Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nitoe mchango wangu kwenye hoja za Kamati, hususan kwenye taarifa ya Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru na kumpongeza sana Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Zungu pamoja na Makamu wake na Wajumbe wote wa Kamati kwa kazi nzuri na kubwa ambayo wameifanya na kuweza kuainisha maeneo yenye changamoto na kutoa maoni pamoja na mapendekezo. Mheshimiwa Mwenyekiti na Kamati yake, nataka niwahakikishie kwamba maoni na mapendekezo waliyoyatoa katika Wizara yangu mara moja nitaanza kuyachambua na kuyashughulikia moja baada ya lingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya tangu amekuwa Rais wa nchi hii. Mambo yote ambayo aliyaahidi kwenye Ilani hii ya CCM na hususan kwenye eneo la Ibara ya 4 na Ibara ya 146 inayohusu vyombo vya ulinzi na usalama. Nataka niwathibitishie Watanzania kwamba Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake ya Awamu ya Tano wamewahakikishia Watanzania kwamba wamekuwa na amani, wamekuwa na usalama, wamekuwa na utulivu, mali zao zinalindwa pamoja na maisha yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba kuna baadhi ya Watanzania ambao wanabeza, wanakejeli juhudi za Mheshimiwa Rais, nataka nimthibitishie kwamba hao hawajitambui na hawajui kwamba yeye yuko na Mungu. Isaya 54, mstari wa 17 inasema: “Kila silaha itakayonyanyuliwa juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa,” kwa sababu Mheshimiwa Rais yuko na Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe ufafanuzi wa baadhi ya hoja ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge. Katika uchambuzi wa Kamati, ukurasa wa 20 wamezungumzia masuala mbalimbali, lakini moja ambalo nitakwenda kulitolea ufafanuzi ni lile linalohusu kuchelewesha upelelezi wa kesi na hivyo wakati mwingine kusababisha magereza kuwa na mrundikano hasa wa mahabusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango uliotolewa na Mheshimiwa Ruth Mollel ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati, ameelezea sana kwa hisia na uchungu mkubwa kwamba kesi nyingi zinachelewa, zingine miaka minne mpaka sita kwa mifano aliyoitoa. Nakubaliana naye, lakini sababu zinazosababisha kuchelewa kwa upelelezi wa kesi sio sababu moja, ni sababu nyingi kadha wa kadha. Kuna sababu zingine ni kutokana na kesi yenyewe jinsi ilivyo, inahitaji utaalam, wakati mwingine inahitaji kusafiri, tunahitaji fedha. Hata hivyo, pia nakubali kwamba, upelelezi mwingine unachelewa kwa sababu ya uzembe wa askari, kwa sababu ya askari kutowajibika na hivyo kuchelewesha upelelezi wa kesi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu nyingine ambayo ni kubwa na naomba Mheshimiwa Ruth Mollel anisikilize vizuri, pamoja na upande huo wanisikilize vizuri, kuna kesi ambazo zinachelewa upelelezi wake kwa sababu ya kutelekezwa. Baadhi ya kesi ambazo zinatelekezwa, nitolee mfano wa kesi maarufu ya Mheshimiwa Tundu Lissu. Kesi ya Mheshimiwa Tundu Lissu imetelekezwa. Katika mazingira ya kawaida kesi inapotelekezwa Jeshi la Polisi hawana namna nyingine ya kufanya uchunguzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika tukio lile lililotokea tarehe 7 Septemba, 2017, lile gari lilikuwa na watu wawili tu. Baada ya tukio lile, sisi wapelelezi na uendeshaji wa kesi kuna wale tunaowaita key witnesses; key witnesses ni pamoja na victim, Mheshimiwa Tundu Lissu na yule dereva aliyekuwa kwenye gari. Katika mazingira ya kutatanisha na ambayo mpaka sasa hatuelewi; ni kwa nini dereva ameitelekeza kesi hii na kutotoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi…

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: …ili atueleze hao ambao waliwafuatilia walikuwa ni watu wa aina gani?

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: …wembamba, wanene; warefu, wafupi, walivaaje …

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, analipotosha Bunge, taarifa.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: … ili kusaidia Jeshi la Polisi liweze ku…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Selasini, taarifa nilishazikataa tangu Mheshimiwa Stanslaus Mabula aliposimama, kwa hiyo naomba ukae tafadhali; Mheshimiwa Kangi Lugola.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema wakatulia ili niwape darasa la mambo ya upelelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukosa ushirikiano wa key witness ambaye ni dereva mpaka sasa, kesi hiyo tumeshindwa kuendelea nayo katika mazingira ya kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini namba mbili; niendelee kutoa maelezo kwa nini kesi zinachelewa. Mheshimiwa Tundu Lissu baada ya kutoka hospitali tulitarajia kwamba angekuja kwa uchungu wa kesi yake ili aje atoe maelezo kusaidia Jeshi la Polisi ili tuweze kuchunguza na kuanzisha ushahidi ambao tunaweza tukapeleka kesi mahakamani. Kwa hiyo katika mazingira ya namna hiyo tunashindwa kuendelea na baadhi ya kesi kwa sababu wanaohusika wanatelekeza kesi zao na wanashindwa kutoa ushirikiano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni matarajio yangu na niwaombe Watanzania wote ambao mnakuwa na kesi zenu za jinai, lazima mtoe ushirikiano kwa Jeshi la Polisi, lazima kesi hizi muwe na uchungu nazo ili kuondoa lawama kwa Jeshi la Polisi kwamba wanachelewesha kupeleleza ilhali ninyi mnatelekeza kesi zenu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kutoa mchango wangu… ninyi ndio mnaumiza Jeshi la Polisi kutoendelea kupeleleza.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Selasini, naomba utulivu tafadhali.

Mheshimiwa Selasini nimekutaja tena, naomba utulivu na wewe ndio Chief Whip kwa sasa, naomba utulivu.

(Hapa Mheshimiwa Selasini aliendelea kuhitaji nafasi ili atoe mwongozo)

NAIBU SPIKA: Siwezi kukupa nafasi kwenye miongozo wakati nimekataa.

Mheshimiwa Kangi Lugola, ongea na Kiti.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwenye kipengele hicho kwamba katika mazingira ambayo mashahidi muhimu hawatoi ushirikiano kwa Serikali, wasitumie ndimi zao kupotosha wananchi kwamba Serikali inahusika katika vitendo kama hivyo ilhali wao hawataki kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala la wahamiaji haramu; Waheshimiwa Wabunge wametoa michango yao juu ya wahamiaji haramu hasa katika Mikoa ya Kigoma, Kagera pamoja na Katavi. Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli inawahakikishia Watanzania kwamba wahamiaji haramu, hasa ambao wanatoka kwenye Nchi za Congo, Burundi, Rwanda pamoja na Uganda, kupitia Uhamiaji tunaendelea kufanya misako pamoja na doria na kuwabaini wahamiaji haramu wote wengine tunawarudisha kwao wengine tunawashtaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo katika kushughulika na suala hili la wahamiaji haramu, kuna maeneo mengine yana changamoto kubwa kama ambavyo Mheshimiwa Oliver Semuguruka amezungumzia maeneo ya Kyerwa kule. Nilipokwenda kule Isingiro, nikaenda Ruambaizi, pia kuna lile ziwa ambalo amelizungumzia ambapo wahamiaji haramu wanapenda kutumia mitumbwi na kuvuka kuja upande huu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Uhamiaji tutaendelea kufanya doria ikiwa ni pamoja na kutafuta uwezekano wa kuwa na boti katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika suala la wahamiaji haramu Serikali imeielekeza Idara ya Uhamiaji kuhakikisha kwamba wanasirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa hiyo niliyoitaja kuhakikisha kwamba wanafanya operesheni maalum ya kuwabaini na kuwachukulia hatua mahamiaji haramu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala la vitambulisho vya Taifa ambavyo vinatolewa na NIDA kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wametoa michango yao. Nataka niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa wanaendelea kubaini na kusajili na kutoa vitambulisho vya Taifa na wale ambao hawajafikiwa, wale ambao hawajapata vitambulisho wasiwe na wasiwasi, vitambulisho hivi lazima kila Mtanzania ambaye ana miaka 18 na kuendelea atapata na vitambulisho hivi vinatolewa bure. Kwa hiyo wale ambao hawajafikiwa wasidhani kwamba kuna ukomo na kwa sababu hajapata kitambulisho kwa hiyo sasa hatapata kitambulisho.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Kangi, muda wako umwekwisha.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)