Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami napenda niungane na wajumbe wenzangu kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati ambao wamewasilisha taarifa zao katika Bunge letu asubuhi ya leo. Kwa kuwa muda wangu ni mfupi, napenda nijielekeze moja kwa moja katika masuala ambayo nimejipanga kuyachangia.

Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza ni uvuvi. Eneo la uvuvi kwa kweli Serikali haijawekeza ipasavyo. Mara nyingi tumekuwa tukijielekeza kwenye operesheni zaidi kuliko kuwawezesha wavuvi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leseni za uvuvi zinafuata kalenda ya mwaka yaani Januari – Desemba. Januari ilivyoanza tu hata tarehe 15 bado operesheni za kuwasaka wasiokuwa na leseni zimeanza na kuwatoza faini kubwa zaidi ya shilingi milioni 1 kwa mvuvi mmoja wakati faini inaanza kutolewa baada ya mwezi Machi, kuanzia Januari, Februari mpaka Machi wanatakiwa wavuvi wakate leseni lakini mwaka huu kabla hata ya Februari operesheni imeanza, wavuvi wangu wa Naumbu, Msanga Mkuu, Mkubiru na Msimbati wamepigwa faini mpaka shilingi milioni 4, hali kwa kweli kule ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri pamoja na kwamba tumezungumza naye, walikuja wavuvi pamoja na Waheshimiwa Madiwani kutoka Kilwa, ameahidi kwenda Kilwa siku ya Jumapili. Nimuombe Mheshimiwa Waziri asiishie Kilwa Kivinje na Kilwa Masoko, katika ziara yake aende mpaka Mtwara, Msanga Mkuu, Mkubiru, Msimbati, Naumbu na Mgau kwa sababu kero hiyo kwa kweli ipo kwa wavuvi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutoa ushauri kwa Serikali, naomba wafanye utafiti wajue ni nyavu zipi zinazoweza kuvua dagaa na baada ya kuzijua Serikali yenyewe iingie mkataba na viwanda wanunue hizo nyavu, waweke mawakala wa kuuza hizo nyavu Kilwa, Mafia na Mtwara ili wavuvi wetu ikiwezekana wakopeshwe na wanaoweza wanunue ili kuondoa hii sintofahamu ya kila siku tunawaelekeza nyavu za kununua halafu baada ya siku mbili tunaenda kuzikamata hizo hizo tunazichoma moto. Kwa hiyo, niiombe Serikali yenyewe kama inavyofanya kwa pembejeo za kilimo na katika maeneo mengine na huku kwenye uvuvi yenyewe itafute mawakala wa kusambaza zana za uvuvi ambazo wao wamezipitia na kuzithibitisha na kuziona kwamba baada ya utafiti wao zinafaa kuvua dagaa, pweza na kamba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huo ndiyo ulikuwa mchango wangu wa kwanza kwa kweli wavuvi wetu hawana amani lakini ni eneo ambalo kwa kweli kama Serikali hatuwawezeshi. Ukiacha mradi wa MANCEP ambao ulipita kipindi hicho, hakuna mradi mwingine wa uhakika ambao umekuja wa kuwawezesha wavuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nililetewa na Naibu Mheshimiwa Waziri injini ambazo kama Wizara iliona wangeweza kuzitoa kwa ruzuku kwa wavuvi. Nilivyoenda kuwatangazia wavuvi wangu waliniambia hizo mashine ni ndogo sana kwa kwenda nazo baharini. Sasa sijui wakati Wizara wananunua waliwashirikisha vipi wavuvi wetu.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo nilitaka nilichangie ni ununuzi wa korosho. Tulifurahi sana Serikali ilivyoamua kununua korosho kutoka kwa wakulima wetu na bei ambayo iliitoa lakini muda ambao tunauchukua katika mchakato mzima wa kununua korosho kwa kweli ni mrefu mno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kawaida ununuzi wa korosho unaanza mwezi Oktoba ikifika Desemba wale wanunuzi wanavyokwenda Chrismas inakuwa ni kama ununuzi umeishia, wanavyorudi sikukuu za mwaka mpya labda minada ikiendelea ni mitatu, minne na ununuzi unakuwa umeisha. Sasa hivi mpaka mwezi Februari hata asilimia 60 ya ununuzi haijafikiwa. Wamehakiki zaidi ya tani 200,000 lakini waliolipwa hawajafika hata tani 150,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, cha kushangaza katika takwimu zetu tunaambiwa katika vyama 605, wameshalipa vyama 600 lakini ukiangalia tani zilizouzwa hazijafika hata tani 150,000. Sasa sijui hizo takwimu zimekaaje, watatuambia wanaokuja kutujibia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine, Halmashauri zetu zote za Kusini ushuru wa korosho ndiyo chanzo chetu kikubwa cha mapato. Mpaka sasa hivi tunavyozungumza mwaka wa fedha 2018/2019 bado miezi mitano tumalize na hatujapata ushuru na hatuna uhakika kama tutapata na hatujui kama tutapata tunaupata lini. Niiombe Serikali suala la ushuru kama ambavyo wadau wengine wamelipwa na kwa kawaida ileile Sh.3,300 ambayo Serikali ilisema itanunua kutoka kwa wakulima, wadau wote wangepata pesa zao kutoka kwenye pesa zilezile bila hata kuhitaji bajeti nyingine.

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali ijitahidi kuhakikisha wadau wote wanaohusika katika ununuzi wa korosho na wakulima wetu hasa wakubwa maana yake wakulima wakubwa mpaka sasa hivi hawajaanza kulipwa. Imekuwa kama ni adhabu sasa kuwa mkulima mkubwa wa korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)