Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU SHAURI LA KUDHARAU NA KUDHALILISHA BUNGE LINALOMKABILI NDUGU PROF. MUSSA ASSAD, MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI

Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU SHAURI LA KUDHARAU NA KUDHALILISHA BUNGE LINALOMKABILI NDUGU PROF. MUSSA ASSAD, MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI

MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru ninaomba niweze kujibu kidogo baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na Mheshimiwa Catherine Magige yeye aliongelea suala la uzalendo. Ni kweli, duniani kote uzalendo kwanza. Nashukuru ameunga mkono Kamati, lakini naomba niende kwenye hoja za Mheshimiwa Mbowe ambaye alianza kwa kusema kwamba Azimio lilikuwa limefanyiwa maamuzi kabla.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii siyo kweli kwa sababu Mheshimiwa Mbowe kwanza ni Mjumbe katika Kamati ya Uongozi na wakati tunajadili ratiba ya kwanza alikuwepo na hata hii ya pili, pamoja na kwamba hii ya pili alichelewa amekuta ndiyo kwanza imeisha, lakini alifika. Ni kwamba hoja hiyo ililetwa kwenye Kamati yetu na Kamati ile wamo pia wa Vyama vya Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbowe anapoongelea composition, uwiano wa wale Wajumbe wanaoingia kwenye Kamati ya Maadili, huu uwiano umewekwa kwa taratibu na kanuni za Kibunge. Pia tusije tukawa tunajisahau, Chama cha Mapinduzi ndiyo chenye Wabunge wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tusipoangalia hoja nyingine zinazotolewa kwa mtu wa kawaida anayesikiliza anaweza akadhani kwamba hizi Kamati zinapangwa tu. Hizi Kamati zinapangwa kwa uwiano wa Wabunge. Kwa hiyo, siyo rahisi na sioni kama mnaelekea huko, labda kama mnaweza nanyi mkawa na Wabunge wengi kama Chama cha Mapinduzi, pengine uwiano huo utakuwa sawa, lakini kwa hapa ilipo ndiyo kanuni zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Mheshimiwa Mbowe anaposema Kamati ile inakuwa haitendi haki, siyo kweli. Mheshimiwa Mbowe alikidhalilisha kiti pamoja na Bunge na aliitwa kwenye Kamati ya Maadili na Madaraka ya Bunge. Baada ya kumsikiliza hoja zake na kuomba msamaha tulimsamehe. Sasa leo Mheshimiwa Mbowe kama anamtetea Mheshimiwa Profesa Assad ambaye hakuomba hata msamaha na pamoja na kwamba aliambiwa maana ya udhaifu, neno “dhaifu” kwa mtu wa kawaida anavyoweza kulichukulia, bado hakuomba msamaha, anamtetea, hii haijakaa sawa sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, la Mheshimiwa Hassan anasema no one is perfect. Ni kweli, hata Mheshimiwa Profesa Assad sio perfect katika kila jambo. Nashukuru katika hili umetuunga mkono. Sisi tuliliona hilo, lakini unapokuwa ni kiongozi ambaye unaaminiwa na Taifa, hata hayo Mataifa makubwa tunayoyasema ambayo tunayatolea mfano, yamekuwa hayakubali mtu kutoa taarifa za nchi yake nje ya nchi. Mfano ni Wamarekani, wanamtafuta mtu mmoja kama sikosei anaitwa Slowden na bado hajaropoka chochote, lakini wana wasiwasi kwamba kuna taarifa mbalimbali za nchi anazijua, wanamtafuta wamkamate wakati wowote.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine uhuru aliouzungumzia Mheshimiwa Mbowe, ni kweli anapozungumza kwamba Ibara ya 18 ya Katiba imetoa huo uhuru anaouzungumza yeye, mimi nilidhani angeenda akasoma pia na mipaka ya uhuru huo, kwa sababu Waheshimiwa Wabunge hakuna uhuru wowote ambao ni timilifu. Uhuru wowote unaopewa, not absolute, siyo timilifu. Kuna mipaka imewekwa kwenye Katiba hiyo hiyo, Ibara ya 30 kila uhuru una mipaka yake. Sasa mtu akivuka mipaka hiyo, ndio mambo kama haya ya Mheshimiwa Profesa Assad yanatokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Vuma amem-quote Mwalimu, Baba wa Taifa kwamba amewahi kusema, uhuru bila nidhamu unakuwa kama ni wazimu. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wajumbe, kila jambo na hasa jambo ambalo linahusiana na uhuru wa chombo kingine, kuna mipaka yake; Bunge, Mahakama lakini pia na Executive. Hizi kanuni tumejiwekea wenyewe, anayezivunja, ndio ataletwa kwenye Kamati ya Maadili. Siyo kila mmoja anayeletwa kwenye Kamati ya Maadili anapewa adhabu. Kwa hiyo, maneno ya Mheshimiwa Mbowe siyo ya kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine Mheshimiwa tunayemwongelea hapa, Mheshimiwa Profesa Assad alikuwa na nafasi ya kuzungumza yale ambayo alizungumza nje, alikuwa na nafasi ya kuja kuyazungumza hapa kwa sababu anahudhuria vikao vya Kamati zetu mbili. Anayo sehemu ya kuyasemea hayo, lakini siko alikosemea. Anayo nafasi ya kuyasemea, kwa hiyo, uhuru wake aliutumia vibaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Mbowe alisema kikao cha ambacho kimekaa Kamati ya Maadili ni kama kikao cha Chama cha Mapinduzi. Hii siyo kweli, kwa sababu kama nilivyosema mwanzo, wamo pia Wajumbe wa Kamati ambao wanatoka Vyama vya Upinzani.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo yangu, naomba sasa Bunge likubali taarifa pamoja na Azimio.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. DKT. CHRISTINA G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.