Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Oliver Daniel Semuguruka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu na pia kuwa mchangiaji wa kwanza katika Bunge lako Tukufu jioni hii. Kwanza kabisa nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anazozifanya katika Taifa letu. Pia nazipongeza Kamati zote mbili pamoja na Mawaziri na Wizara husika kwa ushirikiano wanaoutoa kwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijielekeze moja kwa moja kuchangia hoja zote mbili zilipo mbele yetu. Kwanza kabisa nianze na ripoti ya Nishati na Madini. Nianze kumshukuru Waziri wa Nishati kwa kuwezesha kupata umeme katika Wilaya yetu ya Ngara, lakini kuna vijiji ambavyo havijapata umeme, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, nasikitika kwa kuwa simuoni humu ndani, lakini Naibu Waziri yupo, naomba alisikize hili. Kuna kaya ambazo hazijapa umeme katika Wilaya yetu ya Ngara, naomba wajitahidi wamalizie ili waweze kupata umeme. Kwa mfano, unaweza ukakuta kuna kaya mimi nina umeme, Mheshimiwa Matembe hana umema, Mheshimiwa Kangi ana umeme, ndiyo ilivyo. Kwa hiyo naomba kila Kaya wapate umeme, kwa kweli wanafanya kazi nzuri na nampongeza sana Mheshimiwa Rais, bila yeye hata tusingeweza hata kupata umeme huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijielekeze moja kwa moja katika mradi wa Kabanga nickel, ambao uko Wilaya ya Ngara. Mradi wa Kabanga nickel umesemwa muda mrefu sana, pindi niko shule ya msingi, mpaka sasa hivi nazeeka unaitwa ni mradi tu wa Kabanga nickel, lakini hakuna kitu ambacho tunakiona. Kwa hiyo, ninaomba, naishukuru sana Serikali kwa kurudisha leseni ya Kabanga nickel Serikalini, lakini naomba Mwekezaji wanayemtafuta Serikali awe ni mwekezaji kweli, kwa sababu kuna wawekezaji ambao ni makanjanja. Nimesema tangu niko primary wanakuja wawekezaji wanatafuta research kwamba kuna madini ya Kabanga nickel wakifika wanaondoka, hamna kinachoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati niko shule ya msingi nilikuwa naona ndege zinapita, unaambiwa zinaenda Kabanga nickel kuangalia madini yanavyoendelea. Baada ya muda wale watu wana disappear, hiyo research gani inayofanyika? Kweli mimi mpaka nafika umri huu, hiyo ni research kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishukuru kwamba Mheshimiwa Rais ameweza kuliona hili na kurudisha leseni Serikalini. Naomba iwe kweli kweli, sababu wananchi wa Wilaya ya Ngara wanahitaji kunufaika na mgodi ule, kwa sababu bila kunufaika na mgodi ule, wanaishia tu kuona majengo, kuna majengo yamejengwa na pale na Kabanga nickel, ukienda pale ni Kabanga nickel. Kwa hiyo ni vema zaidi tuweze kupata ushirikiano na Serikali walete Mwekezaji wa kweli, asiwe Mwekezaji wa uongo uongo ili tuweze kunufaika na hayo madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, madini haya yanapatikana Ngara mpaka Congo, Congo yapo nafikiri kwa asilimia 65, pia yaani huo mkondo unaanzia Ngara mpaka Congo. Sasa kwa nini Congo waendelee kunufaika sisi Tanzania tusinufaike au ni kwa sababu tuko mpakani. Kwa hiyo, naomba Waziri wa Madini na Naibu wake wanisikilize kwa makini, kuna ujenzi wa reli ya kati, tunapenda ikitokea tuweze kunufaika na hii reli ya kati, tupate kusafirisha haya madini yetu ili yaweze kununuliwa huko nje, lakini sasa hakuna hakuna kinachoendelea.(Makofi)

Naomba niongelee pia Jimbo la Kyerwa; madini ya tin, naiomba Serikali ifanye haraka kukamilisha taratibu za kuruhusu kusafirisha tin kwenda kwenye masoko ya nje. Wananchi wa Kyerwa wanasubiri kwa hamu sana ili waweze kunufaika na hayo madini ya Kyerwa. Pia naomba wananchi wapate mafunzo ili wanufaike katika mgodi ule kwa sababu kuna ambao wanaenda kuchimbia vijembe, akifika kule mara unaporomoka udongo umemuua, kuna vifo vingi vimetokea. Jamani hivi kweli hatuwezi kuangalia hili kwa jicho la huruma?

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kyerwa wanapenda sana wanufaike na haya madini ya tin, lakini hakuna mafunzo yanayotolewa kwa wananchi. Pia wachimbaji hawana vitendea kazi, ndiyo kama huo mfano nilioutoa, vitendea kazi anaenda na kajembe kake amekaweka begani, kajembe ka kawaida, hawezi kuambiwa kwamba kuna kitu hiki kinatakiwa kifanyike uchimbe hivi uende urefu fulani hivi, hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwona pale Naibu Waziri wa Madini, naomba mtusaidie ili tuweze wale wachimbaji wadogo wadogo wa Kyerwa waweze kupata elimu ya kuweza kujua hapa nikienda kuchimba na haka kajembe hakatanisaidia au mwisho wa siku atafariki, ataacha familia yake inateseka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naiomba sana sana Wizara ya Madini iangalie kwa jicho la huruma mradi, mgodi wa Kabanga nickel na mgodi wa Kyerwa, kwa kweli nawaomba sana sana. Mheshimiwa Rais wetu mpenzi anasaidia wanyonge, sasa hawa wachimbaji wadogo wadogo na wale watu wa hali ya chini, tulisipowasaidia inaleta ukakasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tuna ripoti mbili za Kamati ziko mbele yetu. Naomba nijielekeze katika ulinzi na usalama. Wilaya yetu ya Ngara, mimi ni mzaliwa wa Ngara japo ni Mbunge wa Mkoa Kagera Viti Maalum, lakini wahamiaji haramu wako wengi. Hao wahamiaji haramu wanatokea Burundi, wanapita njia za panya, njia za chocho, kwa hiyo wakipita njia za panya wanakuja kutudhuru sisi Watanzania ambao tuko mpakani. Kwa hiyo, naomba Serikali itusaidie kupata magari mapya na mafuta ya kutosha ambayo yatafanya doria, masaa 24.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika kusema ilikuwa ni mwaka juzi, 2017, kuna Afisa wa Uhamiaji alipata ajali na akafariki kwa sababu ya gari bovu na alikuwa anaenda kwenye doria katika hizo njia za panya za uhamiaji. Sasa naomba tuweze kupata magari ya kutosha mapya na tuweze kupata mafuta ya kutosha ili hata wale Maaskari wa Uhamiaji waweze kufanya kazi zao bila kipingamizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikirudi Karagwe, ni mpakani pia tunapakana na Uganda, Rwanda na Burundi yaani kuna Ziwa linazunguka. Naomba upande wa Karagwe barabara siyo rafiki kabisa, barabara ni za shida sana. Naomba Wizara hii ya Usalama na Mheshimiwa Kangi, babu yangu ananisikia, watuwekee barabara rafiki ili hata mtu akienda kufanya doria aweze kufika. Katika hilo naomba sana sana kwa Mheshimiwa Kangi, Waziri wa Mambo ya Ndani atusikilize na atuangalie kwa jicho la huruma; kule Karagwe kuna maziwa mfano Ziwa Ngoma, Buligi, Kavunjo, Nyamlebe, tunaomba kupatiwa boti ili doria ziweze kufanya kazi kwa urahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaomba kuwepo kwa boti kutasaidia kupambana na biashara haramu zinazofanyika majini kwa sababu ile Karagwe imezungukwa na ziwa. Kwa hiyo, tusipopata boti ndiyo hivyo wahamiaji haramu wanatusumbua wanatoka, Uganda, Rwanda na Burundi hakuna tunachofaidika. Kwa hiyo Mheshimiwa Kangi, babu yangu Waziri wa Mambo ya ndani, naomba ulifanyie kazi tupate boti kwa ajili ya kusadia wananchi ambao wako Karagwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda Misenyi, Wilaya ya Misenyi kwenye Kituo cha Ushuru wa Pamoja na Uganda yaani tulijiunga Kituo cha Ushuru Uganda na Tanzania. Kile kituo kazi kinafanya kazi twenty four hours, lakini Maaskari wa Uhamiaji ni wachache, hawatoshi, yaani mtu anaweza aka-overnight, akaja akashinda, hivyo. Kwa hiyo hatafanya kazi kwa ufanisi, naomba tuongezewe Maaskari wa Uhamiaji, pale ni mpakani, ukitoka tu pale Mutukula unaingia Uganda. Kwa hiyo wanaotoka Uganda kuja Tanzania wengi ni wahamiaji, sasa tutawajuaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto tuliyonayo Maaskari wa Uhamiaji ni wachache, mtu mwingine anaweza akachoka hata asiweze kufuatilia aanze kuangalia pasipoti imetoka wapi na inaenda wapi. Kwa hiyo, tukipata Maaskari wa kutosha wa kuwa wanapeana shift itatusaidia hata sisi. Kwa hiyo naomba sana sana Mheshimiwa Kangi babu yangu atusaidie katika hilo. Tangu mwaka jana 2018 ndiyo huo muungano ulifanyika Uganda na Tanzania, lakini ndugu zetu wa kule Uganda wana Maaskari wa kutosha wa Uhamiaji why kwetu tusipate wale Maaskari wa uhamiaji wa kutosha? Ni kwamba hawapo au ni ile kutokupanga kwamba ukiambiwa uende Kagera ni mpakani huko, kama changamoto tunazozipata kwamba ukienda huko kuna Wanyarwanda, kuna Wahutu, utauawa no siyo hivyo, mimi nimezaliwa Ngara lakini kuna shida hizo za wahamiaji, lakini wakitusaidia katika kuleta Maaskari yanaisha. Kwa hiyo naomba hilo lifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, gari la uhamiaji la Misenyi ni chakavu chakavu yaani halifai katika kufanya doria, hivi kweli tuko Tanzania na tuko mpakani mwa Uganda? Yaani Maaskari wa Uganda ndiyo wanasaidia kwamba huyu ni mhamiaji kutoka Uganda, huyu ni Mganda amekujaje Tanzania yaani ni aibu, kwa hiyo naomba sana sana, waweze kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna tishio la usalama mpakani, kama madawa ya kulevya ni ngumu sana kubainika sababu mbwa aliyepo pale Misenyi amezeeka, hata akifundishwa hawezi kufundishika. Sasa tunafanya kitu gani? Kwa hiyo naomba wahusika watulee mbwa ambaye bado ni kijana sijui niseme yaani ambaye anaweza kufundishika akaelewa. Kwa hiyo naomba sana sana, Wizara ya Mambo ya Ndani muweze kutuangalia kwa jicho la huruma.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, naona dakika zimeisha nilikuwa nayo mengi. Ahsante sana. (Makofi)