema zahanati hizi katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga; Zahanati ya Solo na Zahanati ya Ihalo. Wananchi kwa nguvu zao wamejenga majengo mengi, wodi za wazazi na watoto. Tunaomba angalau tupate hata shilingi milioni 200 ili zahanati hizi ziende zikafanye kazi kubwa ya kuwahudumia wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado haitoshi, alipokuja Mheshimiwa Waziri Mkuu mwaka 2018 niliomba katika Halmashari ya Wilaya ya Kishapu Kituo cha Afya cha Nobola. Kituo kile kinahudumia Tarafa nzima katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu. Naombe nao muwafikirie waweze kupata fedha kile kituo kiweze kuboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa elimu kwa Mkoa wa Shinyanga, namwomba sana Mheshimiwa Jafo, katika Shule za Sekondari, tuna shule ambazo nimekuwa nikizisemea; Shule ya Sekondari Samuye, shule hii iko katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. Tatizo kubwa la shule hii, hii ni Shule ya Kitarafa, wanafunzi wengi wanatoka mbali. Ombi langu kwako ni bweni tu wala sina ombi lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuiombea Shule ya Sekondari ya Ukenyenge ambayo pia ni Shule ya Kitarafa iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu. Ombi kubwa katika shule hii ni bweni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwekiti, haitoshi. Katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga nitumie fursa hii kuiombea fedha Shule ya Sekondari ya Old Shinyanga ambayo pia ni Shule ya Kitarafa. Ombi langu kubwa ni ujenzi wa bweni ili tuwaondoe wasichana kurubuniwa barabarani wanapokuwa wanaenda shule na kurudi majumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuzisemea shule zetu za msingi. Alipokuja Mheshimiwa Waziri Mkuu tukiwa Kishapu niliiombea Shule ya Msingi Beredi na Shule ya Msingi Mwangili. Mheshimiwa Waziri Mkuu alilipokea na aliyekuwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Kakunda aliahidi kwamba shule hizi zitaletewa fedha. Shule hizi zina msongamano mkubwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)