Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Godbless Jonathan Lema

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nafurahi kwamba leo Bunge lina utulivu wa kutosha na taarifa na miongozo pengine jana mlijadili mkasema haina maana sana. Jana nilikuwa natafakari sana, kwamba ndani ya Bunge hili Wabunge wote tuliopo sasa tukapewa fursa na Mwenyezi Mungu ya kuishi miaka 30 inayokuja mimi nitakuwa na miaka 72, wewe utakuwa na takribani miaka 100, pengine Mheshimiwa Jenista atakuwa na miaka mingi zaidi. Maana yake ni kwamba hata kama tutakuwa hai wengine watakuwa hawana nguvu kabisa za kulitumikia Taifa hili. Thamani yetu leo si kulinda Chama Tawala ni kulinda misingi ya haki katika Taifa na ndio wajibu wa kwanza wa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiishi kula leo, kuvaa leo, kuendesha gari leo, halafu usitafakari maisha ya wajukuu wako, ya vitukuu vyako baada ya maisha yako hapa duniani, si tu utakuwa ni Mbunge mkatili, utakuwa ni mzazi mkatilii. Kama kuna kitu tunapaswa kukichunga Wabunge wote bila kuangalia itikadi yetu ni juu ya namna gani tunalisaidia Taifa kuheshimu Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ndio msingi tuliokubaliana kwamba kwa sasa tutaishi kwa madhumuni haya na kwa utaratibu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yoyote duniani, iwe ni Marekani, iwe ni Venezuela, iwe ni Kenya, ikianza kuishi nje ya utaratibu wa Katiba na sharia, Serikali hiyo inakuwa ni kikundi cha wahuni ila wamevaa suti, yoyote duniani. Namna pekee ya kuthibitisha umahiri wa Maprofesa, Madaktari, form four na watu wote wenye hekima, namna pekee ya kuthibitisha umahiri ni kuishinda hofu linapokuja suala muhimu la haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtoto wangu mimi na mjukuu wangu mimi natarajia siku moja akutane na Mahakama huru hata kama nitakuwa sipo, same to mtoto wa Mheshimiwa Jenista, same to mtoto wako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunapoona haki inachezewa, lakini inachezewa kwa kwa sababu inatupa fever ni sawa sawa na chloroquine imepakwa chocolate, utaila kwa muda utasikia radha ya chocolate baadaye utakutana na uchungu. Hakuna uovu ambao hautalipwa ni nature, ni karma. Kuna mambo leo yanawatokea watu wa CCM ambao huko nyuma walikuwa untouchable.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikutana na Manji siku moja Karimjee, nikamwambia kwamba kuna kipindi wewe ulikuwa untouchable. Leo kuna watu walikuwa hawaguswi katika katika Serikali hii, walikuwa ni wafanyabiashara wakubwa, walikuwa ni viongozi wakubwa, leo wako magereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna utawala unaoweza uka-guarantee usalama wa mtu isipokuwa haki, kwa sababu haki haina tu kipaumbele cha system ina kipaumbele cha Mwenyezi Mungu peke yake. Waheshimiwa Wabunge tunapokaa hapa Bungeni kujadili mambo ya msingi; jana nimeshangaa; kwamba suala la mkono wa sweta (govi) linaweza likatolewa na Bunge na TV ya Bunge likapelekwa mitaani halafu masuala mengine ya msingi ya kusaidia nchi kama vile michango ya Wabunge wa Upinzani inanyimwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, michango yetu siyo uhaini…

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawasaidia, leo tunaongea michango yetu si uhaini, michango yetu…

T A A R I F A

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea hiyo taarifa. Hiyo ni sehemu ya mfano wa jambo hilo, lakini yako mambo mengi, kwamba leo mawazo yetu ndani ya Bunge si mawazo ya kuiangusha CCM. Mimi leo mkitawala kwa haki, kwa upendo, kwa sheria na mkafuata Katiba, hata mkitawala milele sitakuwa na tatizo. Lengo letu si kuwatoa ninyi madarakani, lengo letu ni kuona ninyi mnatutawala kwa haki na ndiyo maana ya upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo chuki inajengwa, leo kiongozi mmoja m-NEC wa Chama cha Mapinduzi anahutubia anasema Mheshimiwa Lissu siku akitua ashambuliwe, Mheshimiwa Zitto ashambuliwe, leo Mheshimiwa Zitto yuko Bungeni, tumemwondoa juzi, Mheshimiwa Zitto juzi alikuwa anafuatiliwa usiku kwa kazi za Kibunge si za kuuliza madawa la kulevya, si za kubaka mtoto, kwa kazi za Kibunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilitekwa Makuyuni kwa kazi ya Kibunge, wakaua mtu mmoja polisi, kwamba wale ni watu waliokuwa wanakuja kuniteka mimi. Nikapelekwa jela kwenye ile kesi yangu dhidi ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli. Nikiwa jela wale vijana wakaletwa jela, wakapelekwa dispensary nikajifanya naumwa nikapelekwa dispensary nikaanza kuongea nao. Cha ajabu wale vijana waliokuwa jela walitolewa jela siku ya Jumapili na Mbunge, Mheshimiwa Jitu alikuja kuwachukua na gari siku ya Jumapili ambapo Mahakama wala Magereza haifanyi kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya mambo yanafanya tulipwe machozi, tunaguna, siyo mimi peke yangu ninayeguna, tumesikia juzi hapa Itigi, Mkurugenzi ameua, ameingia ndani ya Kanisa la Sabato, ame-shoot, mzazi anasema ame-shoot, Mkurugenzi akasema ilikuwa ni kwa bahati mbaya. Tunaona taarifa ya polisi leo inasema Mkurugenzi yule hakuua, walioua ni Polisi wa Wanyamapori waliokuwa nje.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya maneno tunaongea hapa kwanza hili suala haliko Mahakamani; lakini siku Bunge hili likafikiri hata jambo lililoko Mahakamani lakini lina mashaka ya damu ya mtu, Bunge hili haliwezi kulijadili tunainajisi legitimacy yetu kama Wabunge. Waheshimiwa Wabunge thamani ya mtu mmoja ni zaidi ya kilometa 10, 000 za lami, thamani ya mtu mmoja, hata kama ni kichaa, ni zaidi ya SGR ya kutoka Tanzania kupita nchi zote za SADC. Kazi ya kwanza ya serikali yoyote duniani ni ku-protect human rights. Kama huu si msingi wetu wa imani, kwamba maisha ya mtu mmoja yanaweza yakawa considered na vitu, thamani yetu ya kuishi haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanaendelea kufa, watu wanaendelea kupotea na yote hii ni Katiba. Inawezekana kabisa kuna nia njema ya Serikali, kumsaidia Mheshimiwa Rais kutekeleza majukumu yake ni kumwambia ukweli kwa sababu ukweli ni nguvu. Leo tunavyoongeza kuna watu wanaozea mahabusu. Jamani mimi nikiongea habari ya mahabusu; pasu nimekutaka na Mheshimiwa Profesa Kabudi nimeongea naye; kuna watu wana kesi za money laundering wako mahabusu, Sh.300,000 mtu yuko jela miaka mitano. Kenya leo kila kesi ina dhamana isipokuwa kesi ya uhaini, Uganda leo kila kesi ina dhamana mpaka kesi ya uhaini. Dhamana ni hoja kuu imewekwa kwenye Katiba hii ndiyo Mtobesya. (Makofi)

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lenye Wabunge zaidi ya watu 350, hutarajii kumkosa mtu kama huyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi, mimi napita Magereza zote, kuna kesi inayotumika vibaya, Profesa yuko hapa, ni Mwanasheria. Money Laundering Act; Waheshimiwa sikilizeni tuna miaka miwili kutoka humu ndani, haya mambo ninayowaambia sisemi kwa niaba ya CHADEMA nasema kwa niaba ya watu wote sisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walioko Magereza leo wengi hawakuwa makada wa Chama cha CHADEMA. Concern yangu hapa nini, leo Mahakama ya Kikatiba ilinusa section 148 ya CPA ambacho kilikuwa kinampa mamlaka DPP ya kuweka watu ndani kwa certificates. Mimi nimekaa ndani kwa certificate, watu wengi wakaa ndani. Sasa haya mambo leo yanaonekana ni CHADEMA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili kundi hili linaweza likaamua leo, tunaamua tu leo kwamba hatugombanii ubunge, tu naacha siasa halafu ninyi CCM mjae huko, then what? Halafu nini kifanyike? Yaani assume huku mmejaa, huko mmejaa Mheshimiwa Waziri Mkuu ni wenu, Mheshimiwa Rais wenu halafu then what, then what? Kimsingi ni sheria, kimsingi ni utaratibu. Ndiyo maana tunasema Waheshimiwa Wabunge turudi turudi kwenye sense. Nawaambia, kwa hali ilivyo leo na nisikilizeni mimi ninyi, Mawaziri mlioko kwenye Baraza hili na Makatibu Wakuu, kwa utaratibu wa sasa ninavyouona jiandaeni, la sivyo badilisheni sheria; jiandaeni ninyi na hamtajua. Kwani, Waheshimiwa viongozi, kwani Magufuli ni CHADEMA, Magufuli si CHADEMA, ni purely CCM. Wakati Magufuli anashinda Urais.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Lema, Mheshimiwa Rais utamu-address kwa cheo chake tafadhali.

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani na namheshimu sana. Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Mtukufu Magufuli, siyo CHADEMA ni CCM na watu wote leo wamekuwa responsible na matatizo waliyofanya kwenye kazi zilizopita siyo CHADEMA, wengi ni Makada wa Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema hivi, mtafanya mitimanyongo yote mnayoweza kufanya, mtafanya kila mnachoweza kufanya; tunaweza tusirudi Bungeni tena; mtasema tutamweka mtu wetu Profesa Kabudi huyu, atalinda utawala uliopita. Akina Kikwete walifikiri hivyo hivyo, utawala uliopita haulindwi. Walifikiri hivyo hivyo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema, bado dakika tano. Zangu ni 15.

MWENYEKITI: Ahsante. Tayari Mheshimiwa Lema. Ulianza na dakika sita.