Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hoja iliyo mbele yetu, bajeti ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na meli au usafiri katika Ziwa Viktoria. Waziri Mkuu ametueleza namna walivyoweka mkataba ili kuweza kujenga meli katika Ziwa Viktoria. Tangu meli ya Viktoria iharibike ni karibu miaka saba. Wananchi wa Mkoa wa Kagera wameteseka sana na hasa wanawake ambao walikuwa wanatumia meli ile ili kuweza kusafirisha bidhaa na hasa za kilimo na kufanya biashara kati ya Mkoa wa Kagera au Bukoba na Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, meli hii sasa imekuwa ni hadithi. Tunaomba Waziri Mkuu atueleze pamoja na kusema kwamba wameweka meli kubwa ambayo itaweza kusafirisha abiria zaidi ya 1,000 na mizigo, je, hii meli itakamilika lini? Wananchi wa Mkoa wa Kagera kwa kweli tumeteseka kiasi cha kutosha kwa sababu bidhaa zote zinazokwenda Mkoa wa Kagera zinasafiri kwa njia ya barabara. Kwa hiyo, wananchi wa Mkoa wa Kagera wanateseka sana na kwa kweli tusingependa kulalamika kwamba labda mkoa wetu haupendwi, mnatutupa sana kutokana na matukio mbalimbali hata yale ya tetemeko majibu tuliyoyapewa, tunaonekana kwamba sisi ni watu ambao hatustahili sana kupata huduma kutoka katika Serikali hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye barabara vijijini. TARURA ni wakala ulioanzishwa ili kuona barabara za vijijini zinaweza kutengenezwa. Barabara hizi zilikuwa zinatengenezwa na Halmashauri za Wilaya, ikaonekana kwamba huu Wakala ungeweza kusaidia barabara hizi zikatengenezwa na zikaweza kupitika mwaka mzima. Mimi niseme, TARURA wanafanya kazi nzuri tatizo walilonalo ni ukosefu wa fedha. Serikali haitoi fedha za kutosha kwa TARURA ili waweze kutengeneza barabara vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mfano mdogo tu. Mimi ninafanya kazi katika Halmashauri ya Bukoba Vijijini, wana mtandao wa barabara kilomita 593 na wanapewa bajeti ambayo ni shilingi milioni 800.09 tu kwa bajeti ya mwaka mzima. Ukigawa hizo hela kwa kilomita 593 kila kilomita inapewa karibu shilingi milioni 1.4. Unaweza kuona, je, hiyo pesa inatosha TARURA kuweza kutengeneza barabara nzuri? TARURA wanaweza kutengeneza barabara kama zile zilizokuwa zinatengenezwa na Halmashauri, wanapitisha magreda na mvua ikinyesha zinarudi kule kule zinakuwa mbovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuiambie Serikali kwamba pamoja na kutengeneza huu Wakala wa TARURA, basi wapewe pesa za kutosha. Mjue kwamba kule vijijini ndiyo kuna mtandano mkubwa sana wa barabara na wananchi wanataka huduma hiyo ili waweze kusafirisha mazao yao na kuweza kuinua kipato na maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niongelee kuhusu Tume ya Uchaguzi. Waziri Mkuu ametuonesha jinsi vituo vilivyoongezeka Tanzania Bara, Tanzania Visiwani kule lakini Tume hii ya Uchaguzi naiona kama ndiyo Taasisi pekee ambayo inaweza kudumisha amani katika nchi yetu; ni Taasisi ambayo kazi yake ni kupanga safu ya uongozi katika nchi hii; ni Taasisi ambayo inasimamia moja ya kigezo cha demokrasia katika nchi, kwa sababu uchaguzi ndiyo mwisho wake unaleta matatizo katika nchi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume hii kwa kuangalia uchaguzi mdogo uliofanyika, wote uliofanyika baada ya uchaguzi wa 2015, wamefanya mambo ya ajabu na ya kushangaza sana. Mimi nina jina langu ambalo ningeweza kuita Tume, lakini naogopa msije mkaniambia futa maneno, kwa sababu hii Tume nimeipima nikasema ni kitu gani hiki? Tumekuwa na Tume miaka nenda rudi lakini siyo Tume hii tuliyonayo sasa hivi. Hawa watu nao wamejitoa ufahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshuhudia chaguzi Wilaya ya Muleba katika Kata ya Buhangaza. Nilimwona Mkurugenzi anakuja na Polisi nikiwepo kwa macho yangu. Polisi sita, bunduki sita, anakuja kubeba boksi kama mwizi. Huyo ni Mkurugenzi ambaye anasimamia uchaguzi, yuko chini ya Tume. Wakurugenzi walio wengi ni makada wa Chama cha Mapinduzi, inawezekana wamepewa maelekezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa tahadhari kwamba Tume inawaona Watanzania kama watu legevu, Watanzania ambao wamelelewa katika misingi ya kutopenda kufanya vurugu, Ninachotaka kuwaambia, Tume isitupeleke Watanzania kwenda kufanya mambo yasiyostahili katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa Monduli, nimeshuhudia kwa macho yangu, nilikuwa Mto wa Mbu, nimeona ni jinsi gani Polisi wameweka magari zaidi ya 15, niliyahesabu, magari ya washawasha, wanatisha wananchi. Hatuwezi kufanya uchaguzi wa vitisho. Unatisha wananchi wanashindwa kutoka nje kwenda kupiga kura halafu unasema umeshinda, umeshinda kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Tume sasa iwe huru na pale ambapo uchaguzi utafanikiwa kwa uhuru na haki, mtu atakubali kwa sababu kwa miaka yote ya nyuma mbona tulikuwa tunakubali mtu akishinda anamshika mwenzake mkono! Kinachotokea sasa, nami nashangaa Serikali iliyoko madarakani, tazama mlivyo wengi ndani ya Bunge, mnahofia nini? Kama mnajigamba kwamba mnafanya kazi nzuri, mnasema maneno yenu, mmefanya kazi, sasa mna wasiwasi gani? Kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kama wewe unajiamini, unaendaje kwenda kufanya madhara ambayo yanafanywa na Tume? Sasa hivi katika siasa za Tanzania sisi upande wa Upinzani tunashindana na dola, hatushindani na Chama cha Mapinduzi. Nami nimeona kwa style hii kumbe ninyi ni wepesi kama hamna Polisi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Tume, Waziri Mkuu atueleze: Je, BVR zimenunuliwa katika nchi yetu? Ziko ngapi? Zinatosheleza? Tunaomba kujua wananchi wanajiandikisha lini? Tunaomba kujua ni lini Watanzania wataweza kukagua majina yao katika daftari la wapiga kura? Kwa sababu tangu mwaka 2015 hili daftari la wapiga kura halijawahi kuboreshwa. Sasa kama linaboreshwa, je ni lini?

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Rwamlaza, kuna taarifa.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tu kupunguza pressure kidogo ya suala la daftari kwa Mheshimiwa Mbunge, naomba tu nimpe Taarifa kwamba Serikali hii sikivu ambayo inafanya kazi kwa umakini sana, suala la uboreshaji Daftari la Wapiga Kura kwa mujibu wa sheria na Katiba, kazi hiyo imeshaanza. Sasa hivi Tume iko kwenye hatua ya awali ya kufanya majaribio ya vifaa vyake na mfumo mzima na kanuni zilizopitishwa na Vyama vya Siasa. Wameshaanza hiyo kazi Wilaya ya Kisarawe na hapo Morogoro. Kwa hiyo, Kata mbili sasa hivi ziko kwenye majaribio na mwezi wa Tano tunaanza uboreshaji wa Daftari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tu nimwambie Mheshimiwa Mbunge pressure itulie, BVR ziko za kumwaga, kila kitu kiko tayari kabisa. Tuko tayari kabisa kwa kuanza kuboresha Daftari. (Makofi)

MWENYEKITI: Mhesimwa Rwamlaza, taarifa hiyo.

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jenista Taarifa hiyo Mheshimiwa Jenista wasifanye siri, uchaguzi siyo siri, uchaguzi siyo msiba bwana kwamba hautakuwa na maandalizi. Semeni basi Watanzania wajue mnachokifanya, mpaka uulizwe hapa? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wakijua, watajua kwamba sasa uchaguzi wetu utafanyika kwa uhuru na haki. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Si umeshasikia lakini sasa!

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa kwa mzungumzaji.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kumpa Taarifa mzungumzaji kwamba ni kweli daftari la mfano limeshaanza na ukiwemo Mkoa wangu wa Morogoro, mimi kama Mwenyekiti wa Chama, CHADEMA Mkoa wa Morogoro na Mjumbe wa Kamati Kuu, tumeingia kwenye hilo zoezi kwenye Kata moja ya Kihonda. Sisi kama wadau wakubwa wa Daftari hili tumezuia kabisa na Tume kuhamasisha wananchi waende wakajiandikishe isipokuwa Tume wametangaza siku moja tu na hawakufika kwenye maeneo ya mbali ambayo wananchi walipo. Kwa hiyo, Daftari limeenda kwa kusuasua sana, mpaka limemalizika juzi ni wananchi 6,000 tu ndio waliojiandikisha. Kwa hiyo, ni CCM tupu ndiyo wanaofanya hiyo kampeni. (Makofi)

Hiyo nakupa… (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Rwamlaza.

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa hiyo, kwa sababu najua lazima mizengwe ifanyike katika uchaguzi huu. Kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa Waziri, hakikisha kwamba mambo yanaenda vizuri. Wewe ni mwanamama kwa sababu nchi hii ikiingia kwenye matatizo kuna matatizo kuna siku utakuja kusimama na kuomba samahani kwa wananchi kama Rais wa Algeria alivyofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mnapofanya matendo haya msijue kwamba baadaye huko Mungu akikujalia ukafika miaka 90 kwamba hutaweza kulaumiwa na baadaye ukasimama mbele ya watu kuomba msamaha kwa matendo machafu yaliyofanyika. Kama watu wataingizwa katika hali mbaya au katika mapigano au katika malalamiko na mambo mengine ambayo hayastahili kutokea kutokana na uchaguzi mbaya unaotokea katika nchi hii. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)