Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hoja za Kamati hizi mbili. Nianze kwa kusema kwamba Kamati zimeandaa taarifa nzuri sana. Napongeza Kamati zote mbili; Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama lakini pia Kamati ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuishukuru sana Serikali kwa hoja waliyoitoa asubuhi kwa maana ya kauli ya asubuhi juu ya mauaji yaliyokuwa yanaendelea kule Njombe. Kwa namna ya pekee nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri kwa namna wanavyoshughulikia hili jambo kwa ujirani mwema kabisa na kwa nguvu zote kuhakikisha kwamba mauaji Njombe yanatokomezwa au yanadhibitiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Naibu Waziri, yeye aliweza kushiriki pia katika misiba kule Njombe, hasa ya wale watoto watatu pamoja na kuongea na wananchi na kutoa maelekezo mbalimbali kwa Jeshi la Polisi na viongozi wengine ili kwa pamoja kuweza kutokomeza mauaji yaliyokuwa yanaendelea kule Njombe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, naomba nichangie kidogo kwenye nishati ya madini, hasa juu ya umeme vijijini kwa maana ya umeme wa REA. Kwanza, napongeza kazi zinazofanywa na Wizara hii, wanafanya kazi kubwa na tunaona matokeo; vijiji vingi vinaendelea kupata umeme na maendeleo kupitia umeme yanapatikana na viwanda vingi vinafunguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye maeneo ambako hii miradi inaendelea kwa sasa, bado kasi yake siyo kubwa, ni ndogo hasa tukiangalia kwenye mikoa yetu, hasa kwenye Jimbo langu, kasi ya usambazaji wa umeme ni ndogo. Naomba Serikali ijitahidi kuwapa Wakandarasi fedha ili waweze kuhakikisha kwamba wanasambaza umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo tayari kusambaza umeme lakini ukiwauliza tatizo kubwa linakuwa ni fedha, wanashindwa kupata fedha kwa ajili ya kununua nguzo na vifaa mbalimbali kama nyaya na transformer. Pia kuna tatizo la uzalishaji wa hivi vifaa. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, wajitahidi kuhakikisha kwamba wale wazalishaji wa vifaa na fedha zinakwenda kwa wakati ili maeneo yote ya vijijini yaweze kupata huu umeme wa REA. Ni muhimu sana na nina uhakika kabisa itatubadilisha Tanzania baada ya muda siyo mrefu Tanzania haitabaki kama ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kidogo juu ya Shirika la TANESCO. Shirika hili pia linakabiliwa na madeni mengi kama walivyoeleza Wajumbe na inavyoeleza taarifa, lakini ulipaji wake wa madeni hayo bado unakwenda kwa kasi ndogo. Naomba Serikali ilipe madeni kwenye shirika hili ili liweze kujiendesha. Ilivyo sasa hivi, inapotokea kuna tatizo ambalo linahitaji vifaa, wanunue transformer au vifaa kwa ajili ya kurejesha umeme kwenye eneo fulani, inachukua muda mrefu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo mengine, kwa mfano, Nyanda za Juu Kusini, maeneo yetu yana mvua nyingi, kwa hiyo, umeme umekuwa ukiathiriwa, transformer nyingi zimekuwa zikiunguzwa na radi. Kwa hiyo, inapotokea transformer imeungua, inakuwa ni vigumu; na inachukua muda mrefu sana kurejesha umeme katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati, alikuja kwenye eneo langu akakuta tatizo kubwa sana la umeme kwenye maeneo ya muhimu; ya hospitali na maeneo ya vijiji kwenye Kata moja ya Ikuna, lakini alipofika alitoa kauli na akaleta ile transformer. Nashukuru sana kwa Wizara nzima, Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kuleta hii transformer. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo sasa, mpaka leo hii ile transformer haijafungwa, sijaelewa wanakosa vifaa gani? Kwa hiyo, naomba mwezeshe hili Shirika la TANESCO ili liwe na uwezo wa kurejesha huduma haraka, kwa sababu linapochelewesha huduma, madhara yanakuwa makubwa. Viwanda vinasimama kufanya kazi na huduma haziwezi kuendelea kwa sababu umeme haupo. Likiwezeshwa vizuri litaweza kujitegemea na kuhakikisha kwamba umeme unarejeshwa kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye maeneo haya ya Nyanda za Juu Kusini kwa sababu kuna radi nyingi, napendekeza kama inawezekana, tutumie ule mfumo wa Shirika kama la CEFA ambalo wanajenga transformer zinajengewa ndani na sijawahi kusikia transformer ya CEFA imepigwa radi. Kwa hiyo, kwenye maeneo ya mvua tunaweza tuka-adapt ule utaratibu wa CEFA ili transformer…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa. Muda wako umekwisha.

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)