Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Hamadi Salim Maalim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kojani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi hii. Kwanza, naomba ni- declare interest kwamba ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze na asilimia kumi ya wanawake, vijana na walemavu. Kwa kweli Halmashauri au Mikoa yetu mingi sana kwenye asilimia kumi hii ya wanawake na vijana inaonesha kwamba hela hii inatiwa mifukoni. Naomba nitoe mfano hai wa kitabu hiki cha Mkoa wa Manyara kwa bajeti ya 2016/2017. Mkoa wa Manyara asilimia kumi ya bajeti ya 2016/2017 ilitenga Sh.1,552,261,255 lakini kati ya hizo zilizotolewa kwa vikundi ni shilingi milioni 511.3 sawa na asilimia 33.

Mheshimiwa Spika, nasema pesa hizi zinaingizwa mifuko kwa sababu ukipitia kitabu chote hiki hukuti popote hiyo Sh.1,040,000,000 ambazo hazikutumiwa zilipoelezwa kwamba zimetumiwa kwa shughuli fulani. Ukiwauliza wao wenyewe wanapokuja na randama zao hizi wanasema kwamba zilizobakia zimetumiwa lakini unapopitia kitabu chote hiki hakuna eneo lolote linaloeleza kwamba hii shilingi bilioni moja iliyobakia imetumiwa ama katika ujenzi wa madarasa au katika ununuzi wa meza na viti au vitu vingine. Inasemekana kwamba hela hii inaingia kwenye mifuko ya wahusika. Naomba Halmashauri/TAMISEMI ifuatilie kwa kina suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ajenda yangu nyingine ni Mfuko wa Rais wa Kujitegemea. Mfuko huu tunajua kwamba umeanzishwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anachaguliwa na pande mbili za Muungano (Zanzibar na Tanzania Bara) na safari iliyopita najua Zanzibar alipata kura zaidi ya laki tatu, inawezekana hivyo.

Mheshimiwa Spika, sasa Mfuko huu wa Kujitegemea hadi leo unatumika upande mmoja tu wa Muungano. Ushauri wangu, ama mfuko huu ubadilishwe jina uwe ni Mfuko wa Rais wa Tanzania Bara au kama ni Mfuko wa Rais wa Kujitegemea kwa sababu Rais ni wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mfuko huu pia ufike Zanzibar kwa kusaidia Wazanzibar walioko kule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipengele kingine ni suala zima la...

SPIKA: Mheshimiwa, hakuna Rais wa Tanzania Bara.

MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Spika, sawa hakuna Rais wa Tanzania, sasa kama ni hivyo mfuko utumike pande mbili ijulikane kwamba ni Rais wa Jamhuri ya Muungano usitumike upande mmoja, ndiyo tunachodai.

Mheshimiwa Spika, kipengele kingine ni upande wa TASAF kwenye kunusuru kaya maskini. Naomba niseme kwamba suala hili kwa kweli kwa Zanzibar limepiga hatua kubwa sana. Wenzetu wa upande wa Bara kwa kiasi fulani tunapotembelea miradi tuki-compare wa kule na huku kwa kweli wenzetu wamepiga hatu kubwa sana. Katika kipindi kifupi tu kilichopita kwenye malipo ya Oktoba na Desemba imeonyesha kuna tofauti ya malipo yale waliyokuwa wakilipwa mwezi Oktoba na mwezi wa Desemba. Kwa hivyo, nitawaomba wahusika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana, dakika tano zimeisha.

MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Spika, naomba nimalize tu kidogo, naomba dakika moja.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kuna wahusika ambao Oktoba walilipwa Sh.60,000 lakini Desemba wakalipwa Sh.36,000; mwingine akalipwa Sh44,000 mwezi Desemba akalipwa Sh.32,000 bila kupewa taarifa kwamba makato haya yanatoka wapi. Naomba suala hili lifuatiliwe ili tupate ufumbuzi wa kujua watu wetu wanakatwa pesa hii kwa misingi gani?

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)