Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Peter Joseph Serukamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. PETER J. SERUKAMBA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa nafasi hii uliyonipa na nawashukuru wachangiaji wote, ripoti yetu imechangiwa na watu 25. Yameongelewa mengi sana, nitajitahidi kuongea yale machache ambayo wameongea watu wengi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la kwanza ambalo Kamati yetu imelisisitiza na Waheshimiwa Wabunge wamelisema ni umuhimu wa Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote. Bado tunaiomba Serikali kama kuna zawadi Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli na Serikali yake tunaweza tukawapa Watanzania ni kuleta Bima ya Afya kwa Watu Wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili ni watumishi wa afya. Tumefanya kazi kubwa sana ya kujenga vituo vya afya na zahanati. Bahati nzuri kaka yangu Mheshimiwa George Mkuchika ametuahidi, ni muhimu sana kupata watumishi wa afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la tatu nataka kuipongeza Serikali kwa dhati kabisa. Serikai imefanya kazi kubwa katika uwekezaji mkubwa hasa Hospitali za Muhimbili, Jakaya Kikwete, Mloganzila, Benjamini Mkapa, MOI na Ocean Road. Pia tumejenga hospitali za mikoa, hospitali za wilaya na vituo vya afya. Kwa vyovyote vile haya ni mafanikio makubwa. Naomba niipongeze Serikali kwa kazi hiyo kubwa wanayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo kama Kamati tunaiomba sana Serikali, umefika wakati tuanze kuhangaika na kinga. Wanasema kinga ni bora kuliko tiba. Tukihangaika na kinga tutapunguza gharama kubwa za afya. Ili tuweze kuhangaika na kinga lazima tuhangaike na watu wanaoitwa Community Health Workers. Hawa ndiyo wako vijijini, wanaishi na wananchi, watatoa elimu, watasaidia kwenye chanjo na wataeleza umuhimu wa usafi. Naomba nieleze tuliyoyaona Rwanda, wao hawa Community Health Workers wamesaidia kupunguza vifo vya akina mama kwa asilimia 80. Kwa hiyo, niiombe Serikali tuhakikishe tunaiangalia kwa makini kada hii na kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la elimu. Tumeandika kwenye ripoti yetu na kila mwaka tumekuwa tunaandika na tutaendelea kuandika. La kwanza, Serikali inafanya vizuri sana kwenye kutoa mikopo ya watoto wanaokwenda vyuo vikuu. Ukiangalia nchi zote zinazotuzunguka wanazo tuzo kwa maana ya scholarship award. Naomba sana Serikali umefika wakati sasa tuanzishe scholarship award.

Mheshimiwa Spika, maana yake ni nini? Scholarship award ni watoto waliomaliza form six waliopata point tatu na point nne. Kama Serikali tuwaoneshe appreciation kwamba tumekubali wamefanya vizuri na watasomeshwa na Serikali. Tunapendekeza scholarship award hii ingeitwa Magufuli Scholarship Award. Hii itaongeza morale shuleni na kwa vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la university classification. Tuna universities nyingi sana, nadhani imefika wakati sasa tuanze ku-classify vyuo vikuu vyetu. Duniani huko universities ziko classified. Ukienda Marekani wanaitwa Ivy League maana yake ukisoma chuo hicho, hata mtu ukimwambia nimesoma Harvard kuna maswali haulizi. Kwa hiyo, nasi tutengeneze Harvard ya Tanzania kwamba labda nimesoma University of Dar es Saalam, kama ndiyo high classified hata mwajiri anasema hapa ni pazuri. Kwa hiyo, naomba tuanze kuona umuhimu wa suala hili.

Mheshimiwa Spika, niipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano imefanya kazi kubwa sana kwenye elimu. Wazungu wanasema access, tumetoa access, watoto wote wa Tanzania wana access kwenye education, watoto wote wa Tanzania wanapata elimu bure. Baada ya hii ya access imekuja na changamoto ambayo itaenda kwenye ubora, vyumba vya madarasa na walimu.

Mheshimiwa Spika, kwa nini nalisema hili? Tulilisema siku za nyuma, najua wengine inawezekana hawajalitafakari vya kutosha, amelisema Mheshimiwa James Mbatia na Waheshimiwa Wabunge wengi wamelisema. Nadhani umefika wakati, baada ya haya mafanikio makubwa tuliyonayo ya elimu hebu tuangalie upya mfumo wetu wa elimu, tujue kama tuna matatizo yako yapi, je, tatizo ni financing, walimu, vitabu, ni mitaala ama ni muda wa kufundisha? Tukifanya hivyo tutakuwa tume-solve tatizo la miaka 50 ijayo kama Taifa.

Mheshimiwa Spika, huwa napenda kutoa mfano, mwaka 1981 Rais Reagan aliangalia hali ya Marekani ilikuwa inadorora kwenye world stage kwenye education wakaanzisha Tume ya Elimu ambayo ilifanya kazi kwa miezi 18 ikaja na ripoti na ripoti hiyo famous, inaitwa ‘A Country at Risk’. Taifa kubwa liliangalia likaona hapana tunakokwenda tutashindwa kuangalia.

Mheshimiwa Spika, sasa na sisi imefika wakati wa kuliangalia suala hili la elimu yetu. Watoto wetu wanamaliza chuo kikuu hebu tu-taste output. Maana wakati unafanya huo uchunguzi wata-taste output, je, lazima watoto wote waende university hakuna tertiary education? Maana tuna tatizo la ajira na tuna watoto wengi wana degree lakini pamoja na tatizo la ajira hatuna mafamasia, mafundi mchundo na wafanyakazi wa hoteli wazuri. Haya yote yatawezekana iwapo tutaunda Tume ya Elimu na kwa kweli itatusaidia sana na tutakuwa tume-solve tatizo la miaka mingi ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la walimu wa hesabu na sayansi, tunarudi hapo hapo. Inawezekana tukasema tatizo letu ni walimu wa hesabu na sayansi lakini inawezekana hilo si tatizo peke yake. Pengine tunasema tatizo ni maslahi ya walimu inawewezekana siyo tatizo peke yake. Tunaishawishi Serikali ione umuhimu wa kuleta Tume ya Elimu ili tuangalie mfumo wetu wote wa elimu kuanzia kindergarten mpaka university tuone kama liko tatizo liko wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumefanya vizuri sana wanasema kwenye hard infrastructure. Tunajenga reli, umeme na barabara; these are the hard infrastructures. Umefika wakati tuwekeze vya kutosha kwenye soft infrastructure ambazo ni pamoja na education. Nchi zote zilizoendelea miaka ya 60 siri yao namba moja ni elimu. Kwa hiyo, niombe sana tulifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la utafiti. Tulikubaliana tupeleke asilimia moja ya GDP. Hata hiyo tunayoipeleka inazidi kupungua. Suala la utafiti ni muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, nimalize kwa mambo mawili. Moja, hapa Bunge wakati tumeanza 2016 tulitunga Sheria ya Vyombo vya Habari. Nimuombe sana Waziri wa Habari, Michezo, ile sheria ilipigiwa kelele sana lakini ilikuwa ni sheria nzuri sana kwa ajili ya kusimamia waandishi wa habari na vyombo vya habari. Tunajua Kanuni zimetungwa na sheria ile ilitaka tutunge vyombo fulani vya kusimamia wandishi wa habari, mpaka leo vyombo vile havijatungwa. Kwa hiyo, niwaombe Serikali wajitahidi watunge vyote vile ili tuanze kusimamia hii kada na tuendeleze weledi katika vyombo vya habari.

Mheshimiwa Spika, mwisho ni michezo. Nimewasikiliza Waheshimiwa Wabunge wengi sana waliozungumzia suala la michezo. Michezo ni ajira. Mwezi Aprili tunakwenda kwenye mashindano ya AFCON lakini tuulizane maswali, timu yetu iko kambini?

WABUNGE FULANI: Hapana.

MHE. PETER J. SERUKAMBA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA
JAMII: Tunawezaje kushinda ikiwa mpaka leo hatujaenda kambini? Michezo iko Aprili leo ni Februari, mnataka tushindane tukiwa tumeanza kambi wiki moja kabla? Ni lazima kama nchi tuwekeze kwenye michezo na tuongeze bajeti ya Wizara ya Michezo. Tukifanikiwa hapo ninayo hakika vijana wengi watakwenda kucheza kimataifa wataleta dola nchini na kwa kweli itakuwa ni ajira ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nami niwashukuru sana wote waliochangia na kwa vyovyote vile wamekubali tuliyoyapendekeza kama mapendekezo yetu ya Kamati. Pia niwashukuru sana Mawaziri, Mheshimiwa Waziri Ummy, Mheshimiwa Profesa Ndalichako na kaka yangu Mheshimiwa Harrison Mwakyembe. Nawashukuru sana kwa ushirikiano mnaotupa kwenye Kamati yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimemsikia Mheshimiwa Waziri Profesa Ndalichako anasema hukukosea kutuunda Guantanamo na naamini Mheshimiwa Spika hukukosea. Watu wanajituma sana na unajua ukishatengwa na ukapelekwa gerezani inabidi muungane ili mfanye vizuri zaidi. Hiyo ndiyo huwa sifa ya watu waliotengwa, wanaungana na wanafanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nitoe hoja kuomba Bunge lako Tukufu liweze kupitisha mapendekezo yetu yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Spika, naafiki. (Makofi)