Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kukumshukuru Mungu kwamba nimeweza kusimama katika Bunge lako Tukufu ili niweze kuchangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambayo ipo mbele yetu. Naomba nikushukuru na wewe kwa kunipa nafasi ya kuchangia, lakini nimshukuru sana na nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu, ametoa hotuba nzuri iliyosheheni miradi mingi ya maendeleo, iliyofanywa na Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli ukianza kusema kazi zilizofanywa na Awamu ya Tano utamaliza siku tatu unazungumza tu. Kwa hiyo, niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano, nampongeza Rais na Mawaziri wote na Wakuu wa Mikoa, nchi inasonga mbele. Naona kila mtu ana mtazamo wake katika mambo. Baada ya Rais kufanya mambo mengi sana, kuna jambo sasa hivi ameamua kama mnaangalia mambo vizuri, ameamua kuweka misisitizo kwenye uwekezaji. Kwa nini nasema hivyo? Mheshimiwa Rais ameangalia vizuri akaona uwekezaji ndani ya nchi haujakaa vizuri, akaamua kuteua Waziri wa Uwekezaji, Mheshimiwa Angella Kairuki ambaye mimi namwamini sana, amempa Wizara hii na ameiweka chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwa nini ameweka msisitizo kwenye Wizara hii ya uwezekezaji? Dira ya nchi yetu ni kwamba ifikapo 2025 tuwe tumefikia kuwa kwenye Taifa ambalo ni la uchumi wa kati, lakini tuliangalie Taifa la uchumi wa kati na tulipo. Ili tufikie kwenye uchumi wa kati, tunahitaji tuboreshe viwanda kwenye nchi yetu, lakini viwanda tutaviboreshaje, lazima tusimame imara kwenye uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, ili Rais asisitize zaidi katika uwekezaji amewaita Mabalozi wote Ikulu akafanya dhifa, akala nao chakula, lakini akatoa tamko kwa wale ambao mnasomasoma magazeti, kwamba ni mwaka 2019 ni mwaka wa uwekezaji. Mheshimiwa Rais alizungumza kwa wale Mabalozi, lengo lake ni kwamba Mabalozi wote wachukue tamko lile kwenye nchi zao kwamba Tanzania imeamua mwaka 2019 ni wa uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, naomba dakika zangu zote nichangie kwenye uwekezaji. Mimi ni Mwalimu ndugu zangu na Walimu tunaamini unafanya vizuri ukisimamia specialization. Nisingependa kuzungumza mambo mengi sana nitazungumzia uwekezaji na nitachangia kwa maandishi pia nikizungumzia uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, naifahamu nchi yangu vizuri na nimekuwa Bungeni hapa kwa muda wa kutosha. Tumezungumza sana kuhusu pamba na naomba Waheshimiwa Wabunge wanaolima pamba mnisikilize kidogo. Tumezungumza sana kuhusu zao letu la pamba, lakini nikiri bado hatajatumia pamba vizuri kwenye nchi hii. Kuna mikoa minne mikubwa inayolima pamba, Mkoa wa kwanza Simiyu, Mkoa wa pili Shinyanga, Mkoa wa Tatu ni Mwanza pamoja na Geita na wengine wanajaribu jaribu, lakini hii ndio mikoa minne inayolima pamba vizuri. Ukiangalia Mkoa wa Simiyu ukisoma vizuri utaona, Simiyu pekee inalima zaidi ya 40% ya pamba inayolimwa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, hapa nimezungumzia pamba ndani ya nchi, twende kwenye zao la pamba Tanzania katika Afrika na pia twende kimataifa. Tanzania katika kilimo cha pamba ni namba nane, inachukua nafasi ya nane katika nchi 30 za Afrika zinazolima pamba. Hiyo ni upande wa Afika, lakini Tanzania katika kulima pamba Tanzania inashika nafasi ya 22 duniani katika nchi 77 zinazolima pamba. Kwa hiyo, tunaweza Watanzania tukajipambanua kwamba tunalima pamba. Kama dunia nzima nchi zinazolima pamba zipo 77, Tanzania tunashikika nafasi ya 22; kama Afrika zipo nchi 30, Tanzania tunashika nafasi ya nane Waheshimiwa hatulimi pamba? Tunalima pamba.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kama Mbunge mzoefu kusema bado hatujatumia zao za pamba vizuri. Nilipomsikia Mheshimiwa Rais ametangaza 2019 ni mwaka wa uwekezaji, naomba Serikali waende wakajitikite kwenye kuwekeza kwa kutumia zao la pamba, kwa nini nasema hivi? Kwa sababu kuna nchi ndogo hapa Asia inatiwa Bangladesh, mnaifahamu, Bangladeshi hana umaarufu katika kulima pamba hata kidogo, soma vitabu vyote hana, lakini Bangladesh anaongoza kwa kuwa na textile Industry, anaongoza kutuvisha watu wote duniani. Mmarekani anauza nguo sana duniani, lakini viwanda vyote vipo huko Vietnam. Bangladesh ni namba one, anatumia pamba ya ku-export, sasa sisi tuko namba 22 duniani, tuko namba nane Afrika, tuna uwezo wa kufanya vizuri kama Bangladesh na kumzidi. Hivyo, ni lazima Serikali na Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji aende akamsaidie Mheshimiwa Rais, hakumchagua kwa sababu nyingine, amemwamini. Uwekezaji ndio utakaotupeleka kufika kwenye Taifa uchumi kati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu katika uwekezaji iwapo Serikali wata-invite mataifa mengi kuja kuwekeza katika textile Industry, tutafika mbali, tutakuwa kileleni, tutafika mbali, nina imani kabisa. Naona vibaya kweli kale kanchi ka Bangladesh hakana umaarufu lakini kila nguo unayonunua Marekani made in Bangladesh, Bangladesh, Bangladesh, hawana umaarufu ni kanchi kadogo kenye takribani square mita laki moja hamsini elfu, kitu kama hicho, lakini kanaongoza duniani kwa kutuvisha mavazi ni number one akifuatiwa na China.

Mheshimiwa Spika, niinyenyekee Serikali, sasa ni wakati wa kusimamia uwekezaji, Mheshimiwa Rais amefanya vizuri sana tangu ameanza, jamani kuna ambaye hawatakubali? Rais anafanya kazi nyingi sana, sasa namwomba Mheshimiwa Rais kwa unyenyekevu mkubwa, nampigia na magoti, aipeleke nguvu yake kwenye uwekezaji na uwekezaji huo aende akaitumie pamba ya nchi hii, tutumie pamba ya nchi hii, tutafika mbali sana.

Mheshimiwa Spika, nisingependa kusema sana kwa sababu nataka kusimama kwenye pamba na Mheshimiwa Waziri naomba niseme nachangia nitampelekea faili lenye data akamsaidie Mheshimiwa Rais kazi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono haja na nakushukuru sana. (Makofi)