Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. OMAR M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa pili kwenye taarifa ya Kamati hizi mbili. Awali ya yote nichukue fursa hii kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukutana na wachimbaji wadogo wadogo. Mimi niupongeze uamuzi huu nikiamini ulikuwa ni uamuzi wa busara na nikiamini kabisa moja ya maeneo ambayo yanaweza kutusaidia kuongeza pato la Taifa ni kwenye sekta ya madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika sekta hii ya madini, wachimbaji wadogo wadogo hawa wamekuwa hawapewi kipaumbele. sasa kutokana na Mheshimiwa Rais kukutana na wachimbaji wadogo wadogo maana yake tunaona kabisa dhamira ya Serikali kuwatambua wachimbaji wadogo wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili zipo changamoto mbalimbali na moja ya changamoto hizo Mheshimiwa Rais ameweza kuzizungumzia na majuzi nimemsikia Waziri mwenye dhamana akizungumzia kwamba wapo watu wenye maeneo ambayo wameyashikilia kwa muda mrefu na hawajayafanyia kazi. Ushauri wangu, Waziri mwenye dhamana na eneo hili afanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mmoja tu, katika eneo langu la Wilaya ya Kilindi, kwenye Kijiji cha Kwafumbili, Kata ya Negelo, kuna mwekezaji mmoja ana maeneo mengi sana, ameyashikilia maeneo haya hajayafanyia kazi, lakini wachimbaji wadogo wadogo ambao wangeweza kupewa eneo hili wangeweza kuhakikisha kwamba wanafanya shughuli hizi na Serikali ingeweza kupata mapato ya kutosha. Naamini kabisa Mheshimiwa Waziri atalifanyia kazi hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo mafupi katika eneo hili sasa naomba nichangie katika eneo la sekta ya gesi. Kwa kweli kwanza nimpongeze sana Waziri mwenye dhamana ya nishati hususan katika eneo la REA, amefanya kazi kubwa sana. Ameweza kupita katika maeneo mbalimbali na ameweza kutusikiliza shida zetu. Naamini kabisa umeme huu utakaposambaa katika Vijiji vyetu vyote maana yake wananchi wetu wataweza kupata maendeleo. Ukizingatia dhamira ya Serikali ya nchi ya viwanda, hatuwezi kuendesha viwanda bila kuwa na umeme wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri eneo hili lipewe umuhimu wa hali ya juu lakini pia wakandarasi hawa ambao wamepewa kusambaza umeme vijijini, wamepewa maeneo makubwa sana. Tuangalie namna ambavyo wanaweza kupunguziwa mzigo huu ili dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kwamba kila kijiji kinapata umeme, iweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye eneo la sekta ndogo ya gesi na nikizungumzia eneo la SONGAS. Eneo hili nimzungumzie mtu anayeitwa Pan African Energy. Huyu mtu Pan African Energy alikuja kwa jina la Ocelot; hii ni kampuni ambayo ilikuwa inatokea Canada. Watu hawa walikuja kama wawekezaji kwa ajili ya kusaidia suala la umeme, ikaanzishwa kampuni ya SONGAS ambayo tunasema ni special purpose vehicles.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiiangalia kampuni hii na muundo wake unasikitisha sana. Unasikitisha kwa sababu SONGAS yenyewe ambayo ni special purpose vehicles ukiangalia umiliki wake watu wa TANESCO wana asilimia 9.0, TPDC asilimia 28 na huyu Globeleq ana asilimia 54. Sasa unajiuliza huyu Globeleq huu mtaji aliouwekeza mpaka akapata asilimia 54 ameupata wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kushangaza sana ni kwamba hakuna kampuni iliyosimamia kufanya tathmini, yaani kwamba TANESCO ana asilimia tisa, TPDC asilimia 28 ni nani alisimamia tathmini hizi? Ukiangalia na maelezo ya kutoka kwa watu wa Globeleq wanakwambia kwamba eneo lile la SONGAS ambapo lilikuwa ni eneo la TANESCO thamani yake ilikuwa ni dola milioni moja. Sasa ni nani alisimamia uthamini ambao umehakikisha kwamba Serikali inapata asilimia tisa peke yake? Maana yake unaona kwamba kuna matatizo makubwa sana hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda mbali zaidi unaangalia eneo la TPDC. TPDC wana visima vinne na visima hivi vinne ndivyo ambavyo vinatoa gesi; lakini vinatoa gesi thamani yake imethaminishwa kwa asilimia 28 tu, huu ni wizi mkubwa sana. Naishauri Serikali iangalie namna gani inaweza ikalisimamia suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hilo kuna mambo ambayo yana upungufu mwingi sana na moja ya upungufu ambao upo katika mkataba huu ni eneo ambalo Globeleq katika taarifa zake za pesa anaonesha mkopo wake mwanzoni ulikuwa unaonyesha kama ni preferential, lakini sasa hivi inaonesha kama ni debit note. Debit note maana yake ni kwamba anapotaka kulipa madeni atapunguza gharama zake zote mwishoni ndio atalipa deni. Mkataba huu una upungufu mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nalisema eneo hili kwa sababu naamini kabisa Serikali inapoteza mapato mengi sana; na hii ni kinyume kabisa na mikataba ya madini ya nishati/petroli ya mwaka 2015. Naomba Serikali ilipitie eneo hili vizuri sana na nina uhakika Mheshimiwa Naibu Waziri mwenye dhamana na eneo hili ananisikiliza na atalifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna upungufu mbalimbali ambao nimeuona na ambao Mwenyekiti wa Kamati ameuzungumzia na naamini Serikali itaufanyia kazi. Moja ya upungufu huo ambao nadhani ni mikataba hasi ni suala la TANESCO na Pan African Energy. PAET –Pan African Energy (PAET) wao wanatoa vipaumbele vya kwenye kuwauzia gesi kwanza wanawauzia SONGAS pili viwanda 32 na wa mwisho anakuwa ni TANESCO. Jambo hili halijakaa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu mwingine ambao upo katika mikataba hii ni suala la tozo ambalo TANESCO wanatozwa. Katika Mkataba huu kuna kipengele kinachosema kwamba TANESCO asipoweza kununua kiwango cha juu na cha chini anatozwa faini; eneo hili limekaa vibaya na kwa taarifa yako ni kwamba hadi kufikia Januari, 2018 TANESCO wanadaiwa bilioni arobaini na milioni mia tatu. Mkataba huu haujakaa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo lina upungufu na ambalo ningependa kulizungumzia ni eneo linahusu Production Sharing Agreement. Huu ni mkataba ambao Serikali iliingia na watu wa Pan African Energy. Moja ya upungufu mkubwa ni kwamba watu wa Pan African Energy wao wana-operate kwenye mikondo yote mitatu kwa maana upstream, midstream na downstream, kitu ambacho sio sahihi hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Petroli, inaruhusu Pan African Energy ku-operate kwenye upstream. Tafsiri yake ni kwamba gharama za midstream na downstream zote wanazipeleka juu, maana yake wanaiibia Serikali; Serikali lazima iangalie katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, baya zaidi ni kwamba Pan African Energy katika Production Sharing Agreement wameiwekea sharti TPDC kwamba ili aweze kushiriki katika shughuli za uzalishaji ni kwamba lazima aweze kuweka dhamana na dhamana hiyo lazima ipitiwe na Pan African Energy. Hili jambo ni mkataba hasi na ni lazima Serikali iweze kupitia eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ufupi utaona kwamba suala la Pan African Energy kuna upungufu makubwa sana, niiombe Serikali…

MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kigua kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Yosepha Komba.

T A A R I F A

MHE. OMAR M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea lakini ina upungufu kimsingi, hoja ninazozizungumzia ni kubwa zaidi kuliko hiyo anayoizungumza yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia kwamba TPDC wao hawaruhusiwi kushiriki kwenye shughuli za uzalishaji mpaka waweke dhamana, lakini dhamana hiyo haiwezi kuwa na thamani yoyote ile mpaka iwe imekubaliwa na Pan African Energy. Kimsingi utaona kwamba kuna matatizo makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ufupi niseme Mkataba wa Pan African Energy au Production Sharing Agreement una matatizo makubwa sana. Ushauri wangu kwa Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, naomba wakae chini waone namna gani ambavyo wanaweza kuhakikisha kwamba tunakaa chini kwa sababu Serikali inapoteza mapato mengi. Pamoja na hayo mkataba huu umekwenda vibaya zaidi, unaisha 2024, sasa kwa nini tusubiri mpaka 2024? Nashauri kwa kupitia njia zile tulizoptia kwenye madini basi tuweze kutumia njia hiyo hiyo kwenye sekta ya gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo machache, naunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)