Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia. Kwanza kabisa naunga mkono taarifa za Kamati zote mbili. Pili, nimpongeze sana Mheshimiwa Profesa Kabudi kwa uchapaji kazi na usimamizi wake wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya wanaotambua na kuthamini kazi anazofanya na Geita nadhani ni namba moja. Ukiangalia Geita ya leo na Geita ya mwaka mmoja tu uliopita kabla ya yeye kuamua kutekeleza sheria na kuisimamia ni vitu viwili tofauti. Wengine hata tukiona wanavyomshambulia, tunaumia sana, lakini tunaomba aendelee kukaza buti kwa sababu msimamo wake ndiyo unaofanya hawa watu wapige kelele humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, sisi tunaotoka vijijini tunaishukuru sana Serikali pamoja na Wizara. Mheshimiwa Kabudi, Mahakama inayotembea ni suluhisho kubwa sana kwa watu wa vijijini. Ukienda Jimbo la Geita Vijijini lenye watu takribani 600,000 lina Mahakama moja tu ya Mwanzo na yenyewe inapatikana pengine kilometa 150 ndiyo unaiona Mahakama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaishukuru sana Serikali. Ombi letu ni kwamba sasa Mheshimiwa Kabudi tumeona mmezindua juzi, tunatarajia baada ya muda mfupi, tutayaona haya magari yanakuja huko vijijini kuanza kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nilishauri Bunge lililopita kwamba makosa mengi, ukienda kwenye Magereza kuna mlundikano wa wafungwa na mahabusu lakini watu wengine wana makosa tu ya kuiba kuku. Watu wengine wana makosa ya kukamatwa uzururaji, hata faini yake pengine inakuwa shilingi 100,000/= lakini ameshakula ugali zaidi miaka miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Kabudi kwa uchapaji wake kazi hebu aangalie namna anavyoweza kufanya, makosa mengine tuwe tunamalizana nayo hata kwa viboko watu waendelee kuchapa kazi huko mitaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, sisi Wabunge ndio tunaotunga sheria. Pamoja na minyukano inayokuwa humu ndani, lakini sisi ndio tunaotunga sheria. Kwa hiyo, sheria inapotekelezwa, tusidhani tunapopitisha sheria, tunapitishia mbwa; tunapitishia binadamu tukiwemo na Wabunge. Kwa hiyo sometimes sheria inapotulenga sisi, lazima tukubali kutii sheria bila shuruti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikia watu wengi wanasema; na bahati mbaya rafiki zetu wakizungumza, wanawahi Canteen hawamo humu ndani. Amezungumza Mheshimiwa Lema hapa, anasema alitekwa Makuyuni. Hivi mtu anatekwa halafu anapelekwa Kituo cha Polisi? Hicho ni kitu cha uhuni. Mimi mwenyewe nilikamatwa, siwezi kusema nilitekwa. Unakamatwa, unapelekwa Kituoni, unamaliza shida zako, unaachiwa. Ndiyo maana leo Mheshimiwa Lema yumo humu Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitoa mwongozo wangu jana kwa Mheshimiwa Spika kuhusiana na suala la Mheshimiwa Tundu Lissu. Nimeona mitandaoni wananitukana, wananichamba, lakini sishangai. Bahati nzuri wengine tunaongea nao huko. Hili suala nililolizungumza jana kuna watu wanalifurahia kwa sababu michango inawaua na hawana kitu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili naomba nizungumze, katika Bunge hili hakuna mtu ambaye hatarajii kuugua; hata sisi, hata yeyote. Tunatambua kabisa kwamba Mheshimiwa Tundu Lissu alipata matatizo. Wengine tunaomba kimya kimya, siyo lazima wote tupayuke kama nyie. Tumekuja kushtuka, mtu tunayemwombea ni mcheza sinema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi toka nimekuwa Bungeni hapa, hatujawahi kukaa Bungeni zaidi ya masaa matano tuna-break, tunarudi masaa matano, tunaahirisha Bunge. Naomba niwaambie kwa sababu tunazunguka zunguka na sisi ni wazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua kutoka alikokuwa anatibiwa Mheshimiwa Tundu Lissu, ziara yake ya kwanza ameenda Uingereza. Kutoka Ubelgiji kwenda Uingereza ni masaa manne kwenye Ndege. Huyo ni mgonjwa. Kutoka Uingereza kwenda Marekani ni masaa 10 mpaka 11, huyo ni mgonjwa. Haya, kutoka Marekani kwenda Ujerumani, ni zaidi ya masaa 14, huyu mtu anaitwa mgonjwa, haiwezekani. Hili lazima tuungane mkono. Nanyi mnaomtetea, nataka niwaambie ukweli, pamoja na ….

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nilichokuwa nakisema; na wenzangu Waheshimiwa Wabunge na wananchi wa Singida Mashariki walichagua Mbunge na wao ni wamoja wa watu ambao wanamwombea Mbunge wao apone, hawakuchagua mtu wa kula bata, wanayemwona kwenye TV na magazeti kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokisema hapa, sheria tulizitunga wenyewe. Nashangaa sana na Bunge lako, kwa nini hatutekelezi matakwa ya kanuni? Kama mtu amepona anaweza kusafiri masaa yote na kukaa kwenye hotuba kutukana Taifa...

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ndugu yangu Mheshimiwa Mwakajoka, najua wewe Timu Tundu Lissu, unadhani anakuona ili akupitishe jina. Ninakuomba utulie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasema, wananchi wa Singida Mashariki hawana mwakilishi; na sheria inatutaka mtu akiwa mzima, asipohudhuria vikao vitatu, kuna hatua ya kuchukua na mliitunga wenyewe, inasubiri kutekelezwa wakati gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wasichukue point hapa. Humu humu ndani tunao Wabunge wenzetu wanaumwa, wala hamna mtu anawajadili. Tunaye Mheshimiwa Mkono…

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ninachokisema hapa, ni vizuri Mheshimiwa Spika akachukua hatua ya kuweza kutengua uteuzi wake ili wananchi wa Singida Mashariki waweze kupata mwakilishi wasiwe na mwakilishi anayewawakilisha kwenye TV.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri, tunao watu wanaumwa hapa, lakini kwa sababu wananchi wao wamewatuma kufanya kazi, tunaye Mbunge wa Singida Magharibi hapa Manyoni, ni mgonjwa, anakuja na gongo lake humu ndani; tunaye Mheshimiwa Ridhiwani, tunao watu kibao. Hhaiwezekani mtu anayeweza kukaa kwenye ndege masaa 14 halafu akaachwa tukaendelea kumwona anakula mshanara. Watanzania wanatupima na wanatuona.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)