Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Hassanali Mohamedali Ibrahim

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiembesamaki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hi kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo ameisoma Bungeni leo hii asubuhi.

Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa pumzi zake mimi kusimama hapa nikiwa mzima. Nichukue nafasi hii adhimu kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hotuba yake iliyojaa busara na matumaini ya Watanzania. Kwa kweli naweza kusema katika timu aliyokuwa nayo Rais Mheshimiwa John Pombe Magufuli basi siyo vibaya tukampa Mheshimiwa Waziri Mkuu jina la mchezaji mashuhuri duniani kama Messi kwa sababu Messi kama anavyojulikana basi na Waziri Mkuu naye anafanyakazi nzuri sana kwa kumsaidia Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii nimpongeze vilevile Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa sababu hayo maendeleo ambayo tunayaona katika nchi hii ni moja katika jitihada zake kubwa anazochukua kuwasaidia Watanzania wanyonge na ni mashahidi wetu Watanzania pamoja na sisi Wabunge kwamba kazi anayoifanya Mheshimiwa John Pombe Magufuli ni kazi kubwa sana na kwa kweli anastahili pongezi katika miaka yake mitatu hii amefanyakazi, extra job au extra miles amekwenda Mheshimiwa Rais, kwa kweli tuzidi kumuombea Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nije katika changamoto sasa katika Wizara hii au katika mambo ambayo yataweza kusaidia kutupeleka mpaka 2019/2020. Changamoto iliyokuwepo mwanzo kwamba ni ajira (permit work). Permit work imeleta vilio kwa wale wawekezaji. Wanapokuja watu wao kutaka kufanyakazi katika nchi hii basi kupata permit work imekuwa kazi ngumu sana na hii inarudisha maendeleo ya Mheshimiwa Rais. Kuna watu wanapanga hujuma ya kurejesha maendeleo ya Mheshimiwa Rais na sisi hatutakubali kuona hayo yanafanyika katika nchi hii.

Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu nina ushahidi ya kwamba mtu ana kitega uchumi ambacho ame- invest billions of shillings halafu anaomba kupeleka permit yake ya engineer wake anakataliwa wakati katika kile kitega uchumi ana wafanyakazi 150 ambao wanategemea kupata riziki zao. Sasa kwa ajili ya mtu mmoja hiyo nafasi inakuwa inafungwa, wale wafanyakazi 150 ambao ni Watanzania wanakuwa hawana kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka Wizara hii ambayo inahusika na work permit kidogo walegeze kamba, tusiwavunje nguvu watega uchumi wetu wanaokuja kuleta maendeleo katika nchi yetu ili vilevile Mheshimiwa Kairuki ambaye sasa ameteuliwa karibuni kuwa Waziri wa investors protocol ningemuomba na Mheshimiwa Kairuki atusaidie katika masuala haya kwa sababu ni moja katika kuleta maendeleo katika nchi yetu na kuwavutia wawekezaji na ninamuamini sana huyu Dada Kairuki atatusaidia katika suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine tukija katika masuala ya mawasiliano, mimi nashukuru kwamba terminal III imemalizika kwa 95 percent, niishukuru sana Serikali, lakini kuna changamoto mbili, tatu katika uwanja wa ndege ambao sasa hivi tunatumia terminal II. Utakuta wale ma-porters ambao wanasaidia abiria ambao wanakuja nchini, hakuna hata porter mmoja ambao yupo uwanja wa ndege wote wameondolewa. Sasa nauliza kwamba watu wazima ambao ni walemavu au watu wazima watawezaje kuchukua mabegi yao kuchukua kwenye ile belt kutia kwenye trolley na kupeleka nje? Hii kidogo inaleta picha mbaya sana katika Uwanja wetu wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere ambao sisi tunatumia terminal II lakini tusijetukafanya makosa haya ambapo tunakwenda katika terminal III ambayo tunataka kuiboresha zaidi ili kuvutia watalii ambao watakuja nchini kutumia uwanja wa ndege wetu huu mpya ambao umekamilika kwa asilimia 95. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine nilikuwa nataka wenzetu hawa wa ATC wajipange vizuri kwa sababu ushindani umekuwa mkubwa na wasipojipanga vizuri watakuja kuwa katika hali ngumu kutokana na haya mambo ya ndege inatakiwa mkakati maalum wa kupanga programs kwamba ndege ziende sehemu gani ili mapato ya nchi yaongezeke na kuinua Shirika la Ndege ya ATC.

Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa lingine lipo katika Halmashauri zetu hapa nchini, Halmashauri nyingi sana katika mikoa mingi sana hazikufanya vizuri katika asilimia 10 ya vijana, akinamama na walemavu. Kuna Halmashauri nyingine katika hizo asilimia 10 ya hizi pesa wanazipangia kuzitumia kwa kazi nyingine ambapo hizi asilimia 10 tumepitisha katika Bunge hili tukufu kwamba zinakwenda kwa vijana, akinamama na walemavu, sasa Halmashauri nyingi sana hazikufanya vizuri, lakini tunaomba Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi watusaidie kuhusu masuala haya ya asilimia 10 ili hii itakuwa ni changamoto kwa vijana, akinamama na walemavu katika nchi hii.

Mheshimiwa Spika, nikija katika masuala ya madini, mimi nimshukuru Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli katika kukutana na wadau wa madini ambao kwa kweli ameyatatua matatizo mengi sana. Lakini pamoja na kwamba Serikali imeweka mkakati maalum wa kuuza hizi dhahabu kwa kutumia utaratibu utakaotambulika, lakini bado madini yanasafirishwa nje kwa njia za panya. Bado dhahabu zetu, Tanzanite zetu zinasafirishwa nchi za nje kwa kutumia njia za panya.

Nilikuwa naomba sana wahusika ambao wapo katika boarders zetu wawe wanalifanyiakazi hili na mimi nitakaa na Mheshimiwa Waziri wa Madini ili nimpe changamoto ambapo mimi nafahamu vipi haya madini yanasafirishwa, kwa sababu tukiachia madini yasafirishwe, Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakosa mapato mengi sana na sisi tuna kazi kubwa sana ya kuwapelekea maendeleo wananchi wetu ambao wengi ni wanyonge na wanategemea hizi pesa za maendeleo zifike katika shughuli za maendeleo katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, mwisho katika kumalizia kwangu, katika kuwasaidia wafanyabiashara ambao wanataka kufanya biashara ambapo hiyo inaongeza changamoto, inaongeza mapato katika Halmashauri zetu, wenzetu wa TFDA na TBS kwa kweli wamekuwa na urasimu mkubwa sana, inavunja moyo. Mtu anataka kuanzisha biashara ya kuleta maziwa au kuleta dawa ya mbu, miezi mitano hajapata report kwamba anafaa kuruhisiwa kuleta au haruhusiwi. Sasa kwa kipindi cha miezi mitano inakuwa Serikali kwanza inakosa mapato ya ndani, Halmashauri inakosa mapato. Kwa hiyo, wenzetu wengine wanataka kama kumuhujmu huyu Mheshimiwa Rais ambaye kwa kweli mimi siwezi kueleza mfano wake kwa kazi anayoifanya, anaifanya kazi kwa imani kubwa sana Mheshimiwa Rais na anataka nchi hii iendelee, isonge mbele lakini kuna watu makusudi wanamkwamisha.

Mheshimiwa Spika, kuna watu wanakuwa wanamkwwmisha Mheshimiwa Rais lakini watajibu kwa Mwenyezi Mungu wanajua wao. Lakini mimi naomba TFDA na TBS msiwakwaze wafanyabiashara ambao wana nia ya kuleta mali kuuza Tanzania. Hakuna urasimu wa miezi mitano, miezi sita sijawahi hata kuona katika nchi nyingine ambazo nimetembelea mimi sijapata kuona urasimu huo naona hapa tu Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa haya machache, nichukue fursa nyingine ya kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri sana iliyojaa matumaini ya Watanzania na sisi In Shaa Allah Wabunge tutafanyanae kazi Mheshimiwa Wazitoi Mkuu kumsaidia kuona kwamba hii bajeti yake inapita na tunakwenda mbele mwaka 2020 na vilevile kumsaidia Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ili kazi ya mwaka 2020 kushika hatamu Tanzania iwe kazi rahisi kwetu sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa haya machache, nichukue fursa hii vilevile niwapongeze Mawaziri wote ambao wako chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, niwapongeze kwa jitihada zao wanazofanya na Mungu atawasaidia, lakini haya niliyoyazungumza nimeona bora nitoe changamoto hii ili tupate kusogea mbele siyo katika kumlaumu mtu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa haya machache nakushukuru sana, ahsante sana, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)