Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa na mimi nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa na nzuri ambayo inafanywa katika Taifa hili na hasa ukizingatia kwamba yeye ndiyo msimamizi wa kazi na shughuli zote za Serikali ndani ya Taifa hili chini ya uongozi thabiti wa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Nawashukuru sana kwa sababu tumeyaona mambo makubwa yaliyofanyika na mafanikio makubwa ambayo tumeyapata kwenye elimu, afya, madini, nishati na kadhalika. Vilevile nawapongeza Mawaziri, Naibu Mawaziri, Katibu Wakuu na watendaji wote ambao wanafanya kazi chini ya Wizara hii kwa uandishi mzuri wa hotuba hii na utekelezaji uliotukuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye hotuba hii ukurasa wa 60, Serikali imefanya jambo moja kubwa zuri ambapo imewatambua wazee wetu kwa kuwapatia vitambulisho ili waweze kutibiwa bure. Wazee wetu hawa ndiyo wamejenga Taifa letu, wakiwa vijana wametumia nguvu zao na rasilimali zao kulijenga Taifa hili. Sasa hivi wamezeeka, wameishiwa nguvu, magonjwa yanawaandama kila kukicha, hawana tena mishahara, hawana nguvu za kuweza kutengeneza au kufanya kazi za kuzalisha mali kwa hiyo hawana hela ya kujitibia. Kwa hiyo, huu mpango mzuri wa Serikali wa kuwatambua wazee na kuwapa vitambulisho watibiwe bure ni mzuri na naupongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukurasa wa 60 wanasema hadi sasa wazee ambao wameshapewa vitambulisho ni 1, 042,329. Naomba Serikali iongeze kasi kuwatambua wazee ili ifikapo mwisho wa mwaka huu basi wazee wote wawe wameshatambuliwa na waweze kupewa vitambulisho watibiwe bure katika nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunatambua kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wetu, wote tunatambua kwamba katika Tanzania kwa miaka mingi ijayo sekta ya kilimo itaendelea kutoa ajira kwa watu wengi zaidi kuliko sekta nyingine yoyote ile lakini sasa hivi tunaandaa viwanda ambavyo vinategemea kupata malighafi kutoka kwenye sekta hii. Vilevile tunamuona Waziri Mkuu anavyojitahidi kuboresha na kuongeza tija katika mazao ya kimkakati ikiwemo kahawa, pamba, tumbaku, chai pamoja na korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli uzalishaji umeongezeka lakini pamoja na kazi nzuri ambayo imefanyika, tatizo tunalolipata ni masoko. Wote tunakumbuka mwaka juzi tuliona kilichotokea kwenye mbaazi, tatizo lilikuwa ni masoko. Wote tumeona kilichotokea mwaka jana kwenye kahawa na korosho tatizo ni soko na kwenye mahindi kuna wakati yalizalishwa yakakosa soko bei ikawa ndogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaangalia haya mazao ya kimkakati mengi yanauzwa nje, kwa hiyo, bei ya dunia ikishuka kidogo tu, huku inakuwa ni kiama kwa sababu bei kwa mkulima inaporomoka sana, mkulima anapata hasara. Kwa hiyo, napendekeza kwa Serikali kwa kuwa haya mazao ya kimkakati yanategemea bei kutoka nje, basi Serikali ianzishe mfuko ambao unaitwa Crops Price Stabilization Fund wa kumfidia mkulima kusudi hata kama bei ya dunia ikianguka, mkulima asipate hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili siliongelei mara ya kwanza, ni mara kadhaa nikiwa nachangia nalizungumza, wenzetu nchi za nje kama mkulima kukitokea natural disasters bei ikateremka kunakuwa na ruzuku anapewa kusudi asipate hasara. Nasi tuweke mfuko, mwaka huu korosho wamesaidiwa na Rais lakini tukiwa na mfuko unaoeleweka utasaidia kwenye kila zao ambalo bei zitakuwa zimeporomoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa Botswana nilizungumza na mtaalam mmoja nikitaka kujua wao wanawezaje, wao ni wafugaji kama sisi lakini nyama wanauza nje na wanapata hela za kigeni nyingi sana kutokana na mauzo ya nyama. Wakaniambia kwamba siyo kazi rahisi, hawakurupuki tu kwenda kuuza nje, wanaandaa tangu ndama wamemlishaje, wametumia viuatilifu na vyakula gani mpaka wanapokwenda kuuza wanakuwa na masoko tayari, wanazalisha kufuatana na hitaji la soko. Tujiulize tunavyopata matatizo katika kuuza mazao yetu, je, sisi tunapokuwa tunazalisha kahawa, pamba na korosho kuna soko tunalo-target, tumejiandaa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali kwa kutumia idara ambazo zinahusika na masoko waende huko nje watafute masoko. Watafute nchi marafiki zetu, waingie mikataba nao, watafute mashirika makubwa waingie mikataba nao kusudi tujue kwamba korosho au kahawa ya mtanzania tukishaizalisha tutaenda kuiuza wapi. Vilevile tuandae wakulima waanze kuandaa mazao yao kufuatana na mahitaji ya soko, tusiwaache wakalima vyovyote vile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa mfano wa Mkoa wa Kagera. Tunao watu ambao wanauza kahawa nje lakini unakuta wanawalea wale wakulima tangu zao linapoanza, ule mbuni wanalea kwa mwaka mzima, mbolea gani utumie na mbolea gani usitumie, viuatilifu (insecticides) gani utumie na vipi usitumie, kusudi unapokuwa umezalisha ile kahawa iwe inakubalika kwenye soko lile ulilolilenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza kwamba sasa tuanze kuwalea wakulima kwa maana ya uzalishaji, tuwezeshe zile taasisi zinazofanya tafiti tuwape fedha kusudi waweze kufanya utafiti wazalishe mbegu bora, wakulima wazipande, tuweke mbolea ya kutosha kwa sababu Tanzania hatutumii mbolea ya kutosha, tuzalishe mazao bora kusudi mwisho wa siku mkulima aweze kupata bei inayofaa kwa sababu tutakuwa tumepata mazao bora. Nasisitiza ni kazi ya Serikali kuwahakikisha kwamba wanatafuta masoko kwa ajili ya mazao ya mkulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana ya msimu wa kahawa kwa Mkoa wa Kagera utaanza mwezi ujao wa Mei. Tunaomba Serikali ile mikakati ambayo sasa inapangwa iweze kupelekwa kwa wadau waielewe mapema kusudi tusije tukapata matatizo kama tuliyoyapata kwenye msimu uliopita. Vilevile direct export inaruhusiwa, hawa ni wanunuzi binafsi lakini Serikali isitoe kabisa mkono wake, ihakikishe kwamba inaweka bei elekezi kusudi hawa wanunuzi binafsi wasije wakawanyonya wakulima wakawapa bei ndogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa namalizia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mshashu.

MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)