Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nianze kwanza kwa kuzishukuru Kamati zote mbili, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Kamati ya Kudumu ya Sheria Ndogo. Vilevile niwapongeze Wajumbe wa Kamati hizo na Mawaziri walioshughulika na Kamati hizo kusaidia kufanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa natazama vitu katika Kamati hizi na nimeona kuna jambo nataka nilizungumze la Kamati Ndogo kuhusu kile kipengele cha Kodi ya Majengo. Kipengele hiki cha kodi ya majengo wakati kinatekelezwa katika maeneo yetu kimekuwa na vitisho vingi sana. Kwa hiyo, naomba wakati wanafanya ufuatiliaji wa kipengele waangalie kwa sababu huko vijijini kuna nyumba za nyasi na nyumba za bati, ilifika wakati ukijenga nyumba ya bati unadaiwa kodi, ikaonekana kama ni Kodi ya Kichwa hivi. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie vizuri kwenye kodi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili Taifa ni letu wote na kama kuna watu wana ndoto kwamba nchi hii ni ya Rais John Pombe Magufuli na chama chake na wako tayari kuiharibu kwa wakati wowote wanavyotaka kwa maslahi yao watakuwa wamekosea sana. Hotuba nyingi zinazokuja hapa hata ya ndugu yangu hapa Mheshimiwa Kubenea anauliza habari ya ma-DED kwamba ni makada wa CCM, lakini hapa tuna Wabunge zaidi ya 100 kwenye uchaguzi uliopita na wametangazwa na ma--DED hao wanaosema ma-DED wa CCM. Sasa DED amemtangaza kuwa ameshinda, amekuja Bungeni halafu anamsema ni mbaya, sielewi kinachoendelea huko mbele katika mambo kama hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi yanazungumzwa hapa. Nilikuwa natazama sana wakati Rais wa United State, Trump, alivyo-tweet juu ya White House, kuhusu ya Wazungu wale weupe wa South Africa kwamba anataka kuwalinda wale Wazungu kwa maana ya ardhi ya South Africa. Nikamtazama Julius Malema, nikamtazama Ramaphosa ambaye ni Rais, wote walikusanyika pamoja kutetea ardhi ya South Africa bila kujali upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimuona Malema alienda mbali zaidi anawaandaa wanachama wake anawaambia tuko tayari kufa kwa ajili ya ardhi yetu, hatuko tayari kutoa ardhi yetu kwa sababu ya umasikini wetu au kwa sababu hatuna uwezo wa kufanya jambo hili. Huyu ni mpinzani wa South Africa lakini nchi yetu leo hata tungezungumzia habari ya kugeuzwa kuwa wanawake tayari watu wanatetea. Mimi sielewi kama katika nchi hii hali ya hewa inavyoenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanazungumza democracy lakini wanashindwa kutofautisha democracy and futures of democracy…

KUHUSU UTARATIBU

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa heshima ya Paroko nafuta hilo neno, tunaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine wakati fulani unaweza ukaongea hata ukachanganyikiwa kwa sababu leo kama tuna watu ambao ni Watanzania wanaodhani kwamba Rais au utawala wa nchi hii ambao tuliupata bila kumwaga damu na kuna watu walihangaika kuupata kwa kuzunguka tukapata uhuru, leo ni mwaka wa 48, wanadhani kwamba nchi za Ulaya, za Mabeberu wanaweza kuamrisha Watanzania wakampa mtu Urais kwa kupitia nchi za Ulaya, haya ni mambo ya ajabu na ya aibu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais aliyekuwa maarufu sana hapa duniani na Afrika, Nelson Mandela, alifungwa miaka 27. Alipotoka jela wala hakwenda Ulaya kutafuta Urais, alikaa kule kwake na wala alipotoka jela wala hakutafuta nani alimweka jela. Alikaa kwenye nchi yake akawaambia uhuru tunautafuta na uhuru akapewa na Wazungu waliomweka ndani miaka 27 akaishi nao, ni historia kubwa sana katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna mtu akikosewa dakika mbili, dakika tatu, imekuwa matatizo. Leo tuna Rais bora kabisa katika nchi za Afrika, ameandikwa humu ndani ukisoma, ana miaka mitatu lakini ameandikwa anafanya vizuri. Leo nchi yetu ni ya 10 kwenda kwenye uchumi bora katika nchi za Kiafrika. Sasa leo wanapita tu wanachafua nchi yetu ambayo ni yai letu la kulea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wale wote ambao wana mawazo hayo warudi tufanye kazi ya ndani wasichanganye demokrasia na utekelezaji wa demokrasia. Kama kuna utekelezaji mtu anazungumza ni watu wanafungwa na kesi zinacheleweshwa, mmeona juzi Mheshimiwa Rais ameteua Majaji na anaendelea kuteua ili mambo ya kesi yaende vizuri na mambo mengine pia tunaendelea kuyatendea haki, mfano, uchaguzi tumechagua vizuri na tunaendelea kuchagua. Tunapozungumzia demokrasia maana yake nchi yetu inatekeleza demokrasia. Tumechagua Wenyeviti wa Vitongoji, Wenyeviti wa Vijiji, Madiwani, Wabunge na Rais hiyo yote ni demokrasia, sasa demokrasia inayozungumzwa ni ipi, mimi sielewi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wasilete hofu kwamba utendaji mzuri wa Mhesimiwa Dkt. Magufuli watakosa vyeo, ukikosa cheo ni Mungu ameamua, siyo wewe sasa. Mungu akisema wewe huwezi kuwa Mbunge huwezi kuwa Mbunge. Kwa hiyo, tukubali kwamba nchi ni yetu tumsaidie Rais afanye kazi vizuri ili tuendelee kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, chama ni chenu na Ilani ya Uchaguzi inayotekelezwa ni yenu, tufanye kila namna tumsaidie Rais afanye kazi yake vizuri. Pale ambapo tunahitaji kumshauri, tumshauri vizuri, pale tunapotakiwa kutenda, tutende vizuri. Tukianza kuwa tofauti maana yake ni kwamba chama chetu kinakwenda kufa, kwa sababu aliye na dhamana ya kusimamia Chama cha Mapinduzi kwa sasa ni Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Huyo ndiye mchezaji wetu wa Chama cha Mapinduzi, tukimyumbisha wakamkanyaga mguu ukavunjika maana yake chama chetu kinaenda kupata matatizo, kwa hiyo, lazima tumlinde kwa heshima zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhuru tumeupata, nchi yetu ipo, ina miaka 48 na ina sifa, ni nchi pekee duniani yenye Muungano. Nataka niwakumbushe watu, tusipokuwa watetezi wa mambo mazuri tuliyoyafanya, kama mwaka 1995 Muungano wetu ulivyotaka kuyumba, asingesimama imara Rais wa Awamu ya Kwanza Mwalimu Julius Nyerere, akaita Bunge na Halmashauri Kuu ya CCM na tukakubali kuendelea na Muungano leo Muungano usingekuwepo. Kama hatuwezi kuungana kutetea nchi yetu maana yake wote tunaweza kwenda kwenye matatizo. Nchi yetu ni ya amani na watu wetu hawakuzoea mabomu na timbwilitibwili nyingi, kwa hiyo, tunaomba watu wawe na amani na tuombeane amani ili tuweze kuishi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)