Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na namshukuru Mungu kupata nafasi hii ya kuzungumzia taarifa mbili za Kamati. Nitaanza kuzungumzia taarifa inayohusiana na kilimo.

Mheshimiwa Spika, mimi ni Mbunge ninayetokana na wazazi maskini kabisa kwenye Taifa hili. Ukitaja watu maskini wa nchi hii unataja wakulima. Kama kweli tumedhamiria kuwainua wakulima basi ni lazima Serikali ijielekeze walau tuwe na kiwanda hata kimoja cha zana za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni jambo la aibu sana panga tunaagiza kutoka nje, shoka tunaagiza kutoka nje, jembe tunaagiza kutoka nje, hivi huyu mkulima ambaye tunataka kumuinua tutamsaidiaje kwa karibu kama hatuna uzalishaji wa zana hizo ndani ya nchi? Kwa hiyo, ningeshauri kwamba walau tufufue kile kiwanda cha zana za kilimo Mbeya au tujenge kingine kipya ili mradi uzalishaji wa hizi zana za kilimo upatikane ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nimekuwa nikisema mara nyingi sana kuhusu zao la zabibu. Bahati mbaya sana kila majibu yanapotolewa wanasema zabibu iko katika Bodi ya Mazao Mchanganyiko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zabibu ni zao la kipekee kwa hapa Tanzania linalimwa katika Mkoa wa Dodoma na halilimwi Dodoma yote. Unajua kuna watu hawaelewi wanafikiri Dodoma nzima ukipanda zabibu zinakubali, hapana, zabibu zinalimwa eneo kidogo la Kongwa, baadhi ya maeneo ya Dodoma Mjini, baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Chamwino na Wilaya ya Bahi. Kwa hiyo, unaweza kuona ni muhimu sana hata kutambuliwa tu yale maeneo ambayo zao hilo linastawi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tumekuwa Makao Makuu ya Nchi unaweza kukuta ardhi ileile inayostawi zabibu watu wakaenda kulima na wakaweka vitu vingine tukajikuta hata maeneo tunayotegemea kuzalisha zabibu yakakosekana. Kwa hiyo, kutambua tu peke yake kwamba eneo hili linaweza kustawi zao hili na eneo hili linaweza kustawi zao hili ni jambo zuri na litasababisha wakulima wetu waweze kuinuka na kuendelea kupata uchumi mzuri. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Juma Selemani Nkamia, mdogo wangu kwa siku mbili kwa kuzaliwa. Nikimtangulia mimi kwa siku mbili zinazofuata yeye, taarifa nimeipokea.

Mheshimiwa Spika, haya ndiyo mambo ambayo tunayaelekeza. Mwanzoni kila ukanda ulikuwa una zao lake la biashara, huku wanalima pamba, huku wanalima korosho, huku wanalima kahawa, ule utaratibu ulikuwa mzuri sana kwa sababu wananchi walikuwa wanaangalia ardhi na mazao yanayostawi kwenye ardhi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima tukubaliane dunia nzima ina vitu vikubwa viwili, kuna nuru na kuna giza. Kama unataka kufanya vizuri lazima uvitambue sio kwa sababu humu ndani tuna upande wa Chama Tawala na upande wa Upinzani ndiyo upinge kila kitu. Hivi Mheshimiwa Rais analetewa na Wizara juu ya mchakato wa kufuta shamba fulani ambalo limemilikiwa kwa miaka mingi, watu maskini wa eneo hilo wamekosa maeneo ya kulima, Rais anafuta, leo Mbunge unasimama kutetea kwamba Rais asifute. Mimi sielewi hapa tunatoa wapi hoja hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wabunge wanaokataa maskini wa nchi hii wasipewe ardhi hebu wajitambulishe kwa majina yao na majimbo yao ili wananchi wapate kuwafahamu. Tunaposema Rais anatetea wanyonge tunamaanisha na Mheshimiwa Rais hizi Wizara zote zilizotajwa katika hizi taarifa ni Wizara ambazo zinaweza kumsaidia sana katika vita hii ya uchumi. Maana tunapozungumzia vita hatuzungumzii ya kuuwana moja kwa moja kuna vita ya uchumi sasa, kilimo kikifanya vizuri, viwanda vikafanya vizuri, utalii ukafanya vizuri, maisha ya Watanzania hayatategemea tena wafadhili, tutakuwa huru hata kujitungia sheria zetu wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzijuzi mmeona umaskini mbaya sana, tunalazimishwa tukubaliane na sheria ambazo zinakiuka hata mila na desturi yetu kwa sababu tu tunasaidiwa. Mambo mengine hata ukiyatazama kwao hao walioendelea kidemokrasia hayapo.

Mheshimiwa Spika, juzi nilikuwa na-Google kama Mheshimiwa Musukuma rafiki yangu kuangalia tangu Uchaguzi Mkuu wa Marekani umepita Hillary Clinton hajafanya mkutano hata mmoja wa kushukuru wananchi lakini ndiyo haohao wa kwanza kusema sisi hatuna demokrasia. Mbona Marekani walioshindwa hawazunguki kufanya mikutano ili kuwashukuru wananchi? Haya mambo unayona kwetu tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine, Trump, Rais wa Marekani, hataki ushoga, hakuna mtu anamuuliza, hakuna mtu anampinga, watu wamenyamaza kimya, lakini sisi kwa sababu ya umaskini wetu kila kitu kibaya wanataka kutuletea. Kwa hiyo, Serikali ikijikita kuinua wakulima, kukuza sekta ya utalii tunaweza kupata pesa nyingi ambazo zitasababisha tupange maendeleo yetu wenyewe bila kufuatwafuatwa na mtu mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi leo hii Wabunge tunazungumzia umeme wa Stiegler’s Gorge wakati tayari saini zimeshawekwa, huu ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu sana. Saini zimeshawekwa, mikataba imeingiwa, halafu sisi tunataka kuonesha kwamba eti kuna tatizo, tatizo liko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeelimishwa…

SPIKA: Tena Mheshimiwa Lusinde na Spika nilialikwa nikashuhudia kwa niaba yenu wote. (Makofi)

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Kwa niaba ya Bunge hili. Maana popote anapoalikwa Spika anaalikwa kwa niaba ya Bunge. Kwa hiyo, Bunge lilishuhudia utiaji saini na ujenzi unaanza, tunaanza kuzungumzia eti inawezekana kuna matatizo, jamani tumetumwa au ni akili yetu sisi wenyewe? Mbona tunazungumza kama Bunge la Ujerumani hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana Wizara ya Maliasili na Utalii mmeboresha mazingira. Jimboni kwangu kule tembo wameongezeka mpaka juzijuzi walikunywa pombe za wananchi. Kulikuwa na mnada pale tembo wawili wakakuta wananchi wangu wanakunywa, wananchi wakakimbia tembo wakanywa pombe, ilikuwa shughuli. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa sijawahi kushuhudia tembo akilewa balaa lake ni kubwa. Kwa hiyo, tunachokiomba walau Serikali sasa kupitia KDU itengeneze ulinzi wa kuzuia wanyama waharibifu ili wasiwafikie wananchi na kuchukua pombe yao. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)