Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nakushuruku kwa nafasi hii. Nichukue nafasi hii kutoa masikitiko yangu kwa niaba ya Kambi yetu kwamba hatujaridhishwa na mambo mengi. Napenda kutoa hayo masikitiko yangu.

Mheshimiwa Spika, lakini tuna mchango kutoka kwenye hotuba ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni ambao nimeambiwa tumepewa humu ndani na nitaeleza. Sisi kama Kambi ya Upinzani au kama CHADEMA hatujaridhishwa na mwenendo wa Tume ya Uchaguzi ambavyo imekuwa ikifanya kazi zake. Kumekuwa na upungufu mkubwa sana katika Tume ya Uchaguzi ambayo kimsingi tunaiona kwamba Tume haiko huru. Inasikitisha kwamba tuko kwenye nchi ya kidemokrasia, tuna referee ambaye anapaswa kuwa Tume huru ya Uchaguzi na badala yake siyo Tume huru ya Uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, tuna Tume ambayo Mwenyekiti wake ni mteule wa Rais ambaye ni Mwenyekiti wa chama fulani. Tunajiuliza, je, wengine wanafanyaje? Ni kwa nini yule ambaye ni Mwenyekiti wa chama ndiyo anatuchagulia refa ambapo sisi wengine hatuko kwenye chama chake? Kama hiyo haitoshi kwa maana ya muundo wa Tume, uongozi wake, Mwenyekiti wake, wasaidizi wake, Makamishna wanajikuta ni wateule wa Mwenyekiti wa chama fulani, automatic wanapoteza kile kinachoitwa kuwa huru katika kusimamia mchakato wa uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, sisi wote hapa tumekuwa tunashangilia ukitaja Simba au Yanga, ukimwambia referee ana maslahi na Yanga na aende kuchezesha mechi ya Simba watu wataandamana usiku kucha. Ni kwa nini sisi tuone ni fair tunakuwa na Mwenyekiti ambaye anaenda kupiga kipenga, ambaye anapaswa kusimama katika lakini ni mteule wa chama fulani.

Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi, tuna wasimamizi wasaidizi…

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Waziri wa Nchi.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, naomba tu kumpa taarifa mchangiaji kwamba Tume hii ya Uchaguzi na uteuzi wa viongozi wote waandamizi wa Tume iko kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tume hii kwa uhalali huo huo iliweza pia kumtangaza hata yeye Mheshimiwa Anatropia kuwa Mbunge na yuko ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waheshimiwa Wabunge wote ambao wako ndani ya Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba niendelee tu kumkumbusha Mheshimiwa Anatropia anapodai kwamba Tume hii siyo huru ina maana basi hata Ubunge wake yeye sio halali. Kama Ubunge wake ni halali na yuko ndani ya Bunge basi Tume hii imeendelea kufanya kazi yake kwa maadili na kwa kuzingatia Katiba na kwa sababu hawa viongozi wote wako kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Theonest pokea hiyo.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nadhani siyo lazima niipokee, kuna msemo wanasema the means justify the end na mimi ndiyo nachoeleza leo na kwenye Kambi yetu tumeshauri tulete hapa mabadiliko ya sheria husika tuwe na Tume huru. The means justify the end. Kama unavyonileta hapa Mbunge wa CHADEMA unategemea nitakaa kutetea CCM? Amekuja hapa Msajili wa Vyama vya Siasa ameshangiliwa sana na kuna mtu mmoja aka-post sitamtaja jina akasema wale ambao hamshangilii shauri yenu, hiyo inaonesha to what extent ile level ya independence ipo questionable, the means justify the end. (Makofi)

SPIKA: Kwa hiyo, angekuwa ni huyo ambaye wewe unasema awe angeshangiliwa ingekuwa ni mbaya? Sioni uhusiano wa kumshangilia mtu na role yake, endelea tu.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pili, tuna Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kwa maana ya Wakurugenzi wa Halmashauri kwenye Wilaya zetu. Ukiangalia composition ya watu wengi majority tunaweza kutaja hata majina wameshiriki kwenye kura za maoni za Chama cha Mapinduzi, baada ya kuachwa ndiyo wameenda kuteuliwa kuwa Wakurugenzi, to what extent wale watu wanaweza kuwa so independent? Hiyo yote inaleta questionability ya Tume whether ni huru au siyo huru.

Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi kuna funding yenyewe ya Tume, tuna Tume ambayo inategemea busara za Mwenyekiti kwa maana ya Mheshimiwa Rais hatuna namna ambayo tunaweza ku-finance Tume yetu zaidi ya kutegemea …

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Ruksa Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, tukiendelea kuacha haya maneno yatakuwa yanachukuliwa kama ni maneno sahihi lakini si kweli. Kwenye hotuba hii ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu tunayo Vote maalum kwa ajili ya Tume ya Uchaguzi na inatengewa bajeti na Bunge lako kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya Uchaguzi inapofika kwenye suala la uchaguzi, kisheria na Kikatiba fedha za uchaguzi zinatolewa na Mfuko Mkuu wa Serikali. Kwa hiyo, ni lazima atenganishe hayo mambo mawili, tusiendelee kuacha watu wanazungumza tu vitu ambavyo wakati mwingine siyo vya kweli. Vinginevyo nitakuja kuomba kanuni ya utaratibu na mwongozo ili Mheshimiwa Anatropia athibitishe kama Tume hii inapewa fedha kwa hisani. Tuna Vote hapa tutaipitisha na fedha za uchaguzi kwa mujibu wa Sheria na Katiba zinatengwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

SPIKA: Mheshimiwa Anatropia.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, taarifa nimeipokea lakini amount inayokuwa allocated kwenye Vote inaamuliwa na nani? Tutakuja hapa tutaongea, inaamuliwa na nani?

Mheshimiwa Spika, tunakuja kwenye uandikishaji wa BVR. Kumekuwepo na changamoto ya uandikishaji wa BVR tunakumbuka 2015 lakini hebu tuangalie tangu 2015 ni mara ngapi imekuwa updated na tumekuwa na chaguzi ngapi zilizofanyika hapa katikati. Ina maana assumption ni kwamba wale waliojiandikisha 2015 ndiyo bado wana exist kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ni kwa nini haiwi updated na kwa nini tunaendelea ku-maintain kwamba wale watu bado wako wote lakini wale ambao hawapo kwa nini hawatolewi na waliofikisha miaka 18 wako eligible ku-vote kwa nini wanakuwa hawaingizwi kwa wakati. Hiyo pia inatilia shaka uhuru wa Tume huru ya Uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, tuje kwenye suala lingine, Tume imeendesha chaguzi kadha wa kadha na nyingine zimekuja hizi mpya za voda faster ambazo hazioneshi uhalisia. Uhalisia wa uchaguzi unauona kwenye mchakato husika. Mchakato wa kwanza ni pamoja na watu kuchukua na kurudisha fomu, tuna wagombea niongelee Korogwe, mgombea amepiga kambi kwenye Ofisi ya Mkurugenzi Msaidizi wa Uchaguzi siku nzima, Mkurugenzi hatokei na deadline imefika na unaambiwa amekosa vigezo kwa sababu hajarudisha kwa wakati. Unaweza ukaona ni michakato ambayo inakuwa manipulated makusudi sijui ni kwa nia gani kwa sababu nchi inayoamini kwenye demokrasia nikiingia kwenye uchaguzi naamini nitashinda au utashindwa lakini ikifikia wakati mna mifumo ambayo haipo independent…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Unajua Mheshimiwa Anatropia unajiweka kwenye eneo ambalo nashindwa hata kukulinda lakini umechagua mwenyewe kujiweka kwenye eneo hilo ndiyo linakupa shida kidogo. Duniani hapa kama huyo mgombea wenu alipata matatizo fulani si alikuwa aende Mahakamani tu. Sasa ukituambia sisi Bunge hapa tufanye nini? Kama alifanyiwa jambo ambalo siyo sawa angeenda tu Mahakamani. Hizi taarifa unayosikia na nini wala yasingejitokeza. Endelea tu kuchangia muda bado ni wako, mtunzieni muda wake.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, ushiriki wa vyombo vya dola na kwa kiwango kikubwa katika mchakato mzima wa uchaguzi, tukianzia kupiga kura na kutangaza matokeo. Unaona nguvu kubwa inatumika lakini kama haitoshi kuna incidence ambapo Polisi wamekimbia na maboksi ya kupigia kura, imetokea Kinondoni. Nayaongea haya kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu yeye ndiyo msimamizi anapaswa kukumbusha watu wajibu wao, anapaswa kuangalia, je, taratibu zinafuatwa na kama hazifuatwi yeye ndiyo anasimamia. Ninaongea kwenye hotuba yake kwa sababu yeye ndiyo mtu anayehusika katika suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na mauaji na ugomvi mbalimbali, tuna Katibu wetu wa Kata ya Hananasifu aliuawa katika uchaguzi wa Kinondoni mpaka leo hatupewi taarifa uchunguzi umefikia wapi na aliuawa kwa nini? Hayo ni maswali ya kujiuliza, kama tuliamua ku-embrace demokrasia na tumeamua kuiweka pembeni na kucheza na mifumo tuliyonayo kwa ajili ya kupata matokeo, tunaiweka nchi yetu katika mazingira ambayo siyo sahihi. Tunaiweka nchi yetu katika mazingira ambayo sisi wenyewe tunai-push ambako wengine hawataki kwenda.

Mheshimiwa Spika, kugoma kutoa viapo vya Mawakala, huo ni mchakato wa kawaida wa uchaguzi, inakuwaje Wasimamizi Wasaidizi, Maafisa Watendaji wasitoe viapo kwa wakati? Kwa nini chama kimoja kipewe na kingine kisipewe? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naweza kuongea mengi, lakini mnapaswa kujua, kama tunaingia kwenye mchezo, naamini mnajinasibu kwamba Serikali yenu inafanya vizuri, imepeleka miradi, imepeleka maji, imepeleka shule, hebu twende kwenye uwanja sawa wa uchaguzi, tuwaache Watanzania wachague kati ya mliyoyatenda na sera zetu. Kati ya mlichowapelekea na sisi tutakachokuwa tunawaambia, kuliko kubaki nyuma kutumia vyombo vya dola vilivyopo, kucheza na Tume, kucheza na mfumo kwa ajili ya kupata matokeo. Tuacheni, naamini mmefanya mazuri, twendeni tukapige jaramba, wananchi wenyewe wataamua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakuja kwenye hoja yangu ya pili, naongelea uminywaji au mifumo ya utoaji haki isiyoridhisha. Leo kupewa dhamana katika Kituo cha Polisi au Mahakamani nimekuwa ni hisani siyo tena haki. Nitatoa mfano wa kilichomtokea Mwenyekiti wa CHADEMA, Mheshimiwa Aikaeli Mbowe. Sitaeleza chote kilichotokea, lakini Jaji Rumanyika alisema, kilichofanyika katika shauri hili ni sawa na kuchukua mzigo ukaufunga mbele ya mkokoteni, kwa maana ni mambo ambayo ni ya aibu. Akasema, masharti ya kufuta dhamana yanapaswa kuwa magumu kuliko masharti ya kutoa dhamana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Theonest, unajua unachojadili ni mambo ya Mahakamani ambayo tena kesi yenyewe bado inaendelea na pia, Jaji wa Mahakama ya juu anakosoa vitendo vya Mahakama ya chini yake. Sasa unataka Bunge tuingiliaje? Endelea tu Mheshimiwa Theonest, naona leo kidogo haujajipanga vizuri.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, natoa mfano wa kinachopaswa kusimamiwa. Ninaeleza kilichotokea, ninaeleza wajibu wetu kama watunga sheria. Ninaeleza umuhimu wa kutoa haki kwamba, ukienda Magerezani wamejaa watu ambao wangeweza hata kupatiwa dhamana tuka-save fedha nyingi za Serikali kuliko kuendelea kuweka watu ndani.

Mheshimiwa Spika, kumekuwepo kupandikiza kesi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Naambiwa ni kengele ya pili, lakini kwa kuwa ulikatizwa katizwa sana, nakuongeza dakika tatu.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kumekuwepo tatizo la Polisi kubambikiza kesi kwa wananchi likiwepo suala zima la money laundering. Sasa hivi ndiyo umekuwa mtindo wa kisasa. Ukitaka kupigwa kule ndani na usitoke, kesi unayobambikizwa ni ya money laundering ambayo upelelezi wake unachukua muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, ni lazima tuangalie hata vyombo vyetu vinavyofanya kazi. Nadhani ni kama wiki mbili au tatu zimepita tumepata taarifa ya mtu aliyebambikizwa kesi na Askari, lakini upelelezi ulivyokuja kujulikana ikaonekana alibambikizwa kesi na katika mazingira ambayo imeonekana siyo fair. Ni lazima tuangalie mifumo yetu, ni lazima tuangalie, nasi tunatoa rai kwa mujibu wa sera za chama chetu kwamba, kupatiwa haki haitakuwa tena hisani, haki ni lazima ipatikane na ipatikane kwa wakati. Siyo tu kupatikana kwa wakati, ni lazima ionekane inatendeka.

Mheshimiwa Spika, ninamaliza kwa kusema, sisi kama Chama cha Demokrasia na Maendeleo, tunaamini amani na utulivu wa nchi yetu utapatikana katika mifumo iliyopo ikiwa inasimiwa kwa amani. Nimetoa mfano mkubwa wa Tume ya Uchaguzi, kama tuki-temper na Tume ya Uchaguzi; kwa mfano, tunaenda kwenye chaguzi za Serikali za Mitaa, tuki-maneuver na chaguzi za Serikali za Mitaa tunaenda kuwasha moto ambao hatuujui.

Mheshimiwa Spika, wananchi hawako tayari kuzidi kuonewa kwa sababu ukweli wanaujua, haki zao wanazijua na ukweli wanaujua.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)