Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.
Napenda nianze kwa kuzipongeza sana Kamati zote mbili, lakini nitachangia pande zote mbili nataka nianze na uvuvi. Tuliwahi kulalamika sana wakati wa operesheni lakini tukafika mahali tukakubaliana na Mheshimiwa Waziri na tukaamua kumuunga mkono na zoezi la wavuvi haramu kwa kiasi fulani limepungua.

Mheshimiwa Spika, sasa baada ya kutoka kwenye ule uvuvi ambao Mheshimiwa Waziri alikuwa anaukataa, hata huu uvuvi tulionao tena kuna tatizo kubwa. Sasa hivi kwenye ziwa Wizara imeweka masharti kwamba unavua mwisho sentimita 50 mpaka 85, lakini mitego ile ambayo Wizara ilipendekeza ukiitupa kwenye maji inavua mpaka sentimita 100 na kuendelea, sasa inaonekana tena mtu akivua sentimita 86 na lenyewe ni tatizo anatakiwa kuadhibiwa na kutozwa faini ya mamilioni. Sasa tunashindwa kuelewa, labda leo Mheshimiwa Waziri atakaposimama aniambie kwamba hiyo mitego uliyotaka tuitumie tutumie njia gani tukiitupa kule ndani isichukue zile sentimita 86 iwe inabagua zile unazozitaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi siyo kwamba haya masharti uliyoweka watu hawavui, nataka nikwambie Waziri Mpina umeongeza magendo makubwa kwenye ziwa letu. Hii mitego unapoitupa kule kwenye maji wanapopata wale samaki wakubwa ambao wewe huwataki na wanashikwa na mitego yako, soko lake kubwa liko Uganda na Kenya. Hata viwanda vyetu vya sasa vilivyoko huku Kanda ya Ziwa hawakubali kupokea samaki anayezidi sentimita 85, kwa hiyo, watu wanawapata wale samaki wanapeleka kwenda kuuza Uganda.

Mheshimiwa Spika, tatizo lingine hata kwenye soko la kimataifa samaki wetu wamekosa soko. Wewe ni shahidi kwenye viwanda imejaa minofu haisafirishwi kwa sababu minofu yetu ni ya samaki wachanga, wale samaki wenye afya njema wako Uganda na Kenya ndiyo wamechukua soko hilo.

Mheshimiwa Spika, nimwombe Waziri, pengine una utaalam wa kuweza kuwaelewesha wavuvi wetu kwamba mitego uliyotupa wewe mwenyewe inashika sentimita kubwa hukutaka tushike sentimita ndogo, tatizo tena limekuja kwenye sentimita kubwa. Nikushauri sana Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa utueleze.

Mheshimiwa Spika, lakini pia Waziri umeharibu biashara ya bondo. Wewe mwenyewe unafahamu unaposhika samaki mwenye bondo kubwa na soko lake ni kubwa. Wachina ambao walikuwa wananunua mabondo ya Tanzania sasa wamehamia Uganda na Kenya, nadhani ukija hapa utatoa ufafanuzi ili tuweze kukuelewa.

Mheshimiwa Spika, lakini suala la pili niliwahi kusema hapa mpaka nikatoa machozi kuhusiana na suala la ufugaji Mheshimiwa Maghembe akiwa Waziri. Nashangaa sana mtu ambaye hatampongeza Mheshimiwa Rais, labda wale wanaokaa mijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama mnakumbuka vizuri nilisema kuna watu humu wanafuga mbwa na nyanya, hawawezi kuona thamani ya mashamba kwa sababu vitu vinakaa kwenye mazingira ya binadamu. Kwa hiyo, nataka niseme hivi kwa mtu yeyote anayetoka jamii ya wafugaji, anayetoka vijijini asipompongeza Mheshimiwa Rais kwenye hili suala la kuruhusu watu wamegewe maeneo ni mtu wa ajabu na Watanzania mnaotutizama kwenye TV hawa ndiyo Wabunge wenu wanakaa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwenye kazi nzuri aliyoifanya, lakini sisi tunaotoka vijijini tunasema Mheshimiwa Rais tunakupongeza sana na ndiyo kilikuwa kilio cha wanyonge unaowatetea na ikiwezekana endelea na maeneo na mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, linguine ni suala la wakulima. Sisi tunaotoka kwenye jamii ya wakulima yako matatizo mengi sana ya mbolea. Unaweza ukakuta sasa hivi wakati wa kupanda mbolea inakuja mwezi Juni au Novemba wakati mnavuna. Mimi najiuliza Mheshimiwa Rais mimi namhurumia wakati mwingine atapasuka hata kichwa. Wakati akipokea Taarifa ya CAG mwaka jana alizungumza akaielekeza Wizara msiagize mbolea ya nje chukueni Minjigu, Minjingu godown zimejaa mbolea hamnunui. Mbolea ya kupandia inakuja wakati wa kuvuna mbolea ya kuvuna inakuja wakati tumeshamaliza hata kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa napenda Waziri akija hapa atuambie na bahati nzuri Mheshimiwa Rais alikuwa live wakati akielekeza Wizara kwamba lazima mkanunue mbolea ya Minjingu kwa sababu mbolea ya Minjingu ni ninyi wenyewe mmeipima mkaiona inafaa na mkatoa TBS. Utaalam wenu wenyewe tena mnaona kama haifai mnaenda kuagiza mbolea ya nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ukiangalia kwenye hii mbolea, mimi ni mkulima ndiyo maana nalalamika, ukienda Kenya, Uganda na Burundi wao hawaagizi mbolea ya nje wanaagiza mbolea ya Minjingu ambayo sisi tunaiona haifai. Sisi tunang’ang’ana kuagiza nje huku tunasema Serikali ya Viwanda. Jamani naomba Waheshimiwa Mawaziri husika mkija hapa mnipe majibu na sisi tunataka kumuunga mkono Mheshimiwa Rais kweli anachokitaka kifanyike kutengeneza viwanda vyetu vya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesikia watu wakilalamika hapa kuhusiana na suala la mashamba. Bado nazungumza tu yaleyale, unajua watu tunapishana kuna watu wanatoka mijini, kuna ghorofa, wengine wanakaa juu, wengine ghorofa ya tatu, sisi ambao tunakaa plot kwa plot hakuna mtu atawasikiliza na mnajipaka nuksi, watu wakiwasikia mnang’ang’ana mashamba yarudi kwa mabepari hiki kitu Watanzania hawakikubali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niseme mimi ni mwana CCM mzuri nilikuwa Mwenyekiti. Ukisoma ukurasa wa 41 kwenye Ilani ya CCM, kifungu cha 6 kuna baadhi ya watu humu, wana CCM wenzangu wanapiga midomo kwamba tutetee mashamba, wao ndiyo walikuwa viongozi na ndiyo walioanza kuisemea Ilani hii ikiielekeza kwamba tutakapochukua Serikali tuangalie mashamba makubwa tuyafute tuyapeleke kwa wananchi, leo tena wamegeuka ya kwao yaleyale wameyageuza tena.

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, naikubali hiyo taarifa. Tunataka Wabunge wazalendo kama hawa wanaoijua vizuri Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilichokuwa nasema ni Ilani ambayo imeelekeza haya yafanyike Serikalini. Nami nataka niwape moyo wanaosimamia hizi sheria, Waziri Lukuvi na wenzio futeni mashamba, futa, yaani hata yale mengine futa. Haiwezekani watu wanachukua hati wanaenda kukopea nje ya nchi wanapata hela wanaenda kuwekeza Dubai sisi tunaachiwa mapori huku. Naomba wale wanaosimamia Wizara hii futeni wala msiogope. Najua yatakuja maneno ya kusema mmehongwa, mmepewa rushwa, ukiwa unatekeleza sheria kuhongwa ni maneno ya kukukatisha tamaa, futa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)