Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO WA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kukushukuru wewe kwa fursa hii, lakini pili nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, mtoa hoja na timu nzima ya Wizara yake ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama na Mheshimiwa Waziri Mheshimiwa Angellah Kairuki na Naibu Mawaziri wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambapo wengi katika waliotoa hoja wamejielekeza katika kuona namna ambavyo sekta ya mifugo na sekta ya uvuvi zinaweza kuwa na mchango chanya katika pato la Taifa lakini vilevile katika kuinua maisha ya Mtanzania mmoja mmoja. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Wizara yetu ya Mifugo na Uvuvi imejipanga vyema sana katika kuhakikisha kuwa jambo hili la kuinua kipato cha Mtanzania mmoja mmoja linafanikiwa kupitia mifugo na uvuvi lakini vilevile kuwa mchango chanya katika pato kuu la Taifa. Mathalani, hivi sasa pato la Taifa katika upande wa mifugo ni asilimia 7 na upande wa uvuvi ni asilimia 3 na lengo letu ni kuinua na kuhakikisha kwamba asilimia hizi zinaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namna gani tutafanya, ni mikakati mizuri tuliyojiwekea. Moja, ni kuhakikisha kwamba tunadhibiti vyema mnyonyoro wa thamani kuanzia katika kumuandaa ng’ombe mpaka kwenda kumchakata ambapo hivi sasa tumehakikisha kuwa kuna viwanda vipya vinavyokwenda kujengwa vya kuchakata nyama ya ng’ombe. Pale Pwani tuna Kiwanda kikubwa cha Tanchoice lakini hapo Morogoro tunacho Kiwanda kikubwa cha Nguru Hills lakini vilevile tupo katika maridhiano na Serikali ya Misri ambapo tutatengeneza kiwanda kikubwa sana pale Ruvu ambacho kitakuwa na uwezo wa kuhakikisha kuwa nyama nyingi inakuwa processed pale lakini vilevile ngozi na mazao mengine ya mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Dawati la Sekta Binafsi ambalo tumelianzisha sisi Wizarani kwetu, tumehakikisha vile viwanda ambavyo vilikuwa vinasuasua tumeviwezesha. Mathalani, katika upande wa nyama Kiwanda cha Chobo pale Mwanza, tumesaidiana na wenzetu wa Benki ya Kilimo, katika kuhakikisha kuwa wanauchukua mkopo wao na kuwasaidia zaidi ili kuwajengea uwezo ambapo kiwanda kilikuwa kinaonekana kuwa kinasuasua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lkini vilevile upande wa maziwa, tumefanya kazi kubwa ambapo hivi sasa kupitia agizo la Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli limewezesha Kiwanda cha Tanga Fresh kuwa na uwezo wa kutengeneza maziwa ya muda mrefu, tunaita UHT au Long Life Milk. Ndiyo kiwanda pekee katika Taifa hivi sasa kinachotengeneza maziwa lita zisizopungua 40,000 baada ya kuwezeshwa kupata mkopo wa shilingi 12 kutoka katika benki za kibiashara. Vilevile Wizara yetu tumewasaidia Tanga Fresh ambapo sasa wameweza kuchukuliwa mkopo wao huu na Benki yetu ya Kilimo (TADB) ambapo sasa watakuwa na uwezo zaidi hata wa kufikia lita 100,000 kuzi-process kwa siku moja. Hayo ni kwa ufupi katika upande wa mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa uvuvi, jambo kubwa tulilolifanya ni kuhakikisha kuwa tunafufua Shirika letu la TAFICO. Hadi sasa TAFICO inafanya vizuri, imeanza na tumeshapata pesa takribani shilingi bilioni 4.2 kutoka Serikali ya Japan ambazo zinaenda kusaidia katika kununua meli itakayoanza kufanya kazi ya kuvua samaki wetu lakini vilevile inaenda kufanya ushirikiano wa kuweza kupata meli zitakazokwenda kufanya uvuvi katika eneo la bahari kuu. Mchakato wa kupata eneo la bandari unaendelea ambapo tukishapata eneo hilo tukajenga bandari kazi ya uvuvi wa bahari kuu itakwenda kufanikiwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi pia wamezungumzia juu ya sheria na kanuni zetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Ulega.

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO WA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)