Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Eng. Joel Makanyaga Mwaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chilonwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwnyekiti, kwanza kabisa, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuwa mmoja kati ya wachangiaji wa hotuba ya Waziri wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hilo niendelee kumpongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa kazi yake kubwa anayoifanya. Hapa tunapiga kelele ya vitu vingi lakini wenye kusikia wamesikia. Leo akiwa safarini kwenda Arusha amezungumza mambo mazito juu ya watu wanaoleta fujo na biashara yetu ya sukari. Ni jambo ambalo linawagusa wananchi na yeye mwenyewe linamgusa sana ndiyo maana analikemea kila anapokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza kwa dhati kabisa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa hotuba yake nzuri aliyoiwasilisha kwa umakini kabisa. Wakati akianza nilikuwa naangalia kitabu chake kilivyo kikubwa nikasema hii itakuwa kazi hapa lakini ikawa kazi kweli. Amei-summarize kwa uzuri kabisa, hakuna kitu alichoacha ambacho mtu hakuelewa. Utapitia na utapata details za yale aliyokuwa ameya-summarize, nampongeza sana. Amezungumzia kwa undani kuhusu viwanda kwamba Serikali yetu ya Awamu ya Tano inajipanga kufanya nini kwenye viwanda, akizungumzia viwanda vidogo sana, viwanda vidogo na viwanda vikubwa. Amezungumzia biashara na uwekezaji wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba namuunga mkono na naunga mkono hoja hiyo. Naiunga mkono kwa dhati kabisa nikitambua kwamba safari tuliyonayo ambayo tumejiwekea ya kuingia kwenye uchumi wa kati hatujakosea njia. Njia sahihi ni hii ya kupitia viwanda, kwa nini? Tunapozungumzia kuelekea kwenye uchumi wa kati maana yake tunazungumzia kipato cha mtu mmoja mmoja ambapo mwisho tunazungumzia kipato cha Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tuna shida ya ajira, kama mtu hufanyi kazi hakuna jinsi utajiongezea kipato lakini unapokwenda kuwainua wananchi kwa viwanda maana yake unakwenda kunyanyua vipato vyao. Unaponyanua vipato vyao maana yake unapandisha kipato cha Taifa na hii ndiyo njia sahihi ya kutupeleka kwenye uchumi wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia kilimo, ili kilimo kiweze kuboreshwa lazima soko la uhakika liwepo. Kilimo kipo lakini soko halina uhakika, kwa hiyo kilimo kiko katika levels za chini. Tutakapoweka viwanda vitakavyofanya processing ya mazao yetu ya viwandani maana yake nini? Maana yake watu wengi zaidi wataji-engage kwenye kilimo ambacho soko lake lipo. Tunapozungumzia ufugaji vilevile, tunataka watu wafuge wakiwa na uhakika wa masoko yao. Tunapozungumzia uvuvi tunataka watu wavue wakiwa na uhakika wa masoko ya mazao wanayoyapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia viwanda maana yake tunazungumzia value addition ya products zetu tunazozipata. Hili ndilo tatizo kubwa ambalo tumekuwa nalo Watanzania, tatizo hili pia nchi za Afrika tumekuwa nalo sana, kazi yetu ni kuzalisha malighafi na kuwapelekea Wazungu na nchi za nje, wao wanaenda ku-add value, wanatengeneza faida kubwa na kuturudishia sisi tena.
Kwa hiyo, tunapokwenda kwenye hatua hii ya kuzalisha wenyewe, tunapata ajira. Tunapoweka viwanda maana yake kuna watu wanapata ajira viwandani kwa ajili ya ku-process yale mazao lakini mazao yanapotoka pale lazima yafanyiwe biashara, tayari watu wanapata biashara pale pale. Kwa hiyo, ukiangalia chain nzima, hii ndiyo njia sahihi ya kumuongezea kipato Mtanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda sasa nijikite kwangu kwenye Mkoa wa Dodoma, Wilaya ya Chamwino na hasa Jimboni kwangu Jimbo la Chilonwa. Jimboni kwangu ni wakulima na ni wafugaji. Tunalima kiasi cha kutosha pamoja na shida ya mvua iliyopo lakini Mungu anatujalia tunapata kiasi cha kutosha lakini tatizo kubwa ni soko. Nilizungumza juzi kwamba kama tukipata soko la uhakika watu watalima kwa wingi na viwanda vitapata malighafi za kutosha. Tunalima alizeti, ufuta na mahindi lakini soko lake ni duni. Kwa sababu hakuna soko la kuaminika wafanyabiashara wanakuja wananunua kwa bei wanazotaka. Kama tukiwa na uhakika wa viwanda kwamba nalima alizeti najua naipeleka kiwanda gani akinifuata mfanyabiashara nitamuuzia bei ambayo najua hii inanilipa mimi, inalipa muda wangu niliokuwa shambani, inalipa pembejeo zangu nilizotumia shambani na kupata faida kidogo lakini kwa sasa tunauza maadam tuuze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika upande wa viwanda na mazao yetu, kuna mazao yanahitaji viwanda vidogo vidogo, vidogo sana lakini kuna mazao yanahitaji viwanda vikubwa na vya kati kwa upande wa alizeti, ufuta na mahindi. Ninachokiomba kwa Serikali na kupitia kwako wewe Waziri hebu tuangalie namna ya kuwawezesha wananchi wapate mikopo ya kuweza kuanzisha hivi viwanda vidogo vidogo vya ku-process mazao yao kama alizeti, ufuta na mahindi. Sisi kwetu Chilonwa tuna biashara ya uhakika ya zabibu yenye shida ya soko.
Naomba nikuombe wewe sasa Waziri kupitia kwako Mwenyekiti tunahitaji tupewe kiwanda cha uhakika cha kutengeneza mvinyo. Tukipata kiwanda cha uhakika cha kutengeneza mvinyo maana yake watu kwa wingi sana watajitokeza kulima zao la zabibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda hili niliweke sawa kidogo. Kuna mchangiaji mwenzangu mmoja alisema kuna viwanda vya aina mbalimbali, naomba nishauri katika hili tusikimbilie viwanda tu, tunapofikiria viwanda basi tuweke viwanda vyenye teknolojia ya kisasa. Kwa mfano, unapozungumzia Kiwanda cha Mvinyo ambavyo ndiyo vingi viko hapa Dodoma vidogo vidogo, kazi yao ni kukamua ile zabibu na kutengeneza mvinyo, basi! Hayo siyo mazao peke yake unayoweza kuyapata kutokana na zabibu. Viwanda vya wenzetu vina-process unapata juice lakini unaweza ukai-ferment ukapata mvinyo (wine) lakini vilevile unaweza ukai-concentrate ukapata kitu kinaitwa concentrates hizi ambazo tunapigia kelele hapa kwamba wafanyabiashara wengi wa viwanda vya mvinyo wengi wana-import concentrates wanakuja kutengenezea mvinyo hapa wakisema kwamba wametumia zabibu za hapa nchini, sio kweli! Basi na sisi tuanzishe kiwanda cha namna hiyo tuweze kutengeneza juice, mvinyo na concentrates. Tukifanya hivyo tutakuwa tumefanya value addition kubwa sana na kuipatia nchi hii hata fedha za kigeni hasa tukizungumzia concentrates ambazo zina soko la uhakika huko nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nitamke kwamba naunga mkono hoja na ahsante sana.