Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Suleiman Masoud Nchambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kishapu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nikushukuru sana na nikupongeze kwa moyo wako wa kijasiri wakati kina mama wenzako walipokuwa wakijaribu kukuzomea. Nikutie moyo kwani hata Yesu Kristo wakati akiitangaza injili alipokuwa akipita katika mitaa wengi walimbeza, wengi walimuuliza eti wewe ni mwana wa Mungu, eti wewe ni mtakatifu na yeye aliwajibu ninyi mwasema. (Makofi)
Kwa hiyo, hicho wanachokisema wao ni wao wanakisema. Mimi nikutie moyo mama yangu umeanza vizuri, ongeza kasi na sisi Wabunge shapu tutaendelea kukunoa uwe shapu, mambo yako yaende kwa ushapu na Bunge hili lifanye kazi ya kutekeleza mipango mizuri ambayo wananchi wameingia mkataba na Chama cha Mapinduzi wakati wa uchaguzi na Chama cha Mapinduzi kimekabidhi Ilani ambayo inatekelezwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maandiko matakatifu yanasema na wala msifanane na hao kwa kuwa baba yenu anayajua mahitaji yenu kabla ninyi hamjamuomba. Kwa hiyo, sisi tunayo imani Watanzania lipo jambo waliliomba na kupitia Serikali ya Chama cha Mapinduzi Mungu amekabidhi usukani wakiwa na imani wakati wanaomba kama maandiko yanavyosema, niombeni na mkiamini mtapata, Bwana Asifiwe.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa niwape hesabu rahisi sana Waheshimiwa Wabunge. Mbunge mmoja wa Upinzani amesifu sana hotuba yao ya Upinzani, kitabu hiki kilichowasilishwa na kambi ya wenzetu kina kurasa 28 wakati kitabu cha Mheshimiwa Mwijage kina kurasa 217. Katika kurasa 28 zilizowasilishwa na Kambi ya Upinzani, ukurasa wa kwanza, mwasilishaji amewashukuru wapiga kura wake, ukurasa wa pili ametukana, ukurasa wa nne ametoa lawama tu, ukurasa wa nane imetukana na kukisema Chama cha Mapinduzi, ukurasa wa 27 na 28 ni kama viambatanisho. Kwa hiyo, ni dhahiri katika kurasa hizi sita zimebaki 22 ambazo asilimia 70 ya mistari iliyopo katika kitabu hiki kinachowasilishwa na wenzetu wa upinzani ni lawama, kejeli, matusi na mengineyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ukipiga hesabu rahisi kurasa 217 ukigawanya kwa kurasa 22 ni kwamba wapinzani hawayajui matatizo ya Watanzania na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kupitia Waziri mchapakazi, hodari Mheshimiwa Mwijage amekwenda mara kumi zaidi ya matatizo wao wanavyoyajua, hiyo ni hesabu rahisi.
Kwa hiyo, ndugu zangu Wabunge mimi niwatie moyo kazi wanayoifanya wenzetu kwa sisi wafugaji tunapokwenda na ng‟ombe zetu kwenye mabwawa ama malambo, huwa wanaangalia saa hiyo sauti ya vyura ipo wapi ili wajue maji pale ndiyo yana kina kirefu wanakwenda wanakunywa. Kwa hiyo, wao wanapiga kelele kama vyura sisi tunanywesha ng‟ombe zetu, Watanzania wanapata maziwa, wanapata nyama ambazo sasa ndizo shughuli za maendeleo na matatizo na kero zao. Hawa ndiyo kazi iliyowaleta Bungeni wala msiwalaumu, wataendelea kupiga kelele kama vyura na ninyi Mawaziri chapeni kazi sisi Wabunge tutawasaidia na Wabunge wa CCM tufanye kazi ya kuishauri na kuikosoa na kuielekeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Magufuli amekuja na mkakati wa mabadiliko. Nilikuwa napitapita mtaani naongea na wenzangu kule wanasema kazi anayoifanya Mheshimiwa Magufuli ndiyo haswa ilikuwa kazi yetu sisi UKAWA, tena wengine wenzangu wa Zanzibar maana kuna Wabunge wenzangu kule Zanzibar wanakalia Dole, wengine wanakalia Mkanyageni, wengine wapo Mwembemchomeke, ni rafiki zangu huwa nakwenda kuwatembelea wakati mwingine katika maeneo yao hayo niliyoyataja wana Kiswahili ambacho kinazingatia misingi ya neno waliloliongea wanasema haswa anachokifanya Mheshimiwa Magufuli ndiyo ilikuwa hoja ya UKAWA kutekeleza mambo anayoyafanya yeye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka niwaambie ndugu zangu wakati fulani niliwahi kumwambia Waziri fulani wa CCM humu ndani nisingependa kumtaja, muda mwingine mtu akisoma sana akafika mwisho huwa nahisi mimi akili inarudi reverse. Sasa inategemea, inarudi reverse pengine dhamira yake ama ubongo wake umepata frustration fulani maana shetani huwa haonekani, unaona matendo unasema huyu matendo yake yanafanana na shetani. Maneno yake na matamshi yake yanafanana na shetani lakini mimi sijawahi kumuona na sina reference ya kitabu chochote cha Mungu ambacho kiliwahi kumuona shetani kupitia binadamu hapa duniani, lakini matendo ya mtu ndio yanamfanya aonekane ni mtakatifu ama shetani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ndugu zangu zipo lugha zinatumika ambazo Wabunge hao hao wanaotumia lugha hizo wanakuja na madai ya wao kuheshimika katika Taifa hili na Bunge hili, haiwezekani! Waziri anayechukua dhamana ya Wizara katika Wizara yake leo anaitwa muhuni, tapeli na maneno mengine.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Wacha muda uishe lakini nataka niwaeleze ukweli, kwa sababu kazi zenu ninyi ndizo hizo mnazozifanya. Lugha hizi hazipendezi sana…
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Nitachangia kwa maandishi msiwe na haraka, mbona sindano zikiwa zinawaingia upande wenu mnapiga kelele, quinine huwasha baadaye masikioni, tulieni kwanza tuwape vidonge vyenu maana mmekuja kufanya kazi ambayo mnaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi hawa kelele zao wala hazinipi shida mimi ni Mbunge shapu wala sina matatizo na wao.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo tatizo la baadhi ya majimbo kuruhusu watu ambao hawakuwa na sifa na wala hawakujiandaa kuja kutetea wananchi wao kuingia ndani ya nyumba hii lakini angekuwa amejiandaa, amejipanga na anajua wajibu wake wa kibunge ndani ya jumba hili takatifu asingekuwa anaropoka kama mwendawazimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikuhakikishie Watanzania wanaona na wanasikia. Nakuapia Mungu niliwahi kuwaambia wenzenu, shemeji zangu wa Kigoma akina Kafulila, niliwaambia kasomeni Luka 6:38, mtalipwa kwa kile mnachokifanya ndani ya jumba hili leo wako wapi? Akina Machali, Kafulila na Mkosamali wako wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, huyu anayeropoka maneno haya wapiga kura wake watamuona, watamsikia, mwaka 2020 tutaagana naye kwa sababu kazi aliyoifanya ndiyo hiyo ya kuzomea na kutukana, hatarudi humu wala asiwape shida yoyote. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwaeleza wenzangu na kuwakumbusha misingi na wajibu wao ndani ya Bunge nieleze machache.
Mheshimiwa Naibu Spika, liko tatizo kubwa juu ya wakulima wetu, wakulima wetu wanapata tabu sana. Nikuombe Mheshimiwa Mwijage katika maeneo machache kulingana na muda na mengine nitachangia kwa maandishi. Mkitaka wakulima wa pamba waendelee ni lazima Serikali ijiandae kudhibiti bidhaa zote zinazotokana na mazao ya pamba zinazoingia nchini. Wako Wabunge humu walipiga kampeni tukatoa ushuru wa mazao mengi ya pamba kuingia katika Taifa hili tumewakandamiza Wasukuma wenzangu. Nataka nikuhakikishie zao la pamba nenda ka-review ili viwanda viwepo kutokana na zao la pamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, ubarikiwe sana.