Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja zilizoko mbele yetu. Kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi kwa kuipata nafasi hii, nafasi adhimu kabisa. Nianze kwanza kabisa kwa kumpongeza Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kukubali kukaa na wadau wa sekta ya madini, nami pia ni mdau, mchimbaji mdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nijikite kwanza kwenye ushauri, kwa sababu dakika tano ni chache. Kwanza niipongeze Kamati kwa kazi nzuri ambayo wameifanya ya kuyapitia yote tuliyoyapendekeza kwenye kikao tarehe 22; kwa kweli kazi nzuri wameifanya, nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, naomba Serikali iyafanyie kazi haraka yote ambayo yamependekezwa na Kamati ili kuepusha utoroshwaji wa dhahabu na madini mengine. Kwa mfano ucheleweshwaji wa utoaji wa leseni. Ucheleweshwaji wa utoaji wa leseni unachangia sana utoroshaji wa madini kwa sababu kuna watu wanaifanya kazi bila kuwa na leseni Serikali haiwatambui, wanatorosha madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali ifanye haraka sana kuwatambua hawa wachimbaji wadogo wadogo na kuwarasimisha, kuwapatia leseni ili iweze kuwatambua na kuweza kukusanya kodi mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu mwingine ni kwamba NEMC, OSHA, ZIMAMOTO na Madini waweze kukaa pamoja ili kuweza kurahisisha taratibu zote za kuweza kutoa vibali. Leo vibali vimekuwa na matatizo, NEMC anakuja kivyake, OSHA anakuja kivyake, Madini anakuja kivyake; leseni zinachelewa kutoka na zikitoka pia ni kwa gharama kubwa. Naiomba Wizara ya Madini ilishughulikie hili ili waweze kuweka center moja ya kuweza kuyashughulikia haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu mwingine ni kwamba, kuna maeneo mbalimbali; kwa mfano Wilaya ya Nyangh’wale, kuna maeneo makubwa ambayo yanafanyiwa uchimbaji mdogo mdogo lakini wachimbaji hawajarasimishwa mpaka hivi sasa. Nina maeneo kama manane ambayo wachimbaji hawa wadogo wanachimba kiholela, wanaharibu mazingira na pia Serikali haipati mapato. Naiomba Wizara iyarasimishe maeneo hayo ili kuweza kuwapa wachimbaji wadogo wadogo na kuwapatia leseni na kuwatambua ili Serikali iweze kukusanya mapato. Leo hii dhahabu nyingi inatoroshwa kwa sababu udhibiti haupo, Serikali inapoteza mengi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, jana alikuwa akijipambanua hapa Mheshimiwa Wizara wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kingwangalla, anasema anachangia asilimia 27 kwenye Pato ya Taifa, lakini dhahabu na madini mengine yakiwekewa utaratibu mzuri, naamini kabisa itakuwa ni sekta ya kwanza kuchangia mapato makubwa sana katika Taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine ni kuhusu rasilimali watu pamoja na vitendea kazi; Wizara hii ya Madini iongezewe, Serikali itoe pesa kuongezea hii bajeti ili iweze kupata hawa watendaji pamoja na vitendea kazi vya kutosha kama vile magari ili kuweza kuzunguka maeneo mbalimbali. Kwa mfano, ukiangalia leo Geita ina gari mbili ambazo nazo hazifai, lakini pia ina wafanyakazi 20 tu, lakini Geita inaongoza kwa uchimbaji wa dhahabu. Je, wale watumishi 20 watawazungukia vipi wale wachimbaji wadogo na kuweza kukusanya maduhuli ya Serikali? Naiomba Wizara iongezewe pesa ili sasa waweze kuajiri watu wengi na pia kuweza kupata vitendea kazi kama vile gari na vifaa vingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba nitoe ushauri, kwamba Wizara itengewe pesa ili iweze kujenga maabara katika Mkoa wa Geita, kwa sababu Mkoa wa Geita ni kitovu cha dhahabu, ijengwe maabara kubwa na kuweka vifaa mbalimbali kwa ajili ya upimaji wa dhahabu na mambo mengine mbalimbali yanayohusiana na masuala ya dhahabu. Kwa hiyo naiomba Serikali itenge fedha ili kuweza kujenga maabara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na la mwisho niliomba nichangie muda mrefu, sasa dakika tano hazitoshi, naunga mkono hoja. (Makofi)