Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata nafasi ya kuchangia Kamati zetu hizi mbili; Kamati ya Maliasili na Utalii na Kamati ya Kilimo ambazo zinabeba Wizara muhimu sana. Kamati ya Kilimo peke yake mchango wake kutoka kwenye idara ambazo inazisimamia katika Pato la Taifa ni takribani asilimia 33 na tunaambiwa sekta ya utalii peke yake inachangia asilimia 17 katika pato la Taifa. Kwa hiyo, tuna hoja nyeti sana ambazo naamini kwamba Wabunge tunazitendea haki pia.

Mheshimiwa Spika, nitaanza na jambo la uelewa kidogo, jana na juzi tumekuwa na mjadala hapa kuhusiana na masuala ya biashara ya korosho na kulikuwa na ubishani kidogo kuhusu masuala ya kangomba na kadhalika. Kuna jambo ambalo naomba Waheshimiwa Wabunge tulitazame, leo hii sisi tumeweka nguvu kubwa Kagera kuzuia kahawa yetu isiende Uganda. Kahawa yetu ikishakatiza tu mpaka wa Uganda, kule Uganda hawana shida yoyote. Ndiyo maana leo ukitazama mauzo ya kahawa nje, pamoja na kwamba Uganda eneo lake la kahawa ni dogo lakini wanauza tani 306,000 za kahawa kwenye soko la dunia wakati sisi tunasuasua kati ya tani 100,000 na 137,000, sina uhakika sasa hivi tumeuza kiasi gani, lakini Uganda mara zote wanauza nje mara mbili. Uganda sasa hivi ni namba nane duniani na namba moja Afrika kwa kuuza kahawa nje. Kahawa ile ambayo Waganda wanauza, sehemu yake inatoka Tanzania, Burundi, Rwanda na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi leo anaweza akasimama Mkuu wa Wilaya akaita na vyombo vya habari kutangaza kwamba eti amezuia korosho kutoka Msumbiji kuja Tanzania. Nadhani ifike wakati viongozi wetu ngazi za chini na naomba radhi, nitatumia neno tuache ushamba. Re-export ni biashara kubwa duniani, sisi tunapaswa kuweka incentives kama kuna watu wana bidhaa zao ambazo zinauzwa wakazileta tukaziuza sisi zita-appear kwenye balace of payment yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana leo United Arab Emirates wanauza nje bidhaa za thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 295. Katika hizo re-export ni Dola za Kimarekani bilioni 137 yaani ni bidhaa za nchi zingine zikifika pale Dubai au Abu Dhabi na kadhalika, wanazifanyia repackaging wanauza nje, inaitwa re-export. Kwa hiyo, naiomba Serikali izungumze na hawa Wakuu wetu wa Wilaya wa mipakani huko waachane na hayo mambo, waache tabia za kishamba, kama mali inakuja kwetu acha iingie tutaiuza sisi dola zitaingia kwetu. Kwa hiyo, naomba hili jambo tulitazame vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pili na naomba hili nimu- address Waziri wetu wa Kilimo, rasimisha kangomba, ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kwamba tunaondoa ulanguzi. Vyama vyetu vya Ushirika havina incentive ya kuwawezesha wakulima wetu wapate mikopo midogomidogo ya kuweza kushughulika na kero zao ndogondogo. Ndiyo maana ukienda Kagera kule na rafiki yangu Naibu Waziri wa Kilimo anajua kuna Obutura, ndiyo kangomba hiyo ni majina tu tofautitofauti, rasimisheni haya mambo, wapeni leseni. (Makofi)

Wapeni mizani, wataacha kufanya kazi ya ulanguzi na itatusaidia korosho, kahawa au pamba nyingi kukusanywa na tutakuwa hatuna mambo haya.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani leo mtu ambaye anafanya brokerage Dar es Salaam Stock Exchange anaonekana ni mtaalam kwelikweli, halafu unakwenda unamdhalilisha kangomba unamuita mlanguzi, unamuita nini, haya mambo yamepitwa na wakati. Rasimisheni, wapeni leseni na mizani tuweze kufanya kazi vizuri, matatizo mengine yatakuwa yamekwisha bila shida yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ninalotaka kulizungumzia, sasa hivi tuna wakati mgumu sana, ni kweli tuna miradi mikubwa inafanyika, ni kweli kabisa lakini wachumi wenzangu hapa watanisaidia. Duniani kote pale ambapo hali ya uchumi ni mbaya, kuna recession (mdororo), Serikali hutekeleza miradi mikubwa ili watu wapate fedha kuongeza aggregate demand ili uzalishaji uweze kurudi. Sisi hapa kwetu tuna miradi mikubwa kwelikweli lakini aggregate demand haionekani, haiongezeki ni kwa nini? Kwa sababu katika hali ya kawaida ilitakiwa leo Watanzania wawe na furaha kwelikweli kwa sababu tuna miradi inayoingiza fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kwa sababu miradi yetu inatoa fedha kupeleka nje, miradi yetu ni outflows siyo inflows ndiyo maana kuna shida, ndiyo maana liquidity ni problem katika nchi yetu. Ndiyo maana tunazungumzia sijui inflation kwamba imeshuka na nini, ni inflation ambayo inatokana
na watu kutokuwa na fedha za kununua bidhaa, ndiyo maana inflation iko very low. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana ndani ya miaka mitatu, kwa mujibu wa taarifa ya World Bank na jana Mheshimiwa Komu amezungumza hapa, Watanzania milioni mbili wameingia kwenye poverty. Kwa sababu mifumo na maamuzi yetu ya kiuchumi sio ambayo yanakwenda kuwasaidia wale wadogo. Fine, tuna miradi mikubwa tutashangilia lakini hii miradi mikubwa haitengenezwi kwa namna ambayo itamfanya mpaka mtu wa chini aweze kupata hali nzuri ya uchumi.

Mheshimiwa Spika, suala lingine naomba nipate maelezo ya Serikali, tunaambiwa kwamba Tanzania Agricultural Development Bank imepata mkopo kutoka African Development Bank ndiyo fedha ambazo zinatumika kwa ajili ya kununua korosho. Sisi ni watu wazima humu ndani, leo hii nenda kwenye website ya African Development Bank angalia kama kuna credit inayokwenda Tanzania Agricultural Development Bank, hutaona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii dakika chache kabla sijaanza kuongea nimetazama na nimekuta mara ya mwihso ni credit ya tarehe 24 Januari, 2019. Serikali itueleze hizi bilioni 900 zimetoka wapi? Mmekwenda Benki Kuu kuondoa kwenye deposits za Mashirika ya Umma kwa ajili ya kupeleka Agricultural Development Bank na kwenye Bodi ya Mazao Mchanganyiko kwa ajili ya kununua korosho? Haitakuwa mbaya lakini mtuambie badala ya kudanganya.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu mlituambia tutanunua korosho, tutazibangua, tutauza nje, tunauza korosho ghafi kama vile walivyokuwa wanafanya watu wengine. Naomba sasa hivi tuondokane na hiki kitu cha kudanganyana na kutoelezana ukweli. Naomba Serikali itueleze leo fedha zile zimetoka wapi kwa sababu fedha za African Development Bank pale hazipo, sasa mtueleze Benki Kuu mmezichukua kutoka kwa nani, kutoka kwenye akaunti zipi na taratibu zipi ambazo zitatengenezwa kwa ajili ya kuzirejesha fedha hizo, kwa sababu tunajua Benki yetu hii ya Kilimo haina mtaji huo wala hizo deposits za kuweza kununua hizo fedha ambazo zinatakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ambalo ninapenda kulichangia ni hili suala la TFS. Kamati ya Utalii imezungumzia kuifanya TFS iwe Mamlaka kutoka kuwa Wakala, naunga mkono ukurasa wa 13 wa Kamati hiyo kwa sababu wanashughulikia misitu mingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yale matatizo ambayo yalitokea Iringa juzi ya miti ile ya watu wa REA na makampuni yanayotutengezea umeme kuzuiwa kwa ajili ya ushuru wa Halmshauri na kadhalika, ile ni double payment kwa sababu TFS already imeshalipa zile cess lakini pili, Mkuu wa Mkoa akaagiza tena kwamba Halmashauri zilipwe tena, matokeo yake ni nini, sisi ndiyo ambayo tunaathirika tunakosa nguzo kwa ajili ya umeme. Tukiipa TFS mamlaka ya kutosha ikawa mamlaka inaweza ikasaidia kuondokana na hizi kero nyingine ambazo zimetokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, nakubaliana na mapendekezo ya Kamati zote mbili ambazo zimeleta taarifa zake hapa na naamini kabisa kwamba zitaweza kufanyiwa kazi na Serikali italeta taratibu za utekelezaji wake. Ahsante sana. (Makofi)