Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Awali ya yote nikitakie heri Chama cha Mapinduzi katika siku yake ya kuzaliwa, miaka 42 siyo mchezo. Naamini tutaendelea kuwaongoza Watanzania ili wafikie ndoto zao za maendeleo. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, niweze kutoka moyoni kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kauli ambayo ameitoa hivi karibuni kwa wananchi wetu ambao wanaishi katika hifadhi mbalimbali katika vijiji vyao, ambao walikuwa wakipata matatizo makubwa na hifadhi zetu, lakini pia wakulima mbalimbali ambao walikuwa wanatumia maeneo ya vijiji lakini walikuwa na migogoro na hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili halidhihirishwi tu na Wabunge tunaotokana na maeneo hayo, lakini limedhihirishwa na wananchi wetu ambao kwa namna moja au nyingine wamejitokeza hadharani kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kauli yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilichogundua ni kwamba kwa kauli hii, anayevaa kiatu ndiye anayefahamu ni wapi mwiba unamchoma. Kuna miongoni mwetu ambao wanabeza kauli ya Mheshimiwa Rais, lakini kwa wale ambao miaka yote tumekuwa tukiomba Serikali iangalie hili, kwa kweli tumepokea kwa moyo wa faraja na wa pongezi kwa Serikali na kwa Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miaka mitano iliyopita, nilikuwa nikiongelea vijiji vya Gedhamaru, Gijedabung, Ayamango na maeneo mengine katika Mkoa wetu wa Manyara. Tumeona sasa wale wafugaji na wakulima jinsi ambavyo wameguswa na kauli ya Mheshimiwa Rais. Naomba nimtie moyo aendelee kutumikia Watanzania bila kuchoka, kwa sababu maamuzi anayofanya yanawagusa na yanagusa maisha ya wanyonge. Tunamshukuru sana. Ombi langu kwa Serikali, watusaidie mapema. Wizara husika waweze ku- identify hayo maeneo mapema ili wale wananchi sasa watulie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana kauli ya Mheshimiwa Rais ni jambo moja lakini pia utekelezaji ni jambo lingine. Nina imani na Serikali yangu na ninaamini kabisa kwamba hili litafanyika mapema na hatutamwangusha Mheshimiwa Rais kwa kauli nzuri aliyotoa kwa Watanzania ambao kwa kweli wamepokea kwa moyo wa shukrani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie kwa ufupi changamoto ambazo tumeziona kwenye hifadhi zetu. Mimi ni Mjumbe wa Kamati hiyo, tunafahamu hifadhi zetu ambazo zinapatikana Kusini mwa Tanzania ukiachilia mbali za Kaskazini mwa Tanzania, zimekuwa na mchango kidogo kwenye Bajeti yetu ya Kitaifa lakini kwenye pato la Taifa ni kwa sababu ya changamoto ambazo wamekuwa wakikutana nazo.

Mheshimiwa Spika, kwenye kitabu chetu cha Kamati, wamezungumzia au tumezungumzia changamoto za Hifadhi ya Mikumi, jinsi ambavyo ile barabara kuu wanyama wamekuwa wakigongwa zaidi ya wanyama 100, kwa mwaka tunapoteza wanyama hao. Pia hifadhi hizi au hii ya Mikumi imekuwa ikipata kuchafuliwa kwa sababu wanapopita panakuwa hapana doria ya kutosha na hata zile doria hazitoshelezi na wanaopita barabarani wanakuwa watupa uchafu na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Ruaha inahitaji kuangaliwa kwa karibu. Nafahamu kwamba hifadhi zetu zinachangia zaidi ya asilimia 17 katika bajeti yetu na katika pato letu la Taifa, lakini kama hifadhi hizi za Kusini zisipopewa kipaumbele na zikasaidiwa kwa karibu kwa kuondoa zile changamoto wanaweza wakawa wanaendelea kurudi nyuma katika mapato ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa Hifadhi ya Ruaha, naiomba Serikali yangu na ninaamini ni Serikali sikivu, hii barabara kutoka Iringa mpaka hifadhini zaidi ya kilometa 100 ni ombi la muda mrefu kwamba sasa iweze kuwekewa lami. Naamini katika mpango mzima uliopo wa REGRO ambao unalenga kukuza utalii na kusaidia hifadhi zetu kwa upande wa Kusini, unaoendeleza ungeweza kusaidia. Naiomba pia Serikali waweze kuharakisha kusaini mkataba huo wa REGRO ili isaidie katika kuondoa changamoto ambazo ziko kwenye hifadhi zetu.

Mheshimiwa Spika, naomba Wizara husika isaidie pia kuharakisha mfano miundombinu katika hifadhi zetu, Kwa Hifadhi ya Ruaha pamoja na Mikumi na hifadhi nyingine wanatamani sana ndege zitue katika hifadhi zetu ili watalii wale ambao wanatamani kufikia kule waweze kufikia.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu siyo watalii wote ni vijana ambao wanaweza wakastahimili kutembea katika barabara zetu. Kuna watalii ambao ni wazee, wao wanahitaji kutua moja kwa moja katika hifadhi zetu. Kwa hiyo, naomba pia Serikali iangalie kwa karibu sana ili waone pia tunakuwa na viwanja vya ndege katika hizo hifadhi.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, pia naiomba Serikali, sisi tuna hifadhi yetu ya Tarangire katika Mkoa wetu wa Manyara ambako geti la Babati – Tarangire kupitia Babati Mjini pale, sisi tumesharidhia na geti limeshafunguliwa. zaidi ya kilometa 20 ni za rough road. Naiomba Serikali na asubuhi pia mlinijibu swali la bypass, mmeahidi kushughulikia. Tukipeleka lami pale, tutasaidia watalii wetu waweze kufikia hizo hifadhi.

Mheshimiwa Spika, naamini changamoto ni nyingi katika hifadhi zetu, lakini Serikali yetu ni sikivu na inaweza ikafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo nilitaka niipongeze Serikali kwa moyo wa dhati na ninampongeza Mheshimiwa Waziri pia, ni suala la mradi huu wa kurasimisha vijiji na upimaji ambao unafanyika kwa majaribio katika Mkoa wetu wa Morogoro na katika Wilaya za Malinyi, Ulanga na Kirombero, kwa kweli ni mradi uliosimamiwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa moyo wa dhati, huu mradi umesaidia wananchi kumilikishwa maeneo yao na wamepata Hati. Tumefika site, tumeona ni kwa kiasi gani hata akina mama wamepatiwa Hati, siyo wanaume tu. Tumeona ni kiasi gani wale wananchi wameshirikishwa.

Mheshimiwa Spika, nisipoipongeza Serikali kwa mradi huu, nitakuwa sijitendei haki. Nami naomba Serikali itusaidie, kuna fedha za ndani zaidi ya shilingi bilioni saba, lakini ni shilingi milioni 710 ndiyo zimetolewa. Mheshimiwa Waziri, pamoja na kazi nzuri, zikitolewa zile shilingi bilioni saba ambazo ni fedha za ndani, zitatusaidia kukamilisha ule mradi. Huo mradi sasa Mheshimiwa Waziri uweze kupelekwa kwa nchi nzima. Naamini nia ya Serikali ni njema sana, lakini tatizo lako ni bajeti.

Mheshimiwa Spika, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu, tunapoelekea kwenye Bunge la Bajeti, Wizara hii tuipatie fedha kwa sababu wanapowapimia wananchi wakapata haki zao migogoro ya ardhi itakuwa imeisha katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nashukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)