Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii na kipekee kabisa namshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai na nafasi tuliyopata sisi Wabunge kuzungumzia mambo ya maendeleo ya nchi yetu katika jengo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwenyekiti wangu, amewasilisha ripoti ambayo ni nzuri kabisa, ripoti ambayo tuliijadili na ripoti ambayo inazungumzia mambo mengi. Nimesimama kuweka msisitizo katika mambo machache tu ambayo labda naona ni vyema kama wote, tukayafahamu na tukaweza kuyafafanua zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nimpongeze sana Amiri Mkuu ambaye ni Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuvisimamia vyombo hivi na kuviimarisha na hata tukawa na amani katika nchi yetu, amani inayotuwezesha sisi tukae hapa, tuweze kuzungumza kwa nafasi bila wasiwasi,. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii ina amani kwa vile Wizara ya Ulinzi na Usalama na Wizara zote nyingine zinazohusu mambo hayo ziko vizuri, Wizara ya Mambo ya Ndani, ikisimamiwa na Waziri wetu Kangi Lugola na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ikisimamiwa na Waziri wetu, Mwinyi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kamati hatukuona tatizo sana, kwa hela za matumizi kutoka kwa wakati, hela ambazo zilikuwa zina shida ni hela za maendeleo. Inapokuwa kwamba hela za maendeleo haziendi kwa wakati kama ilivyoandikwa kwenye ripoti yetu, inakwamisha mambo mengi na hapa nitaanza sasa na Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, haikuweza kupata hela za maendeleo kwa wakati muafaka na hivyo kufanya majengo yetu yaliyo katika Balozi kuwa katika hali ambayo siyo nzuri. Wakati Balozi zetu haziko kwenye hali nzuri, inaonesha taswira mbovu kwa nchi, majengo yale yanaonekana yamekaa tu na kwa hivyo basi, kwa vile hatukupata pia nafasi sisi Wabunge, kwenda kutembelea yote nitakayozungumza hapa ni kwa nadharia kwa yale tuliyoelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona kwamba kwa kuwa ni ngumu sana kuendelea kulipia kodi ya pango katika maeneo mengi kwenye Balozi zetu, ni vyema sasa, Balozi zetu zikawezeshwa, zikajenga majengo yake, zikaweza kupangisha zikanufaika kwa kodi na pia ikaonesha jinsi ambavyo sisi tunajali heshima ya kuwa na Balozi katika maeneo husika. Sioni sababu ya kutaja yote lakini, niseme ni mengi, imekuwa hivyo, kwa hiyo naweka msisitizo kuwe na mortgage finance ambayo itasaidia Balozi hizo, kwa sasa na kwa muda ujao wakaweza kupata kipato lakini pia wakawa katika hali nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, sio hayo tu, hata magari yaliyoko kule, naamini nitatoa ushuhuda kwa magari yaliyo India kwa sababu niliwahi kwenda matibabu New Delhi nikaliona gari la Balozi na zile fujo za uendeshaji India, gari hilo limegongwa kila upande huku na huku, lakini sio rahisi sana, pia wakawa na magari kwa wakati muafaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali ione umuhimu wa kuonekana kwa sababu wanasema ni vyema muonekano ukawa mzuri, yaani halo effect, mara moja na mtu akaku-judge kwa muonekano mpaka akaja kukuangalia ndani inakuwa ni jambo la baadaye sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kuhusu Wizara hii ya Mambo ya Nje, ni ile (APRM) African Peer Review Mechanism haijaweza kupata nafasi yake katika nchi yetu. African Peer Review Mechanism inaiweka nchi katika mizani na nchi nyingine na sisi tunaamini Tanzania tuna utawala bora, tunaamini Tanzania tuna uongozi mzuri, tunaamini Tanzania sasa hivi, tuko vyema. Ni kwa nini basi, African Peer Review Mechanism isiwezeweshwe ili tukapimwa, tukalinganishwa na nchi nyingine za Afrika wakaweza kweli, kutupa tathmini, wale eminent persons wanaofanya tathmini hiyo, imeshafanyika mara moja, miaka ya nyuma, lakini wakati muafaka, eneo hilo limepauka, ofisi hiyo imebidi wamrejeshe, Bibi Rehema Twalibu aendelee kukaa kaa pale tu lakini sio kwa hali ambayo inakubalika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua huku Bungeni kuna mwakilishi ambaye anatuwakilisha kule, lakini hela wanazopata zinapitia Wizara ya Mambo ya Nje, wangeweza wenyewe kupata fungu lao na wao wakaweza kupangilia na hivyo basi tukaweza kufanyiwa tathmini vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende sasa, kwenye uwakilishi wetu, katika Balozi katika kutafuta biashara. Hivi majuzi yamekuweko mazungumzo na pia hali halisi kwamba kuna mizigo iliyokuwa inakwenda Congo, lakini imekwama kwa sababu au ni ya mahusiano, au ni jinsi ambavyo hatujaweza au Wizara yetu haijaweza kusimamia vizuri, naomba kupitia Bunge hili, sasa Wizara ya Mambo ya Nje, ifanye mkakati maalum ili hata ile mizigo iliyokwamba Tunduma itoke mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kwamba sisi, misimu yetu ya kilimo inafahamika wazi, ni wakati gani tunalima, wakati wa masika, ni wakati gani tunavuna, ni wakati gani tunauza, mara nyingi na imekuweko hata juzi, hata jana, tumezungumza kwamba bidhaa zetu, yakiwemo mahindi hayana soko, lakini kama Wizara hii, ingezungumza na Wizara nyingine za Mambo ya Nje, mahindi haya yangetoka yakapitia Zambia, yakaenda kuuzwa, sioni kwa nini tuna Wizara ambayo inahusika na bado mambo hayo hayatekelezeki kwa haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba wakati wa kupitisha maazimio ya hii ripoti yetu ya Kamati, jambo hilo likafikiriwa na likazungumziwa sana ili tupate masoko mengi, kote, ili bidhaa zetu, ziweze kuuzwa kwa haraka na wakati muafaka, hela hiyo iweze kurejeshwa kwa wananchi wetu na sisi wenyewe tuendee kufaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Majeshi yetu yameendelea kuimarika kila wakati na niseme tu, kuna mambo machache ambayo yakiwekwa vizuri, hata majeshi haya yatakuwa hayalalamikiwi na mambo haya sijui kama yanahusu sana haya majeshi moja kwa moja au yanahusu Wizara ya Fedha kwa sababu ni madeni ya nyuma ya majeshi yetu kulipa katika vyombo vinavyotoa huduma, vikiwemo vyombo vinavyotoa huduma ya maji na vyombo vinatoa huduma ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu tumeingia Bunge hili tumekuwa tukiomba sana madeni ya maji yalipwe kwenye mamlaka za maji. Kuna maeneo ambayo ni nyeti, huwezi kwenda kukata maji; na hapa eneo la uhakika na la karibu sana ni Chuo cha Polisi Moshi. Kuruta wanapoingia pale wanaingia wengi kwa mara moja, maji yale yana madeni ya siku za nyuma ambayo ni makubwa yanakwenda kwenye takriban bilioni mbili. Kwenda kukata maji kwa kuruta haiwezekani na wala haieleweki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba, kwa sasa wanakwenda vizuri kulipa current bills lakini basi Wizara ya Mambo ya Ndani izungumze na ione kwamba italipaje madeni ya nyuma ili ile Mamlaka ya Maji kule Moshi (MUWASA) isifunge shughuli nyingine na wala watu wasichukie watakapoona kwamba wamepeleka pendekezo la kupandisha maji, watadhani kwamba ni kwa ajili ya ile bili kubwa ya CCP ndiyo maana wananchi wanapandishiwa maji. Hapa naweka msisitizo tunaomba sana madeni ya nyuma yalipwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, umeme pia walizungumzia, lakini niseme kwamba ni vyema basi vyote hivyo vikafanyika kwa pamoja ili tuweze kujua kwamba kama tunavyoamini majeshi na msemo unaosema hilo jeshi mambo yake na vitendo vyake sawasawa, viwe sawa hata kwenye ulipaji madeni ili wote waweze kuwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba napongeza ile hali ya vyombo vetu vya majeshi kuweza kuwa na kandarasi zao; ujenzi wa nyumba za polisi wanajenga wenyewe sasa. Hata hivyo, naomba basi pamoja na kwamba wanajenga wenyewe, wajenge nyumba za kwenda juu; na hizi nyumba za kupanga bungalows zinachukua nafasi kubwa. Ni wazi kwamba kwa sasa Mungu haumbi tena nchi, alishaumba, ni sisi wenyewe tutumie vizuri. Kwa hiyo nitoe rai yangu kwamba majengo yanayojengwa sasa polisi na kwingineko yaende juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba nipongeze vyombo hivyo vyote na niwaombee kwa Mungu tuendelee kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)